Ni nyumbu ama nzi wa kijani?

Sikumbuki vizuri tarehe, ama niseme sikumbuki kabisa tarehe japo nakumbuka tu ilikuwa mwezi Agosti mwishoni mwa miaka ya tisini, ambapo hali ya hewa ya mji wa Marangu ilikuwa ya baridi sana. Kwa sisi ambao tunaishi mikoa yenye joto jingi, Marangu haikuwa rafiki sana. Lakini hali ya hewa katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu pale Marangu ilikuwa ya joto sana. Joto la mada na hoja. Wengi tulijikunyata na masweta mazito kujikinga na baridi iliyokuwa inazizima katika moo za mlima Kilimanjaro, lakini hoja na mabishano makali ndani ya ukumbi yalitusahaulisha ile baridi kali.

Wengi wetu tulikuwa bado vijana wadogo kwa kweli. Hata Mh. Zitto Kabwe na Mh. John Mnyika walikuwa bado vijana sana lakini machachari sana. Sio wao tu, ila kulikuwa na watu wengi ninaowakumbuka ambao baadaye walikuja kuwa wanasiasa na wanaharakati mahiri sana, kaka zangu wakina Israel Ilunde, Hebron Mwakagenda na marehemu Aman Nzugille Mahona Jidulamabambasi, na wengi wengine ambao pengine siwakumbuki hivi leo.

Zitto Kabwe

Mjadala ulihusu sana mchakato na umuhimu wa uanzishwaji wa Baraza la Vijana la Taifa. Hata sasa mchakato huu sijui umeishia wapi. Miaka michache iliyopita kabla ya mwaka 2015 nilipata mwaliko wa John Mnyika akiwa kwenye kamati moja ya bunge, pamoja na wabunge wengine wakitaka maoni ya wadau kuhusu uundwaji wa Baraza la Vijana. Mpaka sasa sioni kama kuna dhamira kwelikweli kuhusu suala hili. Nimelikumbuka tu baada ya kuona mjadala kuhusu baraza wiki chache zilizopita. Kijana mmoja ninayemfahamu kwanza alikutana na mimi, alikuwa mwingi wa hekaheka. Akasema ‘afadhali nimekuona braza. Nina jambo nataka nikushirikishe nipate maoni yako.’ Akanitanabahisha kwa jambo lake, yumkini na wengine, sikujua ni wakina nani hasa, ‘tupo kwenye mchakato wa uundaji wa baraza la vijana. Tunataka kuwe na baraza la vijana la taifa.’

Ni kijana mmoja mnakindaki  wa chama cha siasa kwenye mitandao ya mawasiliano ya kijamii. Nikafurahia wazo lake, lakini nikamkumbusha kuhusu huo mchakato, akatahayari kwamba walao nayafahamu haya yapata miongo miwili sasa. Nikamwambia, ‘ndugu ni heri kwamba huko kwenye vyama vya siasa mmeona umuhimu wa kuwapatia vijana wa kitanzania baraza lao lisilo la kiitikadi za vyama ama siasa. Ila kinachonitia hofu ni huu umilikaji wa mchakato ambao sioni kama una urari wa hisia, matakwa na ushiriki wa vijana wengine wasio wanasiasa.’ ‘Kila la heri.’

Si kwamba mimi nimekata tamaa, la hasha, lakini matumaini yanapofifia kilichobaki ni kuomba kudra tu. Ajabu wiki chache zilizopita nikaona kijana wangu huyo ameweka bandiko kwenye ukuta wake wa Facebook akiuliza maoni ya namna gani mabaraza ya vijana ya vyama vya siasa yalivyosaidia vijana wa Tanzania. Maoni yangu yalikuwa kwamba mabaraza ya vijana ya vyama yamesaidia zaidi kueneza propaganda za kichama kuliko kujali maslahi mapana ya vijana wa nchi hii.  Siwezi kusema mchango wao moja kwa moja kuhusu ushiriki na ustawi wa vijana katika muktadha mpana wa kitaifa kwa sabau sijawahi kuamini kwamba hiyo ndio dhima yao. Zaidi hutumika kama vyombo vya kuwaandaa viongozi wa vyama vyao ama kuwa mihimili ya propaganda za kisiasa ambazo hazina maslahi kwa vijana wengi. Kwangu hoja ilikuwa ni Baraza la Vijana lisilo la vyama, baraza huru kwa kila kijana, lenye ushiriki wa makundi yote bila kuegemea itikadi za kisiasa bali lenye kujali na kupigania maslahi ya vijana kitaifa.

Hoja yangu ikajibiwa na kijana mmoja ambaye aliponda akidhani baraza la vijana ni mawazo yangu binafsi. Nikamwomba akasome Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana kisha arudi tuendelee na hoja. Kilichofuata ni kejeli na matusi. Ilibidi nicheke na kusikitika tu maana nisingeweza kuporomosheana matusi mtandaoni na mtu, ambaye ima namfahamu ama simfahamu.

John Mnyika

Nikakumbuka miongo miwili hivi, kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Marangu, ambapo mtu ulikuwa na hoja ya kuchangia lakini ilibidi utumie pengine siku nzima kuipanga na kutafuta cha kusema kwa sababu hukujua useme nini hasa ili uwe na hoja nzito. Zitto ama Mnyika ambao tunawaona leo, hawakutokea kuwa wabunge mahiri wenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja kama suala la nasibu tu. Wao na wengine niliowataja hapo juu walitufanya watu tushindwe kuongea na hata wakati ulipokuwa unaitafakari hoja yako na kuichambua mwenyewe huku ukijaribu kuifanya iwe na mashiko na wakati ambapo ungejitutumua kuongea ungekuta tayari watu walishahama zamani kwenye hiyo mada.

Ilitosha kuwa msikilizaji zaidi kwa sababu ulijifunza zaidi. Tulijifunza kusikiliza na kujibu hoja kwa hoja. Kuwa makini na kuwa na taarifa sahihi, kusoma, kuchambua, kujenga hoja na kujua nini cha kusema na uchaguzi sahihi wa maneno. Katika midahalo kadhaa na nyakati nyingi ambazo niliweza kukutana na watu hawa kuna kitu niliendelea kujifunza.

Njia pekee ya kuzima hoja ya Mnyika ama Zitto popote utakapokutana naye kwenye mdahalo basi ni kupiga kelele ili usisikie, kutukana na kukejeli. Zaidi ya hapo unatakiwa ‘ujipange’ sawasawa tena kwa hoja zenye ushahidi. Sishangai sana ninapoona zile zomea zomea, najua si suala la bahati mbaya. Nachelea kusema kwamba kizazi kile kinapotea.

Kimepokelewa na kizazi cha ‘siasa za mtandaoni.’ Kizazi ambacho kinatumia muda mwingi wa kujenga hoja kwa maneno yenye kejeli. Maneno ya kudhalilisha upande mmoja na kufurahia madhila yawapatao wengine. Kizazi cha tuhuma na kulalamika.

Najiuliza umekwenda wapi umahiri ule wa vijana kujenga hoja? Nini kimeisibu jamii yetu mpaka kufikia kuwa na kizazi cha wanaojiita mahiri wa ‘siasa za mtandaoni?’

Kwa maslahi ya nani hasa! Inasikitisha kidogo kama sio sana kuona vijana wanakuwa makasuku wanaorandaranda kwenye koridi za ofisi za vyama na simu zao za mkononi ama laptop ili kupata matusi mazuri ya kuwatusi wengine kwa fadhila za uteuzi ama nafasi za kupata tonge. Ukipishana nao hoja basi wewe ni nyumbu ama nzi wa kijani. Hivi nawezaje kuwa nzi wa kijani kama hatujakutana chooni? Ama niwe nyumbu na unanibishia kama sio kwamba sote ni nyumbu ndio maana tunaelewana?

Utastaajabu kwambe miongoni mwao kuna watu wazima walioingia huu mkumbo. Lakini kuna mahali kuna watu wanafurahia sana huu ‘ujinga wetu.’ Ujinga ni mtaji mkubwa sana kwa wanasiasa laghai. Na labda ‘laghai’ ni msingi mkuu wa siasa. Kadiri watu wanavyokuwa wajinga ndivyo wengine hutumia fursa hiyo kwa azma zao.

Wakoloni walifaidika sana na ‘ujinga’ wetu (sio upumbavu), wakatulaghai kwa mikataba ya kitapeli na kubeba rasilimali zetu. Tukasaini mikataba bila kujua kusoma na kuandika. Tukauza almasi na pembe za ndovu kwa kubadilishana na shanga na vioo. Leo hii tunalaghaiwa kwa upumbavu na si ujinga tena. Vijana tunaodhamiria kwamba wawe wenye kuchambua na kujenga hoja ili watuongoze siku za usoni ndio hao wanaotumia muda mwingi kuwa makuwadi wa itikadi za kisiasa, wakitarajia takrima ya nafasi za uongozi. Mtu mwenye kupita njia zake kimizengwe atawezaje kusimama na kujenga hoja? Zaidi ya kuwa kasuku asiye na sera bali mwenye hila. Si ajabu wanasiasa wakibadilika ama kubadili mapigo na misikule ya kisiasa nayo hubadili minenguo kulingana na mirindimo ya mpiga zumari.

Kama anakulipa kwanini usicheze.

Wakatabahu.

Mudiri wa Korogwe.

Leave a Comment