Mchakato wa Uchaguzi Mkuu na mianya ya kikatiba

KatibaSerikali iliporidhia hoja ya katiba mpya na kuanzisha rasmi mchakato huo kupitia sharia ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011, wadau mbalimbali walionyesha wasiwasi wao juu ya mchakato huo kutekwa na wanasiasa kwa maana ya ushiriki pamojan na maudhui yake. Kiuhalisia ni ngumu kutenganisha uhusiano wa karibu kati ya katiba na siasa. Katiba ni andiko la kisiasa ki maudhui na hata mchakato wa upatikanaji wake ni jambo la kisiasa hata kama ukusanyaji wa maoni utajumuisha watu wote katika jamii. Msingi wa hoja hii upo katika maana ya katiba yenyewe. Kwa maneno machache katiba inatafsiriwa kama waraka unaoweka makubaliano baina ya watawala na watawaliwa juu utaratibu wa kutawala katika jamii husika.

Kuna baddhi ya mambo ambayo yalijitokeza kama mapungufu ya kikatiba ambayo hata hivyo watu waliokuzwa katika utaratibu wa katiba ya zamani hawakusita kuyapinga. Mambo hayo ni pamoja na suala la uteuzi wa mawazi na uendeshwaji wa serikali katika namna ambayo shughuli za serikali haziathiriwa na siasa. Mambo haya hayakuonekana kukubalika miongoni mwa watawala haswa ukizingatia kuwa Tanzania imewahi kupita katika mfumo wa chama kimoja ambacho kimeendelea kuwa madarakani hata baada ya miaka zaidi ya ishirini ya mfumo wa vyama vingi kuanzishwa.

Kupitia michakato ya kisiasa haswa tukijaribu kuangazia kinachoelea katika hekaheka ya kuwania kuchaguliwa kwa wagombea hapo octoba 25, tunaweza kujiridhisha kwamba maoni ya wanachi yalikuwa na mashiko kwa kiasi kikubwa. Nitazungumzia mambo matatu katika Makala hii, moja ni uteuzi na utendaji wao, mbili na kuhusu tume huru ya uchaguzi na tatu ni kuhusu madaraka ya bunge na mamla ya rais katika mwaka wa uchaguzi.

Wakati wa mchakato wa ukusanyaji wa maoni kuhusu katiba mpya, wananchi wengi na hata tume ya jaji warioba iliridhia kuwa mawaziri wasitokane na wabunge kama katika yetu ya sasa inavyosema. Hoja hii ililenga kuweka msingi wa kwamba mawaziri wafanye kazi kama watalaamu watakowajibishwa na Bunge na si kama wanasiasa ambao pamoja na mambo mengine watakuwa wanasimamia maslahi ya vyama vyao. Pia, msingi wa hoja hii ni kutaka kutenganishwa wabunge na maslahi ya serikali ukilinganisha na hali ya sasa ambapo wabunge ambao ni mawaziri badala ya kufanya kazi yao ya kuisimamia na kuikosoa serikali wao wanaitetea.

Wakati tuko katika kipindi cha kueleka katika uchaguzi ukomo wa majukumu ya mawizir bado ni utata kikatiba. Bunge limeshavunjwa na kwa manti hiyo ni Dhahiri mawaziri ambao bado wanaendelea kutimiza majukumu yao ya serikali ni kinyume na katiba kwani kigezo cha kuwa waziri kikatiba sharti uwe Mbunge. Tunaendeleaje kuwa na mawaziri katika kipindi ambacho hatuna wabunge?. Mawaziri wanaomaliza muda wao pia wamekuwa wakitumia nyadhifa zao kisiasa kitu ambacho si sahihi. Katiba lazima iweke kipindi cha mpito cha kutokuwa na mawaziri haswa nyakati kama hizi ambapo nchi iko katika mchakato wa kutafuta viongozi wapya.

Uhuru wa tume ya taifa ya uchaguzi pia ni mihimu ukaendelea kufanyiwa kazi haswa ikizingatiwa kuwa mchakato wa kutafuta katiba mpya tumeuweka kiporo kupisha uchaguzi mkuu. Uongozi wa juu uliopo katika tume kwasasa ulitokana na uteuzi wa Rais anayemaliza madaraka yake ambaye mpaka sasa bado ni mwenyekiti wa chama chake na anakipigia kampeni. Wakuu wa mikoa na wilaya ambao watakuwa wasimamizi wa uchaguzi mkuu katika ngazi husika nao ni wateule wa Mwenyekiti wa chama kimoja wapo katika mchakato. Ni siku chache sana kuelekea uchaguzi mkuu bado kumekuwa na uteuzi ikiwemo uteuzi wa kamishna wa uchaguzi, na kupanguliwa kwa wakuu wa mikoa na wilaya sambamba na kuteuliwa kwa wengi. Mambo kama haya yanaleta maswali juu ya uhuru wa tume. Ni muhimu maboresho ya katiba yakaweka bayana juu ya ukomo wa kiongozi anayeondoka madaraka kufanya uteuzi unaongilia utendaji wa tume ya uchaguzi katika mwaka wa uchaguzi.

Jambo ambalo lilisahaulika na mchakato huu unatukumbusha, utaratibu wa bunge kutunga sharia zinazohusiana na uchaguzi katika mwaka wa husika. Mwaka 2010, sheria ya kudhibiti gharama za uchaguzi iliburuzwa haraharaka sana na uhusishwaji wadau haukuwa mzuri. Ukisoma kwa ukamini sheria ile utagundua kuwa lengo ilikuwa ni kuwakomoa wapinzani ambao walikuwa wakikodi vifaa vya kufanyia kampeni. Takribani miswaada mitano ilikimbizwa Bungeni mapema Februari chini ya hati ya dharura. Hata hivyo miswaada hiyo yote haikuwa na udharura wowote. Mswaada wa Sheria ya mitandao, sheria ya takwimu, sheria ya vyombo vya habari na Sheria ya utangazaji wa maudhui ya kisiasa yote lengo ni kufunga mianya yote ya kupashana habari. Habari picha, habari takwimu, habari maandaandishi na habari siasa zote zimedhibitiwa. Sheria hizi zikikosolewa kwa kina na wadau mbalimbali lakini ngumu kuonekana kama kuna kasoro kwa wahusika ambao dhamira yao ilikuwa ni kukidhi maslahi ya kisiasa.

Kwa mara kwanza tunajiwekea uratibu wa kutotoa matokeo ya kura ya maoni siku 30 kabla ya uchaguzi mkuu wa hofu za kisiasa katika nchi ambayo imetumia pesa nyingi kusomesha watalaamu mbalimbali wakiwemo watafiti na wachambuzi wa kisiasa. Tunakuwa na sharia ambazo zinalazimu watu kuzungumzia uchaguzi  katika vipindi vinavyorushwa moja kwa moja lazima wawe wawakilishi wa vyama na ni lazima wawe kutokana pande mbili tofauti. Sharia kama hizi zinapitishwa ilihali ikifahamika kuwa kuna vyama huwa vinakataza wagombea wake kushiriki midahalo ama vipindi vinavyorushwa moja kwa moja kama mkakati wa kisiasa. Inafahamika fika kwamba kuna kundi kubwa la wanataaluma ambao shughuli yao ni chambuzi wa kisiasa, hawa nao wasizungumzia uchaguzi?. Haya ni mambo ambayo yanatokana na katiba kutokuwa wazi juu ya utungaji wa sheria haswa katika mwaka wa uchaguzi mkuu.

Na Constantine Deus

Constantine ni mtafiti na mchambuzi

Leave a Comment