Je, maendeleo vijijini yatapatikana kwa kupewa fedha?

 

fedhaHivi sasa mchakato wa kugawa milioni hamsini katika kila kijiji umeanza ambapo serikali za vijiji na mitaa wametakiwa kufungua akaunti benki ili waweze kupatiwa fedha kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wao kujiendeleza.

Yamkini hili ni jambo jema kwa baadhi ya watu ila kwangu mimi napata mashaka na nia hii ya kuwaondolea watu umasikini kwa kuwagawia fedha. Mjadala utaanzia hapa ili tuone kama kweli dhamira hii itasaidia kuondoa umasikini kwa watu walio vijijini.

Hebu tuanze kudadisi kidogo tangu mchakato huu ulipoanza wakati wa awamu ya nne ya Ndugu Jakaya Kikwete. Wakati huo fedha hizi zilijulikana kama mabilioni ya Kikwete, ambapo fedha zilisambazwa katika vijiji na mitaa ya mijini ili kuwasaidia watu kuboresha mitaji na kuwaondelea umasikini. Ila sina hakika ni kwa kiasi gani walengwa walizipata fedha hizi na kwa kiasi gani umasikini umepungua katika maeneo yao.

Wasiwasi wangu hapa sio fedha kuwafikia wananchi ama la, ila je fedha ni nyenzo sahihi ya kuondoa umasikini katika vijiji vyetu?

Hebu tafakari kidogo!

Tangu mabilioni ya Kikwete kugaiwa kama njia moja wapo ya kuondoa umasikini je, umasikini huu umepungua kwa kiasi gani katika vijiji vyetu? Na je, uko wapi mrejesho uliotokana na tathimini ya kuonyesha ni kwa kiasi gani mabilioni haya ya Kikwete yalifanikiwa ama yalishindwa kufikia malengo?

Taaluma ya maendeleo ya jamii inasisitiza ya kuwa kabla ya kuleta mradi wowote wa maendeleo katika jamii fulani kunapaswa kufanyika tafiti zitakazoweza kugundua tatizo husika na nini iwe suluhisho lake. Je, uko wapi utafiti uliofanyika na kugundua maendeleo vijijini yataletwa kwa kuwagawia fedha wananchi?

Je, tulijifunza nini kwenye mabiloni ya Kikwete kabla ya kuanza kugawa mabilioni ya Magufuli na Samia Suluhu kama suluhisho la umasikini katika vijiji vyetu?

Ukiendelea kujiuliza kwa kirefu zaidi, je, fedha hizi zinagawiwa kwa sababu ni suluhisho la umasikini ama zinagawiwa kwa kuwa ziliahidiwa katika kampeni za mwaka 2015?

Ninachojaribu kukieleza katika makala hii ni je, tumefikiria vya kutosha kama wananchi na kugundua hitaji letu ni fedha? Au kwa kuwa tunaona fedha zinakuja hatutaki tena kudadisi kwa kina kama maendeleo tunayoyataka yanaletwa na fedha?

Mara nyingi katika makala zangu nimekuwa nikisisitiza ya kuwa Tanzania inachokikosa kwa sasa ni dira na ramani ya maendeleo tunayoyataka. Je, nyumba yetu ya maendeleo tunayotaka kuijenga tunafuata ramani gani au kila mtu anaweka tofali vile atakavyo?

 

Ramani ya maendeleo i wapi?

Ama je, ramani hii ya mendeleo wanayo mafundi wakuu ila sisi mafundi wasaidizi hatupaswi kuwa nayo kwa kuwa sio mafundi wataalamu? Lakini kama ndio hivyo mbona sisi mafundi wasaidizi ndio tunaofanya kazi kubwa kuliko mafundi wakuu iweje tusiwe na ramani ili tusiharibu nyumba yetu?

Tanzania tulishawahi kuwa na ramani imara ya kujenga nyumba yetu ya maendeleo ila tukaona haifai na kuamua kufuata ramani za kupakua (download) kutoka kwenye mtandao (internet). Je, ramani hii ya kupakua itatupatia nyumba tuitakayo ama tutakuwa tunaiga nyumba za watu wengine bila kujali sisi wenyewe tunataka nyumba yetu iweje? Au kwa kuwa tunataka nyumba ya kisasa hatuna budi kupakua za watu wengine bila kujali sisi tunataka kujenga nyumba gani? Au tunataka kujenga ili mradi tu ifanane na ile nyumba iliyopo London, Manhatan, Paris, New York na kwingineko kwingi.

Nimeamua kutumia lugha hii ya picha ili iwe rahisi kuelewa, nikizungumzia ramani ya mendeleo ambayo Tanzania iliwahi kuwa nayo ni Azimio la Arusha (1967). Azimio la Arusha liliainisha kwa uwazi kabisa ili nchi yetu ipate maendeleo iyatakayo haina budi kuacha kutegemea fedha kama zana ya maendeleo bali fedha iwe matokeo ya maendeleo. Ramani hii tukaamua kuitupilia mbali na kuona haifai na kila mara tukijenga nyumba tunaona ukuta ukizidi kupinda tu kila mara na hatujui nini cha kufanya.

Azimio la Arusha lilisisitiza kwa uwazi kabisa maendeleo ya kweli yatatokana na watu, ardhi, sera bora na uongozi bora. Je, kwanini haya yasisitizwe kwa sasa kama njia muhumu ya kuleta maendelo badala ya kuwagawia watu fedha?

Je, kuna hatari gani katika kugawa milioni hamsini kwa kila kijiji na mitaa?maskini

Kwanza kabisa, kugawa mamilioni haya kwa wananchi hakutosaidia kuleta maendeleo hata kidogo kwani huku ndo kuwafundisha watu kuwa wategemezi na kuwaonyesha ya kuwa bila serikali wao wenyewe hawana mchango katika maendeleo yao. Ndio maana leo hii kila mtu anaamini Tanzania yetu itaendelezwa na wawekezaji kutoka nje ya nchi na wao watabaki kuwa mashuhuda wa maendeleo basi.

Kila mtu leo hii anapaza sauti na kusema bila ya wawekezaji hatuwezi kuendelea, na wawekezaji wakija tunashangilia kama vile tumeona mbingu. Wawekezaji wakianza kuchuma rasilimali zetu na kutuacha mafukara tunaanza kulalamika ya kuwa tunaibiwa ardhi, madini, samaki na mengine mengi. Je, huku kutugawia fedha sio kuendelea kutudumaza zaidi?

Je, si wakati sasa wananchi wakafundishwa namna ya kuvua samaki badala ya kupewa samaki kila mara?

Kitu chengine cha msingi kabisa ni kudumaza fikra za wananchi kwani watu wanajua tayari kuna vya bure vinakuja na hivyo watu wanaacha kutumia vipaji vyao kuweza kufanya uzalishaji imara katika kilimo. Hivi sasa kila mtu anayetaka haya mamilioni anataka kuwa mjasiriamali na hakuna mtu anayewaza kilimo hata kidogo.

Cha kusikitisha zaidi katika mtaa ninaokaa baada ya watu kuambiwa mamilioni haya yanakuja kila mtu kafurahi kwani wamejua neema inakuja. Ila walipoulizwa sasa hizi pesa mtazitumiaje wengi wakaanza kusema tutaunda vikundi na kisha tujidai tunafanya biashara fulani ila tukipatiwa fedha tutagawana na kila mtu atafanya kila anachojua. Nilipigwa na butwaa kwenye ule mkutano wa mtaa nikajiuliza umasikini utaondoshwa na fedha kama hivi ndivyo watu wanavyofikiri?

Kwa upande mwingine, mabilioni haya yatazidi kuwanufaisha wajanja wachache na kuwaacha wengine wakitoa macho bila kujua fedha hizo zimepotelea wapi. Je, mabilioni haya sio muendelezo wa unyonyaji katika jamii maaana wachache wataendelea kuneemeka kwa mgongo wa masikini?

Je, mbadala wa mabilioni haya ni nini?

Tukumbuke ya kuwa maendeleo ni watu na sio fedha, hivyo basi katika kufikia maendeleo endelevu watu hawana budi kushirikishwa kwa kufanya tathimini pamoja na wao ili kujua watu wanauwezo gani wa kufanya kazi na nini hasa wanakosa kufikia malengo wayatakayo. Tunafikiri watu wanahitaji fedha kuwaendeleza kumbe siyo hali ilivyo ni kwa kuwa hatukai nao tukaongea nao na kujua hasa hitaji lao ni nini, ila sisi wataalamu tunawaza kwa niaba yao.

Nitoe mfano mrahisi tu, naishi Tarime mkoa wa Mara ambapo ndizi, viazi mviringo, viazi vitamu, vitunguu vinastawi sana na kwa wingi na kila mji wa mtu ukienda wanashamba kubwa sana la ndizi ambapo kila siku mtu hupaswa kwenda mjini kuuza mkungu wa ndizi kwa bei ya kutupwa kabisa ambapo mkungu wa ndizi huanzia elfu mbili mpaka elfu tano.

Wakulima hawa huzalisha kwa wingi sana mazao niliyotaja hapo juu ila wanachokikosa ni soko la uhakika ambalo lingewawezesha kuuza kwa wingi mazao yao. Ila hili limewakatisha tama na kuona kilimo hakilipi na kuona bora waanze kufanya vibiashara vidogo vidogo ili wapate mahitaji yao ya kila siku. Hata ukitafakari hayo mabilioni watakayopewa ni pesa kidogo sana ambayo wao wenyewe wanaweza kuipata mara dufu katika kilimo chao.

Ukikaa ukazungumza na wakulima hawa wanasema wanaweza kuwa wazalishaji wa kubwa wa mazao hayo kama wangekuwa na soko la uhakika. Na hapa ndipo nilipokumbuka vyama vya ushirika kwani vingeweza kuwa wanunuzi wakubwa wa bidhaa zao kwa wingi kisha wao kuziuza kwa wingi pia katika masoko makubwa.

Sasa hapa badala ya kufikiria ni kwa namna gani elimu bora ya kilimo na kurejesha vyama vya ushirika katika kila wilaya ama kata kama mkombozi wa umasikini siye tunaanza kufikiria kugawa fedha kwa watu kama vile watu wanachohitaji ni fedha.

Watu wanahitaji maarifa, watu wahitaji ramani ya kuwaonyesha watafikiaje maendeleo, tunahitaji kujifunza kutoka kwa wananchi wenyewe, tunahitaji kuwaamini wananchi, tunahitaji viongozi watakaoweza kuwa na maono ya kuwasaidia watu kutimiza malengo yao kwa kuendeleza ubunifu wao, tunahitaji kuwapa fursa wananchi watende bila ya kutoa vipaumbele kwa wawekezaji kutoka nje. Haya na mengine mengi ndio msingi wa maendeleo ya nchi yetu na sio kugawa fedha kwa watu huku wao wanawaza wapate fedha wakaoe zaidi, wakanywe pombe ama kufanya mambo mengine kama hayo.

Watanzania wanahitaji kupewa maarifa imara yatakayo kuza na kuboresha fikra zao katika uzalishaji ili mwisho wa siku wapate fedha za kutosha kuweza kufanya mambo wayatakayo.

 

Mwandishi wa Makala hii ni mtaalamu wa Sayansi ya Jamii. Anapatikana kwa baruapepe; j_mulikuza2000@yahoo.com na simu +255 786 946 931

 

One Comment

 1. YOUNG CHACHAGE says:

  Nadhani hapo hatujapata ufumbuzi wa tatizo la umasikini,kuna maswali mengi sana ambayo pia yatapanua mjadala huu kwa kujiuliza ni nini sababu kuu ya umasikini tuliokuwa nao ni mtu binfsi au mifumo inayo mzunguka huyu mtu?
  Na je ipi njia sahihi ya kutatua?

  Suala hili la kugawa pesa kwa kila kijiji linaonesha kuwa tatizo ni watu wenyewe na si mifumo. Mimi naona kabisa kuwa suala hili limeshindwa kuona yupi mkuu wa umasikini. Tatizo ni mifumo leo hii unaweza ukagawa pesa lakini ardhi ya kulima imechukuliwa na wawekezaji. Leo hii angalia wamachinga watapa hio pesa lakini watakimbizwa na mgambo.
  Hapa moja kwa moja hizi pesa zinaelekea kupotea.

  Swali jingine pia la kujiuliza na ambalo litapanua mjadala huu, Ni je hiyo pesa inatoshereza kwa kila kijiji na vikindi ambavyo vitaundwa hapo kijijini? Hapa tufikiri sana pia maana tunaweza tukagawa pesa hizi kisiasa tu, lakini zitashindwa kuwainua watu kwa ktotosha.

Leave a Comment