Maghufira ya Safira

imagesWakati tulipokuwa tunawahoji wasichana wa Magomeni na Azimio kule Temeke, walituambia kwamba wasichana wadogo wanajiingiza katika vitendo vya ngono katika umri mdogo na kupata mimba kwa sababu ya ‘tamaa.’

Naam, “ni tamaa tu. Wasichana wana tamaa sana.”

Tumejifunza kwamba ili kujua undani wa jambo inafaa kuwa na subira na wenye kuhoji. Kuchokoza zaidi na zaidi mpaka yule anayekueleza aridhike kwamba ametafakari vya kutosha.

Swali letu, “kwanini wasichana wana tamaa?”

“Unakuta msichana anataka kuwa na nguo nzuri, anataka kupendeza na kwao hawana uwezo,” akajibu binti mmoja.

“Wengine wanaponzwa na chipsi-kuku,” huyu mmoja akadakia kisha wote wakaanza kucheka. “Kama yaliyomkuta Safira. Kufika fom’tuu na mimba hilo. Meneja kibendi” Akamtolea mfano msichana mwenzao wa mtaani.

Tukauliza tena, “Kwahiyo nyie wasichana mna tamaa?”

“Sio wote. Wengine hatupo hivyo. Ila kuna wengine ndio wanapenda sana vitu ambavyo haviendani na maisha yao.” Kama kawaida kila mmoja anajitoa na kusingizia wengine.

“Kama safira.” Binti wa watu akawa tena kichekesho.

Wakati tulipokuwa tunawahoji wasichana wa Magomeni na Azimio kule Temeke, walituambia kwamba wasichana wadogo wanajiingiza katika vitendo vya ngono katika umri mdogo kwa sababu ya ‘tamaa.’

Naam, “ni tamaa tu. Wasichana wana tamaa sana.”

Tumejifunza kwamba ili kujua undani wa jambo inafaa kuwa na subira na wenye kuhoji. Kuchokoza zaidi na zaidi mpaka yule anayekueleza aridhike kwamba ametafakari vya kutosha. Swali letu, “kwanini wasichana wana tamaa?”

“Unakuta msichana anataka kuwa na nguo nzuri, anataka kupendeza na kwao hawana uwezo,” akajibu binti mmoja.

“Wengine wanaponzwa na chipsi-kuku,” huyu mmoja akadakia kisha wote wakaanza kucheka. “Kama yaliyomkuta Safira. Kufika fom’tuu na mimba hilo. Meneja kibendi” Akamtolea mfano msichana mwenzao wa mtaani.

Tukauliza tena, “Kwahiyo nyie wasichana mna tamaa?”

“Sio wote. Wengine hatupo hivyo. Ila kuna wengine ndio wanapenda sana vitu ambavyo haviendani na maisha yao.” Kama kawaida kila mmoja anajitoa na kusingizia wengine.

Na sisi hatuachi kuwauliza maswali. “Ni vitu gani wasichana hawa wanahitaji kutoka kwa wanaume?”

Wakaanza kuorodhesha; Chakula, Mavazi, Pesa ya matumizi shuleni, Nauli ya kwendea shule, Simu n.k

“Kwanini wanahitaji hivi vitu kutoka kwa wanaume?”

“Unakuta msichana huyo kwao hawana uwezo. Wakati mwingine hapewi hata pesa ya kula shuleni. Wazazi ni masikini, sasa akipata mtu wa kumpa hivyo vitu unadhani atakataa?” anajibu kwa kutuuliza.

“Wakati mwingine unaenda shule inabidi ujipendekeze kwa kondakta wa daladala, kwa sababu nauli unayopewa haitoshi.”

“Kwani kuna wasichana wenye uhusiano wa kimapenzi na makondakta wa daladala,” tukauliza….

“Ohhh, nini daladala, hata bodaboda.”

“Ehh bodaboda ndio usiseme. Tena anakupeleka na kukurudisha na hela anakupa.”

“Kwa hiyo kinachowasukuma wasichana kuHITAJI hivi vitu kutoka kwa wanaume ni sababu ya TAMAA ama UMASIKINI?”

Kimyaaaaaa

(Kuna tofauti kati ya MAHITAJI ya msingi na MATAKWA. Wasichana wengi wanalazimika kukubali ufadhili wa mafedhuli watakaowapatia MAHITAJI yao kama vile chakula, mavazi, nauli za shule na hata kulipiwa ada. MATAKWA ni vitu vya ziada ambavyo si lazima kuwa navyo. Ikiwa mtu atashawishika kwa ajili ya matakwa, hiyo tunaweza kusema ni tamaa.)

“Hebu tuangalie tena…” tukaendelea kuuliza “kwa siku moja msichana anatongozwa mara ngapi?”

“Mara tatu au nne.” Akajibu wa kwanza, na kabla hajamaliza mwingine anadakia, “inaweza kufika hata mara kumi kwa siku.”

“Kila unapopita unakuta wanaume, na kila ukipita wanakuita. Wanakusumbua, wanakushikashika na unaweza kutongozwa hata mara kumi na tano.”

“Ukienda sokoni unatongozwa.”

“Ukienda kupata huduma hospitali unatongozwa.”

“Njiani unatongozwa.”

“Kwenye daladala unatongozwa.”

“Shuleni unatongozwa.”

“Hata kwenye nyumba za ibada unatongozwa.”

“Ukienda polisi unatongozwa.”

“Ofisi ya serikali ya mtaa unatongozwa.”

“Watongozaji ni wakina nani?”

“Unatongozwa na asiyekufahamu, unatongozwa na ndugu, mwalimu, askari, mfanyabiashara na unaweza hata kubakwa nyumbani na mjomba au binamu…”

Mara nyingi ni watu wazima. Wenye umri zaidi ya hawa mabinti. Swali…

“Mnawezaje kukataa mara zote kumi kwa siku? Mnatumia mbinu gani kujilinda?”

“Sio rahisi. Ndio maana wengine wanapata mimba.”

Watongozaji na wanyanyasaji daima wana mbinu mpya kila wanapojaribu na kushindwa. Watongozaji wanafanya mazoezi ya kutongoza. Na watongozaji watu wazima ama vijana wakubwa tuseme wanakuwa wamejaribu mara nyingi na wanajua nini cha kufanya ili kuwatega wasichana. Bahati mbaya wasichana wadogo hawana mbinu mpya. Hawana stadi za maisha na hawana mazingira yanayoweza kuzifanya stadi zao za maisha zifanye kazi. Mbele ya umasikini, wasichana wadogo wana uthubutu kiasi gani?

Ikiwa mafisadi pamoja na uwezo wao wa kifedha na elimu zao bado hawana uthubutu wa kulinda rasilimali za umma, wanazikwapua mpaka kugawana fedha kwenye sandarusi, je ni vipi kwa msichana aliyepewa shilingi mia tano ya nauli na hiyo hiyo ni pesa ya kula shuleni anaweza kuwa na uthubutu juu ya mwendesha bodaboda anayeweza kumhakikishia kwamba atakwenda shule na atakula bila shida?

Hivi karibuni, nimepanga kwenda kuonana na msichana anayefahamika kama ‘Master Mind’ katika mojawapo ya mitaa ‘hatarishi’ hapa Dar es Salaam. Msichana huyu ana kazi ya kuwakuwadia wasichana wadogo kwa vijana wakubwa na wanaume. Ana ushawishi na anaaminika. Nimepata habari zake, nataka kumuona tuweze kuongea. Huyu ni mmoja tu lakini wapo wengi.

Siku moja tulipokuwa na kikundi cha wavulana na wasichana katika mjadala, wavulana walionekana kuwalumu sana wasichana, wakiwakebehi kwamba hawawezi kazi ngumu, si wajasiri kama wao na wakiwakosoa kwa tabia ya kupata mimba na kuacha shule. Tukawataka wavulana wakae peke yao na wasichana wakae peke yao, kisha kila kikundi kiandike ratiba yao ya siku kuanzia muda wanaoamka mpaka muda wa kulala na waainishe vitu vyote wanavyofanya kwa siku hiyo.

Wote walianza kwa kuamka asubuhi, kisha wavulana wanapiga mswaki, kunawa uso na baadaye kuelekea shambani saa moja asubuhi ama shuleni kwa wale waliokuwa wanasoma. Shambani wanalima mpaka saa tatu kisha ‘dada zao’ wanakuja na uji. Wanakunywa na kuendelea kulima mpaka saa sita. Hapo wanapumzika, wanarudi kula nyumbani na kupumzika tena. Wanarudi shambani kwa saa chache mpaka jioni wanapokwenda kucheza mpira. Majira ya saa moja wanaenda kwenye mabanda ya kutazama runinga na kurudi nyumbani usiku. Halafu wanakula na kulala.

Wasichana aghalabu hudamka mapema zaidi kuliko wavulana, angalao saa kumi na moja kwa shughuli ya kuteka maji. Wakimaliza hufanya usafi nyumbani, kuosha vyombo na kuandaa uji kwa ajili ya ‘wanaume.’ Wanakwenda na uji shambani na huko baadaye watajiunga kulima na kumaliza sambamba na wanaume.

Wasichana watarudi nyumbani kuandaa chakula cha mchana wakati wanaume wamepumzika. Halafu shughuli huendelea kwa kutwa nzima, ikiwemo kurudi tena shambani, kutafuta kuni, kuandaa chakula cha usiku, kisha kuhakikisha kama watoto wadogo wamelala vizuri, kutazama mifugo kama vile kuku na bata wameingia bandani nk. Ratiba ya siku ya wasichana huhitimishwa ifikapo saa nne usiku. Hakuna muda wa kwenda kucheza mpira, nadra sana kwenda kupiga soga na muda wanaopata wa kusogoa na marafiki ni wakati wa kwenda kukata kuni ama kuteka maji. Hakuna muda wa kutosha kujisomea.

Tukawauliza, “kutokana na ratiba hizi, ni wakati gani wasichana hukutana na wanaume mpaka wakapewa mimba?”

Wavulana wakacheka sana, kisha wakasema, “ama tunawaibukia usiku kwenye vyumba vyao ama wakienda kukata kuni.”  Hivyo mbali na wavulana/wanaume kuwa na unafuu katika ratiba zao za siku jukumu jingine walilonalo katika siku ni ‘kuwatia’ mimba wasichana.

“Sasa bado kwa ratiba hii mnataka msichana aweze kushindana na mvulana katika masomo na mambo mengine?”  swali hili lilijibiwa na wavulana wenyewe, “haiwezekani”

‘haiwezekani’ ilitoka kinyonge wakiwa wameinamisha vichwa chini. Walijua si wakati tena wa kumhukumu Safira.

Ni Mungu tu ndiye mwenye kumpa maghafira (msamaha) yake, pale sisi wanadamu tunapomwona Safira (kiwakilishi cha mtoto wa kike) kama mwenye kiherehere cha kujitakia kupata mimba. Mpaka Mafarisayo, wenye kuhukumu tutakapovaa viatu vya hawa wasichana, ndipo tutakuwa wenye haki. Vinginevyo maghafira ya Safira yatapatikana kwa Mola.

Siku njema.

Na Mudiri wa Korogwe

 

Leave a Comment