Changamoto za ukuaji wa majiji Afrika na somo kutoka historia ya jiji la Paris

Paris ni moja kati ya majiji maarufu zaidi duniani katika vigezo mbalimbali vya ubora wa miji na majiji duniani. Mwaka 2016 jiji la Paris linakadiriwa kupokea watalii zaidi ya milioni 18 na kulifanya kushika nafasi ya tatu duniani kwa kuwa jiji lililotembelewa na watalii wengi zaidi duniani, baada ya majiji ya Bhangkok na London. Utalii katika jiji la Paris ni chanzo kikuu cha mapato kwa jiji hilo, vivutio vikuu vya utalii katika jiji hilo vikiwa ni miundombinu mbali mbali iliyojengwa katika jiji hilo, ikiongozwa na mnara mashuhuri wa Eiffel ambao ndo alama kuu ya jiji hilo duniani kote.

Historia inaonesha kuwa kati ya mwaka 1832 na 1848, jiji la Paris lilikuwa changamoto kubwa zilizotokana na kuwa wakazi wengi zaidi kuzidi uwezo wa makazi yaliyo kuwepo enzi hizo ya muundo wa zama za kati za kale (medieval), yaliyokuwa na mpangilio duni na majengo ambayo hayakukidhi mahitaji ya ukuaji wa mji, lakini pia kwa kuwa na mitaa yenye barabara finyu na nyembamba mithili ya chochoro, zilizokuwa na hewa na mwangaza hafifu. Hii ilipelekea kudorora kwa mazingira, afya, kuongezeka magonjwa ikiwemo kipindupindu na uhalifu pamoja na kudorora kwa uchumi katika jiji hilo. Changamoto hizo zilizolikabili jiji la Paris enzi hizo zinafanana kabisa na changamoto zinazoyakabili majiji yanayokua kwa kasi zaidi duniani hasa yaliyomo barani Afrika sasa.

Mtaa wa Traversine, Paris, 1865-66, Picha na Charles Marville, Kutoka Maktaba ya Utawala wa Jiji la Paris

Mtaa wa Traversine, Paris, 1865-66, Picha na Charles Marville, Kutoka Maktaba ya Utawala wa Jiji la Paris

Katika kukabiliana na changamoto zilizoikabiri Paris enzi hizo, aliyekuwa mtawala (emperor) wa Ufaransa miaka hiyo (1852 -1870), Napoléon III (Louis- Napoléon Bonaparte) mpwa wa Napoleon I (Napoleon Bonaparte), akamkabidhi bwana Georges-Eugène Haussmann aliyekuwa mkuu wa eneo la kiutawala la mto Seine lililojumuisha jiji la Paris na vitongoji vya karibu, jukumu kubwa la kulipanga na kulijenga upya jiji la Paris ili kulifanya kuwa jiji la kisasa zaidi.

Pamoja na kupata upinzani mkubwa, bwana Haussmann kwa ustadi na uthubutu mkubwa akisaidiwa na maelfu ya vibarua alilifumua na kulipanga upya jiji la Paris, kwa kubomoa mamia ya majengo ya kale na kujenga katika mpangilio maalumu wenye viwango vinavyofanana jiji zima, barabara pana maarufu kama boulevards zikiunganisha maeneo yote muhimu ya jiji la Paris na kuboresha mzunguko wa watu na vyombo usafiri, pamoja na ulinzi na usalama, kujenga majengo makubwa ya kisasa zaidi ya makazi na biashara yalioambatana na boulevards hizo, bustani za umma, mifereji ya maji taka na miundombinu ya maji safi. Ingawa bwana Haussmann aliasisi na kutekeleza kazi yake ya kuliboresha jiji la Paris tangu mwaka 1853 hadi mwaka 1870, na kufariki mnamo mwaka 1891, kazi yake iliendelezwa hadi mnamo mwaka 1927.

(Katika rangi nyekundu) Boulevards na mitaa liyojengwa na Napoléon III na Haussmann. Picha na Dimitri Destugues

(Katika rangi nyekundu) Boulevards na mitaa liyojengwa na Napoléon III na Haussmann. Picha na Dimitri Destugues

Kazi kubwa ya bwana Haussmann imekuwa na matokeo ya muda mrefu kwa jiji la Paris na kuliwezesha jiiji hilo kumudu na kuendana na mahitaji ya sasa, hususan Paris likiwa ni jiji linaloongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu na kasi kubwa zaidi ya ukuaji wa idadi ya watu katika nchi za Jumuiya ya Ulaya.  Ikumbukwe pia kuwa kazi ya Haussmann kuliboresha jiji la Paris ndio iliyohamasisha (inspire) mpangilio na ujenzi majiji mashuhuri duniani kama Brussels, Rome, Vienna, Stockholm, Madrid, Barcelona, Chicago n.k.

Boulevard Haussmann, ikiwa na majengo yaliyojengwa na Haussmann. Picha na Thierry Bézecourt.

Boulevard Haussmann, ikiwa na majengo yaliyojengwa na Haussmann. Picha na Thierry Bézecourt.

Kwa mujibu wa World Economic Forum, Majiji kumi yanayoongoza kwa kasi ya ukuaji duniani yote yako barani Afrika, Mwanza na Dar Es Salaam zikishika nafasi ya tano na sita.

graph

Changamoto zinayoyakabili majiji yanayokuwa kwa kasi zaidi barani Afrika, likiwemo jiji la Dar Es Salaam, kama zilivyoainishwa na World Atlas, ni uwepo wa makazi duni na holela, barabara finyu, mfumo hafifu wa maji taka na upatikanaji maji safi, magonjwa ya maambukizi n.k. Changamoto hizi zinafanana kabisa na changamoto zilizolikabili jiji la Paris zaidi ya miaka 160 iliyopita kutokana na kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa idadi ya watu.

Maono, maamuzi thabiti ya mtawala wa Ufaransa enzi hizo “Emperor” Napoléon III na umahiri na kazi kubwa ilofanywa na bwana Georges-Eugène Haussmann aliyepewa jukumu la kuunda na kutekeleza mpango kwa kuliboresha jiji la Paris, taribani miaka 160 iliyopita unatoa mafunzo makubwa kwa watawala na jamii zetu hapa Afrika katika namna ya kukabiliana na changamoto za ukuaji wa miji na majiji tulizonazo sasa na miaka kadhaa ijayo.

Tafakuri niliyonayo ni kwamba je nchi zetu za Afrika bado hazina watawala wenye upeo wa kuona mbali, uzalendo, uthubutu na ujasiri, kama waliokuwa nao akina Napoléon III na Georges-Eugène Haussmann miaka zaidi ya 160 iliyopita, wa kuwekeza na kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu mikubwa ya kiuchumi yenye faida za muda mrefu na viwango vya kuweza kukidhi mahitaji ya watu ya sasa na ya miaka zaidi ya 100 ijayo katika majiji na nchi zetu?

Namini tukithubutu tunaweza!

Na Mwandishi Wetu

Leave a Comment