Natafuta habari

camera.jpg_resized_460_

Bado nahangaika,

Bado ninazunguka,

Hadi kiatu kinabanduka,

Natafuta habari.

Nimesikia habari,

Namuuliza askari,

Anasema hana habari,

Natafutaa habari.

Kama mwandishi,

Napita njia hatarishi,

Hadi kwenye kambi za jeshi,

Nikitafuta habari.

Nishawahi kukutwa,

Usiku kucha nikakung’utwa,

Vitu vyote nikapukutwa,

Nikitafuta habari!

Nikatumwa nchi za mbali,

Kwenda kusaka habari,

Maisha yakawa kamari,

Natafuta habari.

Nikafika ukanda wa Gaza,

Vita vimetanda ni “ua galagaza”,

Mabomu yametawala kila nilipojilaza,

Natafuta habari.

Ewe mwanahabari,

Ebu jihadhari,

Unapokuwa kwenye hatari,

Ukitafuta habari!

Manufaa kwa taifa lote,

Manufaa kwa bara lote,

Manufaa kwa dunia yote.

Ntaendelea kutafuta habari!!

Na Naamala Samson,

Naamala ni mshairi kijana na miongoni mwa waratibu wa La Poetista anapatikana Dar

2 Comments

  1. Bwana Mushi says:

    Zuri sana shairi hili. Kaza kaka!

  2. Costantine Deus says:

    shairi zuri kijana, niko napanga vina ili namini niweze kulitupia langu hapa

Leave a Comment