Tumejifunza nini toka Kenya?

Justice David Maraga

Justice David Maraga

Hivi karibuni mahama kuu ya nchini Kenya imetengua matokeo ya urais na kuagiza uchaguzi kurudiwa baada ya siku sitini kama katiba inavyoelekeza. Matokea haya ya urais yametenguliwa baada ya kuonekana kasoro mbalimbali katika uchaguzi ikiwamo matumizi mabaya ya mtandao wa uchaguzi (IEBC) na kutozingatia matumizi sahihi ya karatasi 34A na 34B.

Kwanza nianze kwa kuwapongeza majaji wa mahakama kuu ya nchini Kenya kwa kuamua kusimamia haki na kutoruhusu kubebwa na wimbi la uonevu linalotumiwa na sheria za kiafrika. Ni ukweli usiopingika ya kuwa nchi nyingi za kiafrika na kwingineko duniani hutumia sheria kama chombo cha muondelezo wa unyonyaji na ukandamizaji kwa wanyonge na wavuja jasho maskini.

Ila tumeshuhudia Kenya majaji wameamua kufuata ueledi na kuangalia maslahi mapana ya nchi. Kwa hili walilolifanya wakenya Tanzania yatupasa kujifunza na kuangalia ni kwa namna gani tunaweza kufanya mihimili yetu kuwa imara na yakujitegemea.

Hebu tutizame kile ambacho Kenya imetufundisha katika uchaguzi huu na maamuzi ya mahakama kuhusu matokeo ya uchaguzi.

Kwanza kabisa Kenya walipitia mchakato wa kubadili katiba yao ili kurekebisha mapungufu yaliyokuwemo. Mabadilko ya katiba ndio yameiwezesha na kuipa nguvu mahakama kusikiliza kesi hii baina ya NASA na JUBILEE ambapo NASA wamelalamikia uchaguzi uliokiukwa na kumpatia ushindi Rais Kenyatta wa JUBILEE.

La kuangalia zaidi sio tu kubadilishwa katiba ambayo ni muhimu, ila la pili ni majaji kuamua kutenda haki. Ni muhimu kutambua ya kuwa kwa mifumo yetu ya demokrasia uchwara za Afrika watawala hawapendi kupoteza uongozi hivyo hutumia mbinu zozote kushinda hata kwa kuamuru mahakama itoe matokeo yatakayoipendelea serikali iliyoko madarakani.

Raila O. Odinga

Raila O. Odinga

Sambamba na hili pia, ni ukweli kwamba yamkini chama dola waliiacha mahakama itende kazi yake kwa uhuru (sina hakika kama ndivyo ilivyokuwa ila ni kwa kutizama muenendo wa kesi) ndio maana mahakama ikatoa maamuzi sahihi. Ila kwa tabia za serikali zetu za Afrika mahakama zingeshinikizwa na hatimaye chama dola kikatangazwa mshindi.

Kitu kingine ambacho tunaweza kujifunza kwa hili la Kenya ni uendeshwaji wa kesi ulio wazi ambapo kila mtu angeweza kushuhudia kinachoendelea kwa kupitia runinga. Hili pia tuliona pindi kesi ya Rais wa Afrika ya Kusini Jacob Zuma ilivyokuwa ikiendeshwa mubashara kwenye runinga ya taifa.

Hii inadhihirisha wazi ya kuwa ukuwaji wa demokrasia ni pamoja na kuruhusu uwazi katika mambo nyeti katika jamii kama hili la kuonyesha kesi mubashara ili watu waweze kufuatilia na kujifunza kile kinachoendelea katika mambo makubwa yenye maslahi na nchi.

Uhuru Kenyatta

Uhuru Kenyatta

Jambo linguine ambalo tunajifunza katika hili ni utayari wa Rais Kenyata katika matokeo ya mahakama kuu ambaye alisema “In as much as I don’t agree to the court decision I respect it” kwa tafsiri yangu, kwa kiwango nisichokubaliana na maamuzi ya mahakama naheshimu uamuzi uliotolewa.

Utayari huu unaonyesha chembe za ukuwaji wa demokrasia na nia ya kutokung’ang’ania madaraka kama ambavyo tumeshuhudia viongozi wengine wa Afrika. Mfano mzuri tu ni Rais wa Burundi ambaye ameamua kubakia madarakani ili hali watu hawampendi, hii imepelekea machafuko katika nchi hiyo kwa ulafi wa madaraka.

Kitu kikubwa cha msingi tunachoweza kujifunza kutoka Kenya ni kwamba demokrasia ya kweli inazaliwa na nchi husika sio kusibiri mpaka mabepari wa Ulaya na Marekani waje kutufundisha namna ya kuwa na demokrasia ya kweli. Utayari ulianza kwa kuamua kuwa na katiba iliyotokana na wananchi wenyewe.

Baada ya wakenya kuwa na katiba mpya wakaamua kuiheshimu na kuifuata ili iwafae na kupunguza machafuko yasiyo na msingi. Ni wazi pia katiba hiyo haiwezi kuwa takatifu inabaki na mapungufu ila walau inafuatwa kama vile ambavyo ilitarajiwa.

Swali la msingi la kujiuliza sie watanzania ule mchakato wetu wa katiba umeishia wapi? Mbona hatuuzungumzii tena kama jambo la msingi katika maendeleo ya taifa letu? Ama tunasubiri mpaka watu watoke nje waje kutukumbusha ya kuwa ni muhimu kuwa na katiba mpya?

Natumaini ya kuwa katiba inapaswa kutokana na watu na ni watu pekee wanapaswa kupaza sauti zao ili kuwa na katiba tunayodhani ni bora kwa manufaaa yetu.

Nitoe rai tujifunze kutokana na majirani zetu walivyofanya na sie tuanze kudai kwa nguvu katiba ambayo tunadhani itakuwa na maslai katika maisha yetu kama watanzania.

Kwa kuhitimisha walatini wanamsemo usemao “Si isti et istae, cur non ego?” ikimaanisha kama wengine wameweza kwanini sisi tushindwe. Tujifunze kwa majirani zetu Kenya na tuanze kujenga demokrasia bora kwa Tanzania.

Na Jacob Mulikuza

Jacob, ni mtaalamu wa Sayansi ya Jamii anapatikana Dar es Salaam. 

Leave a Comment