Mitandao ya kijamii ni umaskini kwa Tanzania?

social media icons

nembo za mitandao ya kijamii

Katika miji ya Tanzania leo hii kila kona unayoenda utaona simu za mkononi zenye uwezo wa kutumia intaneti zimezagaa almaarufu kama ‘smartphone’. Kwa mujibu wa jarida la Reuters,   watumiaji wa simu za mkononi Tanzania wameongezeka kwa asilimia 16 mwaka 2014 na kufikia watu milioni 31.86 huku watumiaji wa intaneti wakiongezeka kwa asilimia 22 na kufikia watu milioni 11.35 mwaka 2014. Hii idhihirisha sekta ya mawasiliano inakua kwa kasi kubwa.

Je, ni kwa namna gani mitandao ya kijamii ni umaskini kwa Tanzania ili hali inachingia katika pato la taifa? Nikirejea maneno ya mwanazuoni nguli Dkt. Abunuasi Mwami wakati fulani alishawahi kuniambia ya kuwa “one physical phenomenon cannot cause another physical phenomenon” (tukio moja la kuonekana haliwezi kuleteleza tukio lingine la kuonekana). Mfano; mtu akinywa maji inatarijwa baada ya muda fulani atatoa haja ndogo, lakini je ni tendo la kunywa maji linaloleta haja ndogo au ni matokeo ya hali zisizoonekana ambazo huendelea katika mwili wa binadamu ambapo mwishowe huleta haja ndogo hiyo?

Mfano huu unaeleza ya kuwa ujio wa utandawazi nchini kwetu sio jambo jema kama vile ambavyo wengi wetu tumekuwa tukiliona na kulishupalia.

Utandawazi ama kama vile ambavyo wanazuoni wamependa kuuita ‘utanda-wizi’ umechangia kurudisha nyuma maendeleo yetu kwa kiasi kikubwa japokuwa takwimu za wanauchumi zinaonyesha uwepo wa utandawazi umeleta maendeleo kwa kiasi kikubwa.

Tumeshuhudia namna ambavyo mitandao ya kijamii kama vile face book, twitter, instagram, whatsup, snapchart, tango na mingine mingi kwani hii ikianzishwa kila uchao. Mitandao hii ya kijamii inaendelea kuwa changamoto kwa rasilimali watu hususani vijana ambao wengi wetu tumeikumbatia  na kuifanya kama sehemu muhimu sana na ya ulazima katika maisha yetu.Wapo ambao wamejijengea mtazamo kwamba hawawezi kabisa kuishi bila hiyo mitandao.

Hebu turejee historia kidogo ili tukumbuke tulikotoka na tuweze kukihusisha na kile ambacho kinaendelea kwa sasa kwani tusifikiri yale yanayotokea sasa hivi yamekuja tu bila kuwa na chanzo maalum.

Katika karne ya 20 mwanzoni, bara la Afrika lilitawaliwa na watu kutoka nchi mbalimbali za Ulaya na Uarabuni. Wakati wa ukoloni ili mabwana wakubwa hao waweze kutimiza lengo lao iliwapasa kwanza kututawala kifikra ili kuonyesha yale tunayoyafanya sio ya msingi na kuwa ni mambo yasiyostaarabika na yakichawi.

Ikumbukwe, walivyoanza kuja mabwana wakubwa hawa Afrika walitanguliza wamisionari ili waje kutulegeza kwa jina la kuleta ustaarabu na kutuletea neno la Mungu kwani waliogopa mkinzano. Ni muhimu kufahamu ili uweze kumtawala mtu kiurahisi ni lazima kwanza uanze kuiteka fikra yake ili muweze kuyaona mambo katika sura moja, ndio maana kuanzia hapa ikawa rahisi kuwatumikisha mababu zetu katika mashamba makubwa kwa kuwaaminisha katika kilimo cha biashara na kuacha kilimo kwa ajili ya chakula. Ukoloni huu ulizaa utumwa na mateso ya nguvu kwa waafrika mpaka pale miaka ya 1940 ambapo biashara ya utumwa ilitangazwa kukoma duniani.

Ukoloni huu haukuishia hapa, kwani baada ya nchi nyingi za Afrika kupata uhuru wao ndipo pale ukoloni-mambo-leo ukaanza. Baada ya uhuru nchi nyingi za Afrika zilijua ya kuwa sasa wako huru kufanya yale wayatakayo kama nchi kumbe ilikuwa ni muda wa kupitia upande mwingine wa sarafu iitwayo ‘ubepari’(Capitalism).

Nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani walifanya juhudi zote kueneza ubepari huu katika nchi zote za Afrika ili kuweza kuzitawala upya bila kuuonyesha uwepo wao hapa moja kwa moja.

Ubepari huu ulisambazwa kwa njia ya mashirika ya kimataifa pamoja na Benki ya dunia na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (International Monetary Fund-IMF). Mashirika haya yalitunga sera mbalimbali ambazo nchi za Afrika walipaswa kuzifuata kwa kisingizio cha kuwatoa kwenye dimbwi la umaskini. Isitoshe sera hizi kutoka kwa mataifa ya kibepari zilikuwa na masharti endapo zisipofuatwa misaada ya mali na pesa zingesitishwa kuletwa nchini.

Kwa kuwa nchi nyingi za Afrika hususani Tanzania zilikuwa na shida ikatupaswa kuitikia wito wa mabwana wakubwa na kufungulia soko huria kuanzia miaka ya 1980 tukasahau na kuuona ujamaa kuwa ni mambo ya kishenzi na yakichawi. Huu ulikuwa muendelezo wa kutawaliwa kifikra ambapo ulitufanya kuona bila kupata misaada kutoka kwa mataifa ya kibepari hatuwezi kuendelea na ndipo hapo utegemezi uliokidhiri ulizidi nchini mwetu na kuanza kuagiza kila kitu kutoka nje na kugeuka kuwa soko la mali ghafi ya kutoka mataifa ya kibeberu.

Kama vile haitoshi, utandawazi ukabisha hodi na kwa kuwa Tanzania na nchi zingine za Afrika tulishazoea kupokea tu kwani tulishaaminishwa katika fikra zetu kila kitu kutoka Magharibi ni kuzuri tukapokea.

Mbaya zaidi, mabepari hao wakasema ni vigumu sana kuishi nje ya utandawazi kwani utandawazi huu umefanya nchi zote kuwa karibu kama vile watu waishio kijijini. Inatia simanzi kuona vile ambavyo tulizidi kuaminishwa vitu na tukihoji tunaambiwa misaada itasitishwa.

Mabepari hawa walitaka tuendelee kufuata wasemayo ili waweze kututawala vizuri na ili kufanikisha adhma yao hiyo ndio ikaletwa lugha mpya iitwayo Haki za Binadamu wakisititiza mtu yeyote yuko huru kufanya kile atakacho, na haki hizi za binadamu zilipata tafsiri kutoka nchi za kibepari na zikasambazwa kwa kasi kwa kutumia mashirika ya kimataifa yakisaidiwa kwa karibu na asasi zisizo za kiserikali (NGOs).

Hivi tulishawahi kujiuliza haki za binadamu wa kitanzania ni zipi? Au tafsiri tuliyonayo ni kutoka kwa umoja wa kimataifa? (Nitalichambua hili katika makala nyingine kwa kina).

Je, mabepari wa sasa hawatawali fikra kwa kupitia mitandao ya kijamii? Kwanini basi mabepari hao huanzia kwenye fikra zetu? Jibu ni rahisi Haki za Binadamu, wanataka ukianza kuhoji wakwambie mtu anauhuru wake wa kuamua afanye nini na aache nini. Na ndo maana hata leo ukijaribu kuwauliza vijana walio wengi mitaani iweje leo mnatumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii kuunufaisha umma mambo yako binafsi ambayo hata yale watu wasingepaswa kujua watakwambia tuna haki kama binadamu kuchagua yale tufanyayo.

Leo hii tunashuhudia watu mbalimbali katika mitandao ya kijamii wakieleza umma kuhusu mahusiano yao na wenza wao, wakionyesha sehemu mbalimbali za miili yao, kueleza matatizo yao binafsi kwa jina la kutaka ushauri na wengine kudiriki kurusha picha zao za ngono katika mitandao hiyo kwa jina la Haki za Binadamu.

Umaskini kwa Tanzania unaletwaje na mitandao hii ya kijamii? Tukiangalia kwa uwazi kabisa sharti la ubepari ni kuhakikisha kuwa wanapata faida kubwa kwa kupitia wanyonge ambapo wanyonge hao hutumikishwa sana ili kuweza kuleta faida kubwa kwa mabepari hao.

Hebu tuanze na upande wa kwanza wa unyonywaji, tulishawahi kujiuliza gharama ya kutumia simu ya kawaida isiyokuwa na intaneti (almaarufu kama simu ya tochi) na ile iliyo kuwa na intaneti (smartphone). Labda ndio ama hapana, ila ukiwa na simu ya tochi unahitaji vocha kwa ajili ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno na kupiga japo gharama yake bado sio ndogo kwani itakupaswa kuunga aina fulani ya vifurushi ili kuweza kuwasiliana na mitandao mingine na gharama hii hupanda kila kukicha.

Je ukiwa na simu yenye uwezo wa intaneti (smartphone) inakuwaje sasa? Hapa kuna tofauti kidogo kwani itakupasa kuwa na pesa kwa ajili ya kupiga, ujumbe mfupi wa kawaida na intaneti. Na ikumbukwe gharama hii ni kubwa kwani wameshakuwekea makundi mbalimbali ambayo unapaswa kuchagua ili kufikia huduma yako. Na je usipokuwa na pesa kwenye simu yako hiyo simu yenye uwezo wa intaneti itakufaa nini? Hapa ndipo utaona watu wakitumia pesa nyingi kuhakikisha wanakuwa na vocha kwenye simu zao kwa ajili ya kuweza kuingia kwenye mitandao hii ya kijamii kila siku ili kuweza kupata au kutoa taarifa.

Cha ajabu zaidi, kuna makundi ya watu ambayo hawafanyi kazi kama watoto na wanafunzi ambao wanamiliki hizo simu zenye intaneti na huhitaji kuweka vocha kila siku sijui pesa wanapata wapi au ndo kundi jipya la utegemizi linaanza kuja sasa Tanzania?

Tukiendelea kutafakari zaidi, wanao nufaika na mitandao hii ya kijamii je ni kina nani? Je ni walaji au wazalishaji? Jibu rahisi hapa ni makampuni ya simu ya wawekezaji wa kibepari ndo ambayo hunufaika zaidi na mitandao hii ya kijamii na kuwaacha walaji kuwa maskini ama kwenda jela hasa baada ya kutungwa sera mpya ya matumizi ya mitandao mwaka 2015.

Hebu tafakari kidogo sera ya unyonyaji wa kibepari ni kuhakisha unapata faida kutoka kwa wavuja jasho wa hali ya chini mpaka wale wa juu ndio maana leo hii katika makampuni ya simu utaona viwango wa kujiunga kifurushi kinaanzia shillingi 250 za kitanzania wakiamini hata yule mvuja jasho wa hali ya chini kabisa anaweza kumudu.

Tujiulize kidogo juu ya unyonyaji huu ambapo wengi wetu yamkini hatuuoni ama tunapuuza, ni wangapi wetu tunaweza kukaa bila intaneti kwa siku nzima?

Kwa kuwa makampuni haya ya kibepari yaligundua hii ni sehemu ya kumfanya mtanzania kuwa maskini kwani wengi wetu bado tunavuja jasho kila kukicha ila hatufanikiwi, wameanzisha huduma za kukopa pesa ili upate intaneti halafu utalipa pindi uwekapo salio, je hii sio namna ya kuongeza umaskini kwa mtanzania?

Tuangalie aina nyingine ya umaskini uletwao na mitandao ya kijamii. Hivi tulishawahi kujiuliza mitandao hii ya kijamii imeasisiwa na nani na kwa manufaa ya nani?

Majibu yanaweza kuwa mengi hapa kutokana na kila mtu afikiriavyo, ila, hebu tuangalie ili kuweza kufanya ubepari ushamiri kirahisi ulimwenguni hasa nyakati hizi ni lazima kuwe na mfumo wa usambazaji ambao utafanya taarifa fulani kufika sehemu nyingi kwa wakati mmoja.

Leo hii tuna aina nyingi sana ya mitandao ya kijamii ambayo hutupa taarifa nyingi za kimagharibi ambazo wengi wetu huzifurahia na kuona ndizo zenye tija na kuona zile za kwetu kama zimepitwa na wakati.

Hebu tafakari kidogo, leo hii ukiingia mtandao wa Instagram na kuona Kim Kadashian kavaa nywele fulani bandia na kapendeza sana moja kwa moja nasi tunapenda kuwa kama yeye tunaanza kutafuta hizo nywele zenye thamani kubwa sana nasi tuwe kama yeye. Japo nywele hizo ukizivaa hazileti tija yoyote kwa maendeleo zaidi ya kutumia pesa nyingi ambayo ulivuja jasho muda mrefu kuipata, je huku sio kuendelea kuongeza umaskini kwa watanzania wanaotaka usasa na kuacha ukale kwani mitandao ya kijamii imeshaonyesha ili uwe wa kisasa ni lazima uvae nguza za namna fulani, uweke nywele za namna fulani, utumie manukato fulani.

Ambacho wengi wetu tunasahau sasa ni kwamba haya makampuni ya kibepari ya nywele bandia, manukato, nguo, pochi, kucha bandia wanatumia watu maarufu kuuza bidhaa zao ili sisi wanyonge tuone ndo mambo ya kisasa na kuanza kupapatika nayo mwishoe tunazidi kuwa maskini ili hali wao wakipata utajiri maradufu.

Huu ni ubepari wa hali ya juu, yatupasa kufikiria upya namna ya maisha yetu na kufanya mambo yenye tija ili kuweza kulikomboa taifa letu. Hapa utasikia watu wakisema sasa tufanyaje na ndo hali ya dunia inavyokwenda yatupata kwenda na kasi hiyo,

Wakati naandika makala haya, niliulizwa swali sasa unawashauri nini watanzania ili waepukane na unyonyaji huu? Nilimjibu ya kwamba sio mimi wakutoa majibu bali inatupasa kama taifa kuliona hili ili kuweza kulikomboa taifa kwa kuwa na mijadala kila mahali nchini kwani ukisema tufanye hivi utapata jibu la Haki za Binadamu.

Hebu sasa tuangazie upande wa mwisho wa umaskini uletwao na mitandao ya kijamii. Ili kuweza kutengeneza soko zuri kwa mabebari ni sharti kutengeneza taifa tegemezi ambalo litakuwa sio bunifu na mwishowe kuweza kutoa masoko ya uhakika.

Sasa hivi Tanzania kama taifa linavita kubwa sana ya kupambana dhidi ya mitandao ya kijamii kwani wengi wetu tumesha athirika kiasi kwamba ukikaa dakika mbili mbali na simu yako unajihisi mgonjwa. Tumekuwa walevi wa simu (addicted) kama wenye kutumia madawa ya kulevya au walevi wa pombe ambao hawaendeshi maisha pasi utumiaji wa vileo.

give phone breakKiuhalisia hebu jaribu kukaa na jamaa zako kama wanne mkiwa mahali katika mazungumzo ya jioni halafu angalia vile watu walivyokuwa karibu na simu zao kiasi kwamba meza inakosa mazungumzo kabisa kwani watu wako karibu sana na watu walio mbali na wao kuliko watu walio karibu na wao kiuhalisia.

Ukijaribu kuangalia hili kwa undani utakuta hata familia nyingi watoto wanakosa uangalizi mzuri kwani wazazi wakirudi nyumbani nao wako karibu sana na simu zao kuliko vile walivyo karibu na watoto wao.

Je hii sio aina nyingine ya umaskini? Kwani sehemu muhimu ya maendeleo ya binadamu ni kuhakikisha watu wanakutana pamoja kujadili maendeleo ya nchi yao kwa hoja.

Leo sote fikra zetu ziko kwenye kuangalia mitandao ya kijamii na kusahau kufanya mijadala yenye tija kwa taifa letu.

Mfano mzuri, leo hii kukitokea ajali kila mtu anataka kuwa mwandishi wa hababri wa kwanza kutoa taarifa ya tukio la ajali badala ya kuanza kuwaokoa majeruhi katika ajali hiyo.

Fikra zetu ndio mkombozi wetu kwani fikra zetu zinatuletea ubunifu katika maisha ili kuweza kufanya mambo yenye tija katika taifa ila kwa kuwa tumeukumbaitia ubepari kwa dhati, ubepari huo umeweza kuteka fikra zetu vizuri kiasi kwamba tunasahau kubuni mambo ya msingi ya jamii zetu na kubaki kuwa walaji wa yale yote yanayoletwa na nchi za magharibi tukiona yale wafanyayo kama kuwa sahihi zaidi. Mitandao ya kijamii imefanikiwa kuteka fikra zetu na ubunifu wetu na hivi ndivyo Tanzania itaendelea kuwa maskini.

Na Jacob Mulikuza

Jacob ni mtaalamu wa Sayansi ya Jamii

Leave a Comment