Juu ya ubinafsishaji; Kongole Rais Magufuli!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli

Hivi karibuni katika ziara za Rais John Pombe Magufuli aliweka bayana namna anavyochukia ubinafsishaji wa nyenzo za uzalishaji kama ilivyofanywa na watangulizi wake. Akieleza wazi ya kuwa, watangulizi wake walifanya kosa kubwa sana kuachia nyanja kuu za uzalishaji mali kwa wawekezaji ambao wameishia kuziharibu na kuziua kabisa.

Kwangu mimi hii ni kauli bora kabisa niliyoisikia kutoka kwa Rais Magufuli, japo kunaweza kukawa na mijadala mitaani kwetu kutokana na hili. Ilhali wengine wakiamini ubinafsishaji ni kitu kizuri na wengine tukiamini ubinafsishaji ni kitu kibaya.

Tukianza na wale wanaodhani ubinafsishaji ni kitu kizuri, wanaamini kabisa ubinafsishaji umeleta fursa nyingi katika maisha, wanadhani kumekuwa na urahisishaji wa upatikanaji wa bidhaa na huduma na pia wanaamini kumekuwa na uwezekano watu kujikita katika uhuru wa kufanya yale yatakayo kwa uhuru kama soko huria linavyojipambanua.

Wakati Rais Mwinyi akiingia Madarakani mwaka 1985 alipatiwa jina la ‘Mzee Ruksa’ kwa kile watu walichoamini ahueni ya kufanya vile watakavyo na kukaribishwa kwa soko huria. Watu walishangilia kwani waliona tofauti na ahueni ya maisha ukilinganisha na enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Lakini swali la msingi la kujiuliza hapa je, soko huria tunalolishangilia na kuliimbia ngojera za kulisifu kupitia ubinafsishaji na wawekezaji limeleta tija mpaka sasa?

Hoja mbalimbali zitaibuka katika swali hili ikitegemea uko katika kundi gani na unafaidika vipi, ukitokea kundi la walalaheri utaona soko huria lina tija za kutosha ila ukitokea kundi la walala hoi hautoona tija za soko huria hata kidogo.

Rais Magufuli ametukumbusha madhila ya ubinafsishaji kwa kugusia kidogo swala la mitumba na akieleza bayana ni kwa namna gani viwanda vyetu vya nguo vilikufa kwa kuwa tulishakuwa na uhakika wa kupata nguo za gharama rahisi kutoka kwa mabepari wale baada ya kuzivaa.

Ubinafsishaji na soko huria unapigiwa kelele na Benki ya Dunia pamoja na IMF kwa kuwa inamanufaa kwa nchi zao za kibepari ambazo zinataka kuendelea kunyonya nchi za Afrika katika kila nyanja.

Nchi za Afrika ikiwamo Tanzania zilipewa masharti magumu na IMF na Benki ya Dunia ikiwamo; sharti la ubinafsishaji, kufungua masoko kwa wawekezaji kutoka nje, kupunguza thamani ya fedha zake, kubidhaisha huduma za jamii kama elimu na afya, kuua vyama vya ushirika na kuleta stakabadhi ghalani, kukaribisha wakulima wakubwa na kuua wakulima wadogo, kuleta wachimbaji wakubwa na kuuwa wachimbaji wadogo, kuua benki za wananchi na kukaribisha benki za kigeni.

Ukitafakari kwa kina utaona baadhi ya masharti tuliyopatiwa na mabepari haya kwa muonekano niliouweka hapo juu yana nia ya kuwanufaisha mabepari hao na kuendeleza unyonyaji wa kiasi kikubwa kwa watanzania mafukara.

Viwanda IINia ya nchi za Magharibi na Marekani ni kuhakikisha ya kuwa wanapata masoko ya kutosha kutoka Afrika, mitaji na faida inarudi kwao, kutoa ajira za kutosha kwa watu wao kwa jina la wataalamu, kuendeleza majaribia yao ya kisayansi kwetu kwenye upande wa kilimo, afya, na sera mbalimbali za maendeleo wanazotuletea kama MDG, SDG, MKURABITA nakadhalika.

Ubinafsishaji umeendelea kufanya maisha ya wavuja jasho na walalahoi masikini kuzidi kumasikinika kila kukicha huku kundi dogo la walalaheri wakiendelea kuneemeka kila kukicha. Hebu tizama vile huduma za jamii muhimu kama afya na elimu vilivyogeuka na kuwa bidhaa ya gharama sokoni ambapo wanaoweza kunufaika na huduma hizi ni wale wanaotoka katika familia bora.

Tukienda mbali zaidi, tizama namna mashamba makubwa wamepewa matajiri kwa kauli ya ubinafsishaji ili hali mashamba hayo hayajaendelezwa kwa chochote na wananchi masikini wamebaki na vijisehemu vidogo wanavyogombania kila kukicha. Vile vile kweneye sekta ya madini, wawekezaji wamegaiwa maeneo makubwa ya kuchimba madini ili hali wachimbaji wadogo wakiambulia vieneo vilivyo na madini machache na wakizidi kugombana na wachimbaji wakubwa.

Ukitafakari kuhusu viwanda tulivyovigawa kama karanga leo hii vyote viko hoi bin taabani. Hakuna kiwanda cha kujivunia ila yamebaki maghala ya kuifadhi vyuma chakavu na kufugia popo. Hebu tafakari kwa uchache viwanda vilivyokuwapo Arusha, Moshi, Morogoro, Musoma, Mwanza, Tanga na kwingineko kwingi leo hii vimekwenda wapi?

Kibaya zaidi, ili hali karibia nyanja zote kuu za uzalishaji mali zimebinafsishwa bado tunaagiza kwa zaidi ya asilimia 70 ya bidhaa zote tunazozihitaji kama vile nguo, viatu, madawa, magurudumu, magari, miswaki, manukato, sabuni, vijiti vya meno na mengine mengi.

Madhila ya ubinafsishaji ni mengi mno ukilinganisha na faida tunazozipata. Sera ya Ujamaa na Kujitegemea iliweka bayana ya kuwa uchumi imara utajengwa na watu wake na sio kutegemea misaada kutoka nje ambayo inakuja kwa nia ya kudhoofisha taifa na sio kulisaidia.

Kwa kuhitimisha, ni wakati sasa taifa likatafakari upya na kurudisha nyanja kuu za uzalishaji kwenye umiliki wa wavuja jasho wenyewe. Wavuja jasho warudishiwe viwanda vyao, mabenki yao, vyama vya ushirika, migodi yao, mashamba yao ili taifa lijengwe kwa nguvu ya watanzania na sio kwa nguvu ya mabepari waliojawa na ulafi wa kupora bila huruma.

Na Jacob Mulikuza

Ndugu Mulikuza ni mchambuzi wa masuala ya kijamii na mtaalamu wa Sayansi ya Jamii

One Comment

  1. Elizabeth says:

    Makala nzuri,congrats Mulikuza J.

Leave a Comment