Mfumo sahihi unahitajika kuokoa sekta ya madini Tanzania

Tanzania's President elect John Pombe Magufuli addresses members of the ruling Chama Cha Mapinduzi Party (CCM) at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam, October 30, 2015. Tanzania's ruling party candidate, John Magufuli, was declared winner on Thursday of a presidential election, after the national electoral body dismissed opposition complaints about the process and a demand for a recount. The election has been the most hotly contested race in the more than half a century of rule by the Chama Cha Mapinduzi Party, which fielded Magufuli, 56, a minister for public works. REUTERS/Sadi Said - RTX1TYDQ

Majuma kadhaa yaliyopita Rais John Pombe Magufuli alipokea taarifa kutoka kwa kamati ya Professor Abulkarim Mruma iliyokwenda kuchunguza makinikia iliyokuwepo katika makontena yaliyozuiliwa kwenye bandari ya Dar es Salaam.Taarifa hiyo ilibaini uporaji unaofanywa na wawekezaji wa kibepari kwa kiwango cha hali ya juu. Taarifa hiyo iliwasononesha na kuwashangaza watu wengi juu wa uporaji huo na kuzua mijadala mingi sehemu mbalimbali za Tanzania.Nipongeze jitihada alizozifanya Rais kwa kutaka kufahamu ni kiasi gani hasa cha makinikia kinachosafirishwa kwenda nje ya nchi na kujua kiasi gani kinapatikana kutokana na makinikia hiyo kwenda nje ya nchi.

Ni wazi kuwa uporaji huu haukuanza jana wala juzi, uporaji huu unaofanywa na mabepari tunaopenda kuwaita wawekezaji ni wa muda mrefu ambao umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mfumo mbovu unaolinda rasilimali zetu hapa Tanzania. Tufahamu ya kuwa ubepari ni mfumo dhalimu sana unahitaji mfumo imara kuweza kupambana na ujanja wa mabepari hasa katika kutafuta rasilimali duniani kote. Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa na mfumo dhaifu ulioruhusu mianya mingi ya wizi kufanywa na mabepari kwa ushrika wa watanzania wenzetu ambao walipenda kujinufaisha wao wenyewe.

Katika makala zangu mbalimbali nilipenda kusisitiza ya kuwa uwekezaji Tanzania ni uporaji wa rasilimali za wavuja jasho wanyonge ambao huvuja jasho jingi na kuwafaidisha wawekezaji wachache. Madhara mengi tumeona katika sekta ya madini, ardhi, kilimo na kwingineko. Wizi huu uliotanabaishwa na taarifa ya kamati ya Professor Mruma hautoishia hapa unaweza kuendelea tena kwa nguvu kama mfumo wetu utabaki kuwa dhaifu kiasi hichi. Kuwaajibisha wahusika katika idara muhimu ni moja ya namna ya kupambana na tatizo ila sio suluhisho la kudumu kama mifumo yetu itaendelea kuwa dhaifu kwani tutafukuza watu kila siku na wizi utaendelea kushamiri.

Ni imani yangu ya kuwa kwa utajiri tulionao Tanzania hatuhitaji wawekezaji katika kila kitu na pale inapobidi kuwa na wawekezaji ni vyema basi serikali ikazuia uvunaji wa rasilimali na sio kujiweka pembeni na kusubiri kodi kutoka kwa wawekezaji hao. Mifano kutoka nchi zingine za Afrika zinaonyesha nchi zilizoweka mifumo imara zikafanikiwa katika madini.

Botswana ni moja wapo ya nchi za Afrika zenye utajiri mkubwa wa Almasi ambayo imeifanya nchi hiyo kupiga hatua kubwa ya maendeleo. Moja ya njia bora waliotumia Botswana ni pamoja na serikali kuwa mmoja wa wamiliki katika uchimbaji wa madini, serikali haijakubali mwekezaji ahodhi umiliki wa madini bali serikali ni sehemu ya umiliki wa migodi hiyo. Kwa ufupi nitajaribu kueleza mifumo ya kuimarisha ili tuweze kunufaika na madini yetu na kuzuia wizi wa hali ya juu tunaoendelea kuushughuida hadi leo hii.

Sekta ya madini ni lazima iwe chini ya umiliki wa serikali (State Ownership), hii haimaanishi serikali kumiliki madini tu ila pia itajihusisha na uchimbaji moja kwa moja.

Endapo mwekezaji atakuja kutaka kuwekeza katika sekta ya madini atafanya kazi na serikali na mwekezaji kutoka nje atakuwa mbia wa serikali. Huu ni mfumo imara utakaoweza kuzuia wizi lakini pia utawapa imani watanzania ya kuwa mali yao iko chini ya serikali na itawafaidisha. Umiliki wa sekta ya madini na serikali si tu itadhibiti wizi ila pia italeta hali ya umiliki kwa wananchi na watenda kazi katika sekta hiyo. Kwa sasa hali ilivyo watenda kazi wengi wamekuwa hawana uchungu na mali yao kwani wamekuwa wakiamini madini yameshauzwa kwa wawekezaji ambao wao wanajichukulia chao na hivyo wao wanaona ni fursa kwao kuiba kwa manufaa yao na familia zao.

Mfumo wa pili ni uwazi wa taarifa zote za sekta ya madini kuanzia mikataba inayosainiwa, mapato na matumizi kwa watanzania. Kwa muda mrefu Tanzania imekosa uwazi katika sekta hii ya madini na kupelekea watu kushindwa kuelewa wananufaikaje na madini yao. Hali hii ya sintofahamu imepelekea kuwa na migogoro isiyokwisha katika migodi ya North Mara, Buzwagi, Bulyanhulu, Geita, Mererani, Mtwara na Lindi kwenye mafuta na gesi ambapo watu wengi wanaishi katika umasikini wa kutupwa ili hali wamezungukwa na migodi mikubwa yenye utajiri wa hali ya juu.

Ushirikishwaji wa wananchi katika sekta ya madini (Governance in Mining) ni sehemu nyingine muhimu katika sekta hii ya madini. Mara nyingi tunashughudia kuwepo kwa ushirikishwaji hafifu au kutokuwepo na ushirikishwaji kabisa kwani maamuzi mengi hufanyika kutoka juu kwenda chini badala ya kutoka chini kwenda juu.

Hii imedhihirika hasa katika kugawa maeneo ya uchimbaji kwa wawekezaji ambapo watu wamekuwa wakifukuzwa kila kukicha kwenye maeneo yao ili kumpisha mwekezaji. Hii imeleta migogoro mingi kwani watu hawakushirikishwa katika jambo hili bali maamuzi yalifanyika hotelini mkataba ukasainiwa chumbani mwekezaji akaja.

Nimalize kwa kusema, rasilimali zetu tutazifurahia kwa kuwa na mifumo imara ambayo itawaongoza na kuwaruhusu watu kutenda vyema kwa uadilifu na kuzingatia mfumo imara uliopo.

Moja ya mfumo imara kwa maoni yangu ni kurudisha rasilimali zote ziwe chini ya umiliki wa serikali na serikali iwe sehemu moja wapo ya wazalishaji ndio tutakapoona faida ya rasilimali zetu badala ya serikali kuwa mkusanyaji kodi mkuu na mwekezaji kuchuma rasilimali zetu kwa uhuru atakao.

Na Jacob Mulikuza

Jacob ni mtaalamu wa Sayansi ya Jamii. Anapatikana kwa baruapepe: j_mulikuza2000@yahoo.com

Leave a Comment