Hoja hujibiwa kwa hoja na si vioja!

Na Mwandishi wetu

Ukumbi wa Bunge la Katiba

Ukumbi wa Bunge la Katiba

Ijumaa iliyopita Juni 02 taifa lilishuhudia kitendo kingine ambacho kinatia doa katika mhimili wa uwakilishi wa wananchi, Bunge. Taifa liliweza kudhihirishiwa pasi shaka hoja ya uhitaji wa kuwa na kiongozi wa shughuli za mhimili wa Bunge ambaye hafungamani na upande wowote wa chama cha siasa au kuwa sehemu ya watawala.

Kwa muda sasa, Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeshaanza kuzoea vitendo vya ajabu vya kutumia mabavu yasiyo na lazima dhidi ya wawakilishi wa wananchi hasa pale ushindanifu wa hoja au mantiki inapogonga mwamba.

Asili na dhumuni kuu ya demokrasi ya uwakilishi, ni kutoa fursa pana kwa wananchi wengi kuwatuma wawakilishi wachache waweze kwenda kusema kwa niaba yao yale ambayo ndiyo kipaumbele kwao.

Karne kwa karne, toka Uyunani, Ugiriki hata dola kama za Urumi zilihakikisha wale ambao wanakuwa katika vyombo vya mhimili hasa Bunge wanakuwa na uwezo mkubwa wa ushindanifu wa hoja. Bunge linakuwa ni uwanja wa mapambano wa hoja, fikra na mantiki. Ndivyo ambavyo hata ukumbi wa watanzania wa Dodoma, yaani Bunge unavyopaswa kuwa. Huku kiongozi mkuu aongozaye chombo hicho anapaswa awe amejaliwa upeo wa hali ya juu wa kumudu kuendesha vikao. Kiongozi Mkuu huyo, anapaswa kuhakikisha anatoa fursa sawa na pana kwa mijadala ya kimantiki na yenye tija ambayo inaongozwa kwa hoja na si vioja.

Historia ni mwalimu mzuri daima. Na matukio ya nyuma huzaa matarajio ya matukio ya mbeleni. Katika sheria hutumia lugha ya “precedence” yaani uwepo wa matukio au maamuzi ambayo hujenga msingi wa kuwa mfano na kutumiwa kuchota funzo kwa siku za usoni.

Spika wa Bunge, Job Ndugai

Spika wa Bunge, Job Ndugai

Toka Bunge la kumi [2010 mpaka 2015] ambapo Spika wa sasa, Ndugu Job Ndugai alikuwa Naibu Spika huku Mama Anna Makinda akiongoza Bunge kama Spika kulikuwa na chembe chembe mbali mbali za viashiria vya uwezo duni wa kuhimili mhemko na hisia wa Naibu huyo wa wakati huo. Matukio kadha wa kadha mathalani uvutano uliotokea kwenye kikao cha Septemba , 2013 mpaka kuamuru kutolewa nje ya Ukumbi Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa wakati huo, Freeman Mbowe, na mengine mengi ni mifano mizuri sana.

Kubwa katika yote tukio la mnamo 29 Julai, 2015 lililotokea Kata ya Ugogoni, wilaya ya Kongwa wakati wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakifanya mkutano na wanachama wenzao kuomba ridhaa kuongoza jimbo kwa nafasi ya Ubunge. Jimbo ambalo Ndugu Job Ndugai alikuwa mgombea pia. Alishindwa kujizuia na kumshambulia kwa fimbo mpaka kuzirai Dkt. Joseph Chilongani ambaye alikuwa anamrekodi kwa kitendo chake cha kumshambuli mgombea mwingine Simon Ngatuga aliyeibua tuhuma za ubadhilifu Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwenye mkutano huo wa wananchi. Kila mtu ambaye aliona rekodi ile  alipigwa na butwaa! Hapa tunapata uthibitisho mwingine wa asili ya ndani kabisa ya mhusika kuwa hoja haijibiwi kwa hoja bali, hoja anaijibu kwa vioja!

Tukio lile lilitosha kabisa kuondoshwa katika kinyang’anyiro cha kugombea ridhaa kuwa kiongozi wa watu. Kwani, daima kiongozi ni taa na kioo katika jamii. Jamii inaenenda na kujitanabaisha kwa matendo na mienendo ya wale wanaowaongoza. Fikra na mtizamo inajengwa kutokana nao. Hivyo, endapo akighadhibiwa hivyo ndivyo hutenda pasi busara au utu basi ilitosha kabisa kuwekwa pembeni. La hasha! “funika kombe mwanaharamu apite”… jambo hili lilipita kama vile halikutokea Chama Cha Mapinduzi kikamruhusu kada huyu na kampeni na hatimaye kupewa ridhaa ya kuongoza mhimili wa Bunge.

Katika zama za ushawishi na kuimarisha demokrasia pana kwa ushindanifu wa hoja, ndipo bado sikitiko kushuhudia viongozi wengine wa mhimili muhimu bado wapo katika fikra na mitizamo ya mabavu zaidi kuliko  busara, mihemko kuliko hoja na matumizi ya nguvu kuliko ushawishi.

Je ni bahati mbaya? Au ndiyo kila zama na kitabu chake?

Lazima jamii ihoji hivyo kwani kila aongozaye mbio za kijiti ndiye anaonyesha dira ya namna gani mbio zikimbiwe na kwa mtindo gani.

Endapo kama nyundo inatumika kuua sisimizi au vicheko vya wananchi vinampandisha kisirani inadhihirisha dhahiri shairi ni zama gani tulizopo.

John Mnyika, Mbunge wa Jimbo la Kibamba akitolewa nje ya ukumbi wa bunge na askari wa bunge

John Mnyika, Mbunge wa Jimbo la Kibamba akitolewa nje ya ukumbi wa bunge na askari wa bunge

Zama ambazo hata mhimili wa heshima na jukwaa mama la hoja na minyukano ya mijadala badala ya kuangalia namna bora kuhakikisha ushawishi na ujenzi wa hoja lakini fikra inakuwa ni namna gani linaweza kujilinda na kujiimarisha zaidi na zaidi kuhakikisha wanapambana kwa mabavu si hoja na kila ambaye ana fikra tofauti. Kauli ya Spika, Ndugu Job Ndugai ya kutaka kuimarisha kikosi cha askari wa Bunge [Surgent at arms] ambayo imeibuliwa kutokana na kile anachokiona askari hawakumudu kutii amri yake dhidi ya kumuondosha Mbunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika Ijumaa Juni 02 kwa haraka au namna ambayo alitamani inafikirisha zaidi. Kwani kwa waliotizama wanakiri namna alivyotolewa ndani Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kibamba ilikuwa ni kwa kudhalilisha sana si tu nyadhifa yake bali hata utu. Sasa endapo hiyo haikutosha, je dhamira ya ndani [inner intention] ilikuwa askari wale walipaswa kumdhuru?

Unatafakari pia kwa mapana, hukumu ambayo aliamua kuitoa dhidi ya Wabunge wa wawili; Halima Mdee, wa Jimbo la Kawe na Esther Bulaya wa Jimbo la Bunda Mjini ya kuwafungia kushiriki vikao vyote vya Bunge kwa muda wa mwaka mmoja je ilikuwa kweli inahitajika na ya haki?

Si mara ya kwanza tumeshuhudia Mbunge, mwakilishi wa wananchi akibebwa mzobe mzobe pasi staha na kutupwa nje ya Bunge. Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini Septemba 05, 2013 nae alipata kufanyiwa kitendo mithili ya kile ambacho kimejirudia tena kwa John Mnyika, Mbunge wa Jimbo la Kibamba.

Jamii haishtuki. Bado!

Kwa sasa, haitakuwa ajabu au hakuna la kushtusha kwani uthubutu na uwezo wa kufikiri unaweza kushawishi viongozi hata kuingizwa kwa Makomandoo au Askari maalumu wa kuzuia ghasia [FFU] kukabiliana na Wabunge ambao nguvu yao ipo katika mdomo [ujenzi wa hoja]. Tunachagua kugota kufikiri. Tuafungua ukurasa wa utumiaji wa mabavu!

Endapo pamoja na kumsukuma na kubeba pasi heshima kule kote ambako kumefanywa bado mtoa amri amekerekwa na utendaji kazi, kuna uwezekano mkubwa kabisa tamanio ni uwepo wa askari ambao hata wanaweza si kumbeba na kumtoa nje Mbunge bali hata kumtia ulemavu kwa kipigo watakacho msushia wakati wakiwa katika hilo tendo la kutoa nje. Hii ni ajabu kweli kweli!

Wabunge wakikaa kimya wasiposimama kidete kukemea wafahamu si salama. Kwa yanayowatokea Upinzani, ipo siku wabunge wa chama tawala nao wataonja shubiri yake.

Msomi nguli wa Sheria, Profesa Shivji amenena kwamba; “Bunge sio darasa la kuwadhibiti wanafunzi. Hata darasani tunashauriwa turuhusu mawazo yanayopingana na ya mwalimu, sembuse Bunge.” Na kuongezea; “Kanuni ni kuwezesha/kurahisisha mjadala; sio kuuzima. Nguvu za hoja zinajidhihirisha. Hoja za nguvu zinadhalilisha”.

Ee Mungu usiziondolee baraka ulizozibariki Tanzania!

Mungu ibariki Tanzania.

Leave a Comment