Kwanini hatuzioni kazi za wasomi wa sanaa wa Tanzania?

Mwigizaji Rich, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na mwigizaji Lulu (Picha kwa hisani ya blogu ya othman michuzi)

Mwigizaji Rich, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na mwigizaji Lulu
(Picha kwa hisani ya blogu ya othman michuzi)

Wiki moja au mbili zilizopita, jiji la Dar es Salaam lilizizima kwa habari njema na kugubikwa na mazungumzo pia “habari” za washindi wa “Tuzo” za sanaa ya uigizaji katika filamu. Hawa ni waigizaji “maarufu” wa “Bongo Muvi”.

Binafsi sikupata kusoma tahariri au makala yeyote iliyoandikwa kwa kina kuchambua nini hasa kimetokea na ni nani wamehusika katika kuandaa au kuwatuza “washindi”.

“Magazeti Pendwa”, ambayo wengine huyaita ya magazeti ya “Udaku” yalisheheni vichwa vya taarifa za “Ushindi” huo wa “wasanii wa bongo muvi”.

Sikushangaa kutoona maandiko makini juu ya “Tuzo” hizo kwani sidhani kama mwandishi makini wangaliweza kupata cha kuandika kutoka kwa “Washindi” wale. Uzito wa habari ya “Ushindi” wa “Wasani” hao umekuwa tofauti kabisa ukilinganishwa na tukio la kupatikana kwa Katibu Mkuu mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambapo tumeshuhudia chambuzi za kina, ndefu na makala makini katika vyombo vizito ya habari zimeandikwa na kutangazwa juu ya kupatikana kwa Katibu Mkuu mpya wa chama kikuu cha cha upinzani. Hilo halimaanishi kuwa sanaa sio muhimu, la hasha, bali ni kiashiria sawia, kwamba kuna tatizo sehemu fulani.

Kwa namna fulani, unaweza ukasema kilichotokea kati ya hayo matukio mawili ni kama vile waandishi wa habari husema “Mbwa kumng’ata Mtu si habari, bali Mtu kumwuma meno Mbwa ndio habari”!

Hapa kwetu,  Tanzania,  mpaka tunaingia mwaka 2015 mwezi februari, tulikuwa na taasisi kuu nne zinazotoa mafunzo ya sanaa ya maigizo kwa ngazi ya cheti, stashahada na shahada. Taasisi hizo ni; Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TaSUBa-kama kijulikanavyo sasa), Chuo cha Ualimu Butimba, Chuo Kikuu cha D’Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Butimba, imesitisha kozi ya masomo ya sanaa hapo mwaka jana (taarifa bado hazijathibitishwa rasmi). Tokea mwaka 1975 UDSM walifundisha sanaa, wakati Bagamoyo walianza mwaka 1981 na UDOM, chuo kipya walianza mwaka 2008, na walianza vizuri sana. Nimevitaja vyuo hivi vikubwa zaidi na vikongwe kwenye mafunzo hayo ya fani muhimu ya utamaduni nchini ili kuonyesha ni jinsi gani fani hiyo ni kubwa na muhimu sana katika maendeleo jumla ya utamaduni wetu.

Tumekuwa na wasomi wa fani ya maigizo (“Theater” au “Drama”) wengi sasa, hawapungui 500 kwa idadi yao. Kundi la Wasomi wa sanaa ni pamoja na wataalamu au wabunifu wa mavazi au maleba (costume), wabunifu wa mapambo (make-ups), wabunifu wa mandhari, waandishi wa hadithi na wapangiliaji wa uzalishaji pia waongozaji wa uzalishaji wa filamu/maigizo (directors). Swali kubwa hapa ni, wapo wapi hawa? Na kazi zao mbona hatuzioni?

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na maswali hasa toka kwa Watanzania bila kupatiwa majibu juu ya tansia ya sanaa. “Wasanii” maarufu katika tasnia ya filamu na maigizo ni watu ambao wengi wetu hujiuliza kama taaluma hiyo wameisomea au ni kwa jinsi gani ilitokea wao wakawa ndio watu wanaoshughulika nayo. Kuna baadhi ya kazi walizozalisha zinazua maswali mengi juu ya uwezo au kipaji cha waigizaji pia aina ya migogoro inayowasilishwa katika hadithi zao.

Kwa mfano,nizungumzie kidogo filamu iliyotengenezwa kwa jina la “UNCLE JAY JAY”. Nilitazama filamu hii nikiwa safarini, ilikuwa ikionyeshwa kwenye basi. Sikuelewa msingi wala haja ya kisa cha filamu ile wala madhumuni ya kutengenezwa kwake.

Filamu hiyo ilikosa hata kiwango kidogo kabisa cha fikra ili kutengeneza uwiano wa mazingira ya maisha halisi ya Kitanzania katika malezi ya watoto, na hata jinsi mtu mzima anavyohusiana na watoto iwe kwa mazuri au mabaya kama tunavyoyajua.

Nimeshindwa hata kujadili maudhui ya filamu ile kwa ufupi ili niendelee na ukosoaji wa kazi ile ya hovyo kwa kiwango cha kumuudhi yeyote ambaye amewahi kuona filamu inayoleta maana kwa muundo na maudhui yake.

Filamu za namna ile ni kiashiria tu cha kazi nyingi sana za filamu   ambazo zinaendelea kuzalishwa kila siku kwa namna ileile ikionekana kama ndio njia sahihi ya kufanyika kwa kazi za sanaa ya maigizo hapa Tanzania.

Jambo la kusikitisha ni kwamba katika kundi hili la wasanii hawa “wababaishaji”  wapo wale ambao angalau wamepata elimu katika ngazi ya shahada katika taaluma nyingine , sio sanaa. Nawazungumzia hao kwa kuwa labda wao kwa utashi na elimu waliyonayo hata wangeweza kujiuliza kama wanachofanya ni sahihi au la.

Jalada la filamu ya "Fake Pastors"

Jalada la filamu ya “Fake Pastors”

Filamu iliyoitwa “FAKE PASTORS” kwa kiasi fulani iliandikwa na iliongozwa na kijana ambaye alikuwa anasomea fani ya sanaa ya maigizo Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam wakati filamu hiyo ikitengenezwa. Cha kushangaza kijana yule, hakutumia taaluma aliyokuwa akisomea kusokota hadithi ile wala kuisimulia kwa picha zitembeazo.

Hivi kweli Tanzania tunatatizo la ajira kiasi kwamba msomi mwenye shahada moja anaishia kuwa msafisha viatu au muuza magazeti akikimbia mabarabarani?

Hicho ndicho kisa kilichopelekea wasomi hapo waliokosa ajira kuwa “Fake Pastors”, haya ni mawazo ya “Msomi Yule” ambaye alikuwa mwigizaji nyota wa “KAOLE GROUP” kabla ya kujiunga chuo kikuu.

Mafunzo aliyopata kikundini yalizidi na kufunika hata elimu aliyokuwa anaitafuta.

Binafsi nilihitimisha kwa kusema hakwenda kusoma bali kutafuta cheti pale chuo.

Katika filamu ile aweza kusema mbunifu wa mwanga na madhari kwa kiwango chake alijitahidi kuibeba hadithi ile hata ikapata kuonekana kwa jinsi ilivyo.Sikushangaa hilo kwani mbunifu wa madhari na mwanga katika filamu ile ni msomi wa sanaa kutoka Chuo cha Sanaa Bagamoyo.

Filamu kama “Teenage” ni shida kuanzika katika jina la filamu lenyewe na hatimaye hata hadithi ambayo kwa kiwango fulani inatambulishwa na jina ambalo linamfanya mtazamaji ategemee kitu fulani kuhusiana na maisha ya balehe kwa vijana wadogo.

Waigizaji wa “bongo muvi” ni vigumu kuwachambua na kuwaelewa kwa misingi ya taaluma ya uigizaji kwani wanapingana na mengi sana katika fani hiyo!

Ukiacha kazi mbalimbali ambazo zipo sokoni na pia zinaweza kupendwa sana na wananchi (si lazima kupendwa kwa kazi kumaanishe zina ubora kadiri ya taaluma ya sanaa) ambazo kwa uchache nimemudu kugusia. Kazi za wasanii wasomi zimekuwa hazionekani sana au kuwa gumzo kwa wananchi kwasababu;

Mosi, aina ya mafunzo wanayopata wasomi wa sanaa ya maigizo katika taasisi hizi yanawaandaa watu hawa kufanya kazi zao kwa utaalamu na kuzingatia kanuni ili wazalichasho kiwe bora na kiakisi utaalamu ulitumika nyuma yake.

Kwa mfano; Ili wazalishe igizo au filamu, lazima kuwe na hadithi iliyoandikwa vizuri kitaalamu na itimie kwa vigezo vyake vya uzuri (mgogoro, ujuzi katika uigizaji, ubunifu katika mapangilio wa visa na matukio, burudani katika matendo na maneno ya hadithi na pia mafunzo yatokanayo na hadithi) pia muda wa onyesho kama vile muda wa saa moja au masaa mawili.

Hadithi lazime ichezeke katika umbo maalumu ili ifae kuonyeshwa jukwaani au katika filamu.

Elimu yao inawalazimu wasanii wasomi kuzalisha Igizo au Filamu kwa kuzingatia mahitaji ya uzalishaji hasa fedha za kununua au kukodisha vifaa mfano: nguo, mapambo, ukumbi au mahali pa kuigizia, usafiri; kutengenezesha/kukodi vitu vya kuigizia kama vile silaha na hata mazingira ya kufikirika.

Pia wasomi hawa wanafundishwa kuigiza kwa kufuata mwongozo hadithi iliyoandikwa (script) na sio kuropoka maneno binafsi.

Kila neno katika hadithi hupangiliwa kwa maana na namna yake ya kutamka na hata hali ya kulitamka (furaha, kimahaba, kwa huzuni au hali ya kupagawa) ili litoe mana kusudiwa.

Ukumbi wa TaSUBa wa kazi za sanaa (Picha kwa hisani ya tovuti ya TaSUBa)

Ukumbi wa TaSUBa wa kazi za sanaa
(Picha kwa hisani ya tovuti ya TaSUBa)

Igizo au filamu vinatakiwa kufanyiwa mazoezi (rehearsals) mara kadhaa kabla ya kuwasilishwa kwa watazamaji na hatimaye kuonyeshwa jukwaani au kurekodiwa katika mikanda ya video au DVDs/CDs.

Kwa ufupi nisema kazi ya uzalishaji wa sanaa ya kisomi inataka mpangilio wa kitaalamu na ki-soko kwa maana ya maandalizi ya kukamilisha na kuendeleza uzalishaji. Kama hakuna utaalamu au udhamini wa kutosha katika maandalizi ya kuzalisha Igizo au Filamu, ni MWIKO kwa msomi huyo hata kujaribu kuzalisha kazi ya sanaa kwani kwa namna yeyote iwayo kazi hiyo haitatimia.

Kama nilivyoainisha hapo juu kundi la wasomi wa sanaa linajumuisha  wataalamu au wabunifu wa mavazi au maleba (costume), wabunifu wa mapambo (make-ups), wabunifu wa mandhari, waandishi wa hadithi na wapangiliaji wa uzalishaji. Wasomi hawa kwa namna hii ya mafunzo hawapo tayari wala hawawezi kujaribu kufanya chochote katika kazi yao kwani wanaelewa madhara ya kufanya hivyo.

Kumlazimisha msanii msomi kuzalisha katika mazingira ya dhiki, ni sawa na kumwambia daktari afanye upasuaji kwa kutumia upanga pia atumie miti shamba kukamilisha kazi yake, kitu ambacho ni tofauti na taaluma itakavyo.

Ikumbukwe kuwa maigizo na filamu ni sanaa za kigeni toka ulaya na huja na kanuni zake. Taaluma ya sanaa ya uigizaji ni pana sana, sio rahisi kama wengi wanavyoichukulia kwa “uzoefu” wa kuangalia yanayoonyeshwa na “wasanii wa bongo muvi” katika luninga zetu!
Sababu ya pili muhimu niwadhamini (producers) wa kazi za sanaa, hasa wamiliki wa maduka ya filamu na vituo vya luninga ni kikwazo kwa uzalishaji wa kazi za kisomi.

Kama nilivyosema hapo juu, uzalishaji wa kitaalamu unahitaji pesa (tena pesa nyingi), ukiachia kukidhi mahitaji ya uzalishaji pia kuna malipo ya wasanii na wataalamu waandaaji wengine wa uzalishaji wa kazi za sanaa.

Televisheni binafsi na huria zilipoanza kuonyesha maigizo na filamu za wasanii wa Kitanzania zilianza kwa kuwalipa wasanii nafasi ya kupata umaarufu, sio malipo ya pesa baada ya kufanya kazi.

Hili ni uthibitisho tosha wa hali duni za “wasanii” wa maigizo wengi wa TV “waliostaafu” au kufa masikini lakini wakiwa na majina makubwa kuliko wao wenyewe walivyo.

Wasanii wasomi walikimbilia kufanya kazi za miradi ya kutoa elimu kwa maigizo au filamu kwani wadhamini huko walitoa pesa za maandalizi na malipo ya kazi kwa wasanii. Filamu kama “Rama”, “Chumo”,(iliyoandaliwa na wasomi na kuigizwa na wasanii wengi wa bongo muvi) ni mifano sahihi.

Wasomi wa sanaa hawatafuti umaarufu wafanyapo kazi yao ya sanaa, wanatafuta pesa (ndio maana katika mafunzo yao wanabanwa na kipengele cha maadili ili kutafuta kwao pesa kusivuke mipaka wakatengeneza kila watu watakacho kama vile ponografia).

“Wasanii” wengi wa “bongo muvi” hawajasomea popote fani hiyo waipendayo, wao walijiingiza huko kutafuta umaarufu (majina ya uigizaji yamegeuka kuwa majina yao halisi) na sasa labda wameanza kutafuta “pesa”, sina hakika na hilo.

Wawili tu au watatu waliosomea sanaa wanatokea na mawazo za tofauti kidogo.

Kazi zao nyingi ni duni ki-utaalamu na pia maadili yatokanayo na filamu zao ni mabaya hata mchango wao katika maendeleo ya utamaduni na ustawi wa jamii ni duni zaidi.

Ikumbukwe sanaa ya Tanzania inakusudiwa kuelimisha, kukosoa, kuburudisha na kukumbusha jamii yale yote yanayostahili kuenziwa au kuachwa.

Hakuna fikra za kina katika hadithi za filamu zao nyingi, hawafanyi tafiti ili kuzalisha hadithi bora na za kusisimua, pia hawawekezi vya kutosha katika uzalishaji wenye tija kwa mlaji au msambazaji.

Matumizi ya mchanganyiko wa lugha (vichwa vya kiingereza na hadithi za Kiswahili) ni viashiria vya ukosefu wa utaalamu, kukosa uzalendo na uelewa mdogo wa misingi ya fani husika katika utamaduni wao.
Haya mambo ya TUZO ni upepo wa “Magazeti na TV” pendwa ambavyo havina wataalamu wa kuupatia umma tathmini au taarifa za kutosha ili kustawisha vyote: Wasanii, sanaa na jamii ya wapenda sanaa.

Tuzo kama ambayo wameipokea wasanii wetu wa “bongo muvi” huko Naijeria tuzo hizo zimepokelewa na zaidi ya wasanii 100 wa fani mbalimbali. Tofauti na Tanzania, Naijeria hakukuwa na mchecheto wala upepo kama uliovuma hapa bongo ingawa wasanii wa Naijeria wametimia katika mengi ukilinganisha na wababaishaji wetu.

Hivi tunapojiuliza “tuzo” walizopokea hawa wenzetu ni za nini tunaweza kusema kwa hakika tunachosifia? Je vigezo vya kuzawadia tuzo tunavijua? Kama sisi tungekuwa tunatoa tuzo, je filamu hizi tungezipatia tuzo? Kwa lipi?

Kuna msanii mmoja zaidi naye amepata tuzo kwa kuandaa filamu yake pamoja na “hawa wawili wa bongo muvi” Je tunamjua? Mbona hajajitokeza wala kutangazwa na vyombo vya habari ingawa filamu yake tayari imekwisha kuonyeshwa Tanzania, Kenya, Uganda, Ujerumani na Uingereza na kusemwa ni bora sana? Huyo ni msomi anajua afanyalo.

Tunapendekeza na kushauri, watu wasome ili wafanye kazi zao kwa utaalamu ili zilete tija kwao binafsi na jamii yetu kwa ujumla. Na pundi kusoma inashindikana, basi wanaweza wakaendesha kazi zao za sanaa kwa ushirikiano wa karibu na wataalamu wa sanaa ili kuzinoa vyema kazi hizo.

Pia watazamaji wanashauriwa waache uvivu wa kusema ukweli, hivi hadithi zote tunazozijua, au filamu zote za kizungu na za kihindi tulizoziona hazijatuwezesha kutambua tofauti ya nini bora na nini kibovu?

Tukumbuake kama ilivyo katika hadithi za mama na mwana, filamu au maigizo haviishii kuwapatia wazichezao umaarufu tu!

Wenye masikio na wasikie!

Na Dominicus Makukula

Makukula ni msomi na mtaalamu wa sanaa

Leave a Comment