Elimu haisubiri; Je watoto wetu wanajifunza?

imagesKupata elimu iliyo bora ni msingi wa kufikia malengo ya nchi na dunia na hatimaye kubadili maisha ya mtu na hata jamii nzima kupiga hatua bora kimaendeleo.

Zipo jitihada kadha wa kadha zilizofanyika kuongeza upatikanaji wa elimu hasa ngazi ya elimu ya msingi na sekondari mathalani , ujenzi wa shule za msingi na sekondani katika kila kata (jitihada zilizoanzishwa na Serikali ya awamu ya nne), na hivi sasa, uanzishwaji wa sera ya elimu bila malipo chini ya serikali ya awamu ya tano. Dhuhumi kuu likiwa ni kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya elimu na kwa mapana zaidi kuhakikisha nchi inajikwamua kimaendeleo kwa taifa kuelimika.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimesaini mikataba ya Umoja wa Kimataifa ikiwa ni pamoja na utekelezwaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) yaliyopitishwa mwaka 2015.

Miongoni mwa malengo hayo (17), lengo la 4 ni kuhakikisha upatikanaji wa elimu shirikishi na bora kwa wote. Wadau wa elimu Tanzania pamoja na kufanya jitihada mbalimbali za kuboresha elimu nchini, wamejiunga na kampeni na jitihada mbalimbali za ndani na je ya nchi ili kushirikiana na kupaza sauti zao kwa pamoja.

Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na Wiki ya Elimu Duniani (Global Action Week for Education) inayo ratibiwa na taasisi iitwayo Global Campaign for Education yenye ofisi zake Afrika ya Kusini.

Wiki ya Elimu Duniani (Global Action Week for Education) inaadhimishwa kitaifa wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara yatakayozinduliwa tarehe 24 na kufungwa tarehe 28 mwezi April. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inasisitiza uwajibika na ushiriki wenye tija kwa wananchi katika kutimiza Lengo la 4 la Malengo ya Maendelo Endelevu. Kauli mbiu hii inalenga mambo makuu matatu; Elimu bora, Ushirikiswaji na Elimu Bure.

Kauli mbiu hiyo inatukumbusha wajibu wetu kama taifa hasa wadau mbalimbali katika upatikanaji wa elimu bora ili kuwa na taifa lenye ustawi. Wadau wa elimu kama wanafunzi, wazazi, jamii, walimu, taasisi zisizo za kiserikali, taasisi za kidini, wadau wa mendeleo, viongozi katika ngazi mbalimbali, vyombo vya habari na serikali.

Shirika la Twaweza limekuwa likifanya tafiti za kina kuhusu hali ya elimu nchini zenye lengo na kupima uwezo wa wanafunzi kufanya kuhesabu na kusoma kwa Kiswahili na Kingereza. Ripoti ya Uwezo-Twaweza ya mwaka 2015 ya tathmini ya Elimu iliyozinduliwa tarehe 10/04/2017 imeainisha mambo mengi ya kutafakari kwa mapana juu ya sekta ya elimu ilipotoka, ilipo na inapokwenda.

Tathmini ya jumla inaonesha bado uwezo wa wanafunzi kufanya hesabu na kusoma Kingereza na Kiswahili umeshuka kulingana na matarajio ya mtaala uliopo. Ni 72% ya wanafunzi wa darasa la saba wameweza kufaulu jaribio la darasa la pili huku 35% ya darasa la tatu wakiweza kufaulu jaribio hilo hilo.

Lugha ya kufundishia shuleni ni eneo linalohitaji kuendeleza majadiliano ya kina ya kama bado tunahita mfumo tulionao uendelee, ama tujikite katika lugha moja ya kufundishia  kati ya Kiswahili na kingereza, katika ngazi zote za elimu.

Tathmini hii ya Uwezo inatuonesha kuwa bado kiwango cha ufaulu katika lugha ya kingereza ni mdogo ukilinganisha na lugha ya Kiswahili. Ni mwanafunzi 1 tu kati ya 10 wa darasa la tatu anaweza kusoma kwa kingereza insha ya darasa la pili, na 5 kati ya 10 wa dasara la saba wanaweza kusoma hadithi ya kingereza ya darasa la pili.

Swali la kujiuliza ni je, wanafunzi hawa wa darasa la saba wataweza vipi kuelewa masomo yao ya sekondari yanayofundishwa kwa kingereza ilihali hawaweza kusoma vitu vya darasa la pili? Na je mfumo huu hauandai wanafunzi kufanyqa vibaya katika mitihani yao ya kidato cha nne?

Tafiti hii pia imeonesha bado kuna tofauti kubwa ya uwiano wa ufaulu kati ya miji na mikoa ya Tanzania. Dar Es Salaam imeongoza kwa 64% wakati Katavi imekua ya mwisho kwa 23%.

Vile vile Iringa mjini imeongoza kwa ufuulu wa 74% huku Sikonge ikiwa ya mwisho kwa 15%.  Tofauti hii ndio chanzo kikuwa cha kua na makundi hasa ya wenye nacho na wasio nacho huku familia ziishizo mjini zikiwa na nafasi kubwa ya kufaulu na kuendelea na masomo ya juu kuliko familia za vijijini.

indexJe ipo haja ya kupitia tena bajeti inayotengwa katika sekta ya elimu na kujitathmini tena kwa kuangalia vipaumbele vya taifa? Na je wadau mbalimbali wa elimu wanatimiza wajibu wao kwa kuwekeza zaidi katika maeneo ya pembezoni ili kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi?

Kuna haja kubwa sana kwa Serikali inayojenga Taifa imara kuhakikisha hakuna mgawanyiko na utofauti mkubwa sana kielimu kwani athari yake inakuwa ya muda mrefu kwa jamii.

Nimalizie kwa kugusia kauli za Baba wa Taifa aliesema kuna maadui watatu wa maendeleo ya taifa hili ambao ni pamoja na Njaa, maradhi na ujinga.

Elimu ni njia kubwa na sahihi katika kufuta ujinga ili kuhakikisha nchi inapata maendeleo hivyo serikali kama mdau mkuu wa sekta hii haina budi kuhakikisha inatatua changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta hii adhimu.

Na Rahma Bajun

Rahma ni mchambuzi wa masuala ya kijamii anayepatikana Dar es Salaam

Leave a Comment