Riwaya ya Kizungumkuti: Sura ya kumi

Kizungumkuti

Dar es Salaam

Alhamisi, Juni 5, 2003

 

 

“Mambo?”

“Poa tu Atu.  Nipe stori best.”

“Sina stori best.  Nilitaka tu kufahamu tunakutania wapi?”

“Basi tukutane hapo Sugar Rays

“Poa.  Basi usichelewe.”

Baada ya kuzungumza na Atu kwenye simu, Ali akaendelea na shughuli zake.  Hakuwa amekutana na Atu tangu arudi safari ingawa wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara kwa simu.  Walipanga kukutana Alhamisi hii kwa sababu Atu alikuwa katika mapumziko.

Ali aliamua kupanda daladala.  Akashuka Sokota na kuingia baa ya Sugar Rays.  Atu hakuwa amefika.  Alipokuwa akimsubiri Atu jambo likamjia akilini.  Anamfahamu Hafsa kwa kuotea mambo.  Hofu yake ikawa endapo angepiga simu angeshindwa kujitetea juu ya mahali alipo wakati huo.  Akaonelea ni heri kuizima simu yake.

Atu alipoingia aling’ara mno tofauti na mara ya mwisho walipokutana.  Leo alionekana mrembo hasa.  Suruali yake ya jinsi ya rangi ya bluu ikisindikizwa na fulana nyepesi ya kike nyeupe yenye kukatwa mabegani.  Nguo hizo zilirandana sawia na umbile lake lenye mapaja makubwa huku akiwa amefungasha wowowo la haja  kiasi cha kuwafanya watu wengine mle baa kuguna pindi alipoingia.  Umbo la Kinyakyusa haswa.

“Hee!  Kumbe ushafika?”

“Si kitambo sana.”

“Pole jamani.”  Atu aliposema hivyo akamshika mkono kiasi cha kumwinua kitini.  Wakakumbatiana.  Wateja wengine wakaendelea kumkodolea macho ya tamaa na wivu.  Walipoketi wakaagiza vinywaji na nyamachoma huku wakiendelea na maongezi mawili matatu.

“Mhuu!  Hebu niambie Ali, nd’o nini kuniletea mapozi hivyo mwana wa mwenzio?”

“Huishiwi tu maneno Atu?  Mapozi  gani nimekuletea swahiba wangu?”

“Wewe kila siku nikikuomba tukutane hukosi sababu.”

“Siyo sikosi sababu.  Wewe mwenyewe unafahamu hizi kazi zetu za kujiajiri zilivyo.  Unakula kutokana na juhudi zako.  Ni kwa sababu tu natingwa na biashara.  Si kwamba nakuletea pozi.”

“Sawa bwana.  Lakini si useme tu ukweli kama Hafsa anakuzuia?”

“Wala.”

“Ila?”

“Ni kama nilivyokwambia.  Ni mambo tu ya biashara.”

“Haya bwana.  Enhee, niambie mkeo umemwacha wapi?”

“Nani?  Hafsa?”

“Usitake kunichekesha Ali.  Kwani wewe una wake wangapi?  Una mwingine zaidi yake?”

“Hakuna kitu kama hicho.”

“Tuelezane ukweli basi.”

“Nina mke mmoja tu.  Naye ni Hafsa.”

“Lakini hujajibu swali langu Ali.”

“Swali gani tena?”

“Umelisahau mara?  Nimekuuliza mkeo umemwacha wapi?”

“Ahaa!  Amesafiri muda mrefu sasa.  Yupo Iringa.”

“Yupo maternity leave?

No.  Ameamua akapumzike tu.  Si unajua Benito bado anaendelea na mambo yake ya kijinga….”  Ali akakatishwa na mhudumu aliyekuwa akiwaletea nyamachoma waliyoiagiza.  Baada ya kunawa mikono yao, na mhudumu kuwa ameondoka, Ali akaendelea na maongezi.

“Unasikia Atu; Benito amediriki kwenda hadi shuleni kwa Hafsa.”

“Patamu hapo.  Enhee, halafu ikawaje?”

“Unaona patamu eeh?  Hajafanikiwa kuonana naye kabisa.  Yule mtoto Hafsa ana machale sijapata ona.”

“Kivipi?”

“Basi tu inamtokea.  Mara nyingi sana anayaepuka majanga kimtindo mtindo tu.”

“Kwa hiyo unataka kuniambia kwamba hata sasa anaweza kufikiria kukupigia simu?”

Yah!  Why not?  Nafahamu hivyo na ndiyo maana nimeamua kuizima.”

Atu akacheka kwanza.  Kisha akaongea.  “You are so funny.  Umeizima kwa sababu unaogopa Hafsa akijua upo nami ataanzisha msala ama unaogopa kitu gani?”

“Sivyo unavyofikiria.  Bali nimeona bora niizime kwa usalama ili nizungumzapo nawe nisiwe na hofu.  Nimekosea?”

My God!  We haya wee!  Unanipaka mafuta kwa mgongo wa chupa?”

“Hayo unayasema wewe.”

Anyway, tuachane na hizo stori.  Hafsa ni mke wako, shurti umuheshimu.  Napenda kufahamu, kwa nini kuna uhasama baina yenu na Benito?”

“Unakumbuka siku ile pale Mawenzi Garden nilikwambiaje?”

“Uliniambia kuwa wasaa ukiruhusu utaniambia.  Unataka kusema bado haujakuruhusu?”

“Haswaa.  Bado Atu.  Kama nilivyokueleza ni hadithi ndefu sana.  Ipo siku, ipo tu siku utaijua.”

“Haya bwana mshindi wewe.  Wanasema subira yavuta heri.”

Wakaendelea kuagiza vinywaji.  Wote wakaagiza bia ya Safari ambayo ni maarufu sana nchini.  Kwa muda waliokaa pamoja, wakawa wamekwisha zoweana sana.  Hawakuzungumza tena hadi awamu nyingine ya bia ilipoletwa.  Kila mmoja alionekana kuzama kwenye tafakuri jadidi.

“Enhee Ali, nakuomba wikendi hii tutoke pamoja.”

“Sitopata nafasi kwani Jumamosi nitakwenda Iringa.”

“Kufanya nini?”

“Kwa Hafsa.  Kwa kuwa tupo mbali mbali, tumekubaliana mimi kwenda mara kwa mara.”

“Ushaenda mara ngapi tangu urudi safari?”

“Nimekwenda mara moja.  Nimerudi Jumapili.”

“Kwa hiyo utapata hasara kama utaahirisha kwa wikendi hii moja?”

“Hapana.  Lakini atajisikia vibaya sana.  Anahitaji sana kuniona.”

“Anahitaji?  Kwani wewe huhitaji kumwona?”

“Ulimi hauna mfupa bibie.  Nami nahitaji pia.”  Atu akacheka kusikia hivyo.

“Ulipaswa kusema hivyo.  Ali, najua hata nikikubembeleza vipi huwezi badili ratiba yako.  Ninahitaji sana kutoka nawe.  Lakini sina uwezo wa kukulazimisha.”

“Siyo suala la kunilazimisha Atu.  Tunakaa chini tunaelewana.  Ni jambo la kuelewana tu.”

“Nafahamu hivyo.  Nina ombi jingine.  Hili naamini litakubaliwa.”

“Ombi gani?”

“Naomba nikualike kwa chakula cha jioni kesho nyumbani kwangu.”  Atu alizungumza huku macho yake yakiwa kwa Ali kwa shauku tele ya kujua atakalojibiwa.

“Nitaangalia kama nitapata nafasi.”

“Nilijua tu.”  Sauti ya Atu ikashuka, ikawa yenye kunung’unika zaidi, macho yakiwa mapole.  “Ali, isije ikawa unaona nakusumbua sana.  Kama ratiba yako haikuruhusu, sawa.  Nitajitahidi kuelewa.”

“Usiumie Atu.”

“Kumbe unajua naumia?  Mimi sina maneno zaidi.  Wewe nenda zako Iringa salama urudi salama.  Siku utakayopata nafasi, namba yangu unayo.  Utanipigia simu.”

“Kwa ajili yako, kesho nitapata nafasi.”

“Wow!”  Furaha iliyochanganyika na kutoamini ikaujaza uso wa Atu.  Ukang’aa na kuakisi tabasamu lake la huba.

Maongezi yalikuwa mengi sana wakipeana michapo ya hapa na pale huku wakila na kunywa.

Muda ulipowatupa mkono wakaagana.

Ali akaiwasha simu mara tu alipoachana na Atu.  Akazungumza na Hafsa.  Alipofahamu kuwa Hafsa hakumpigia simu, moyo wake ukatulia.  Njia nzima wakati akirudi nyumbani kwake alikuwa akijaribu kutafakari maongezi yake na Atu.  Hakuona jambo la msingi lililomfanya Atu kubembeleza kukutana naye.  Pamoja na hayo, alijikuta akiyafurahia maongezi yao.  Maswali mengi yakaanza kumtawala, nini maana ya mambo haya?

Siku iliyofuata Ali alikuwa Kariakoo katika shughuli zake kama kawaida.  Kazi nyingi zilimfanya kutotawaliwa na mawazo ya mkutano wake na Atu siku iliyopita.  Hali yake ya moyo ilikuwa tofauti sana.  Alijihisi mwenye furaha sana.  Hakujua furaha hiyo ilitokana na nini.

Jua lilipokuwa likiangukia magharibi, akafunga duka lake.  Akakanyaga mafuta hadi barabara ya Nyerere.  Muziki laini ulikuwa ukimtumbuiza kutoka katika redio ya gari lake.  Alipofika Tazara akaikamata barabara ya Mandela hadi Sokota alipoingia barabara ya Temeke.  Alikuwa ameelekezwa na Atu kuwa akunje kushoto akifika usawa wa Temeke Hospitali.  Akayafuata maelekezo hayo.  Akasimama karibu na mti wa mkungu baada ya kuingia Temeke Wailes.

Akampigia simu Atu.  Atu akatoka kwenye nyumba iliyokuwa ikitazamana na mti huo.

“Karibu sana, sana Ali.”

“Ahsante sana.  Nimeishakaribia.”  Atu akamshika Ali mkono wake na kumwongoza kuingia ndani.  Walipita kwenye korido refu kiasi.  Ali akatambua hiyo nyumba ni ya wapangaji wengi.  Walipotokea uani kulikokuwa na vyumba vingine, akina dada watatu walikuwa wakiendelea na soga.  Wakanyamaza ghafla kumwona Atu na mgeni.  Wawili walikuwa wakiosha vyombo huku mwingine akiuchambua mchele ulikokuwa kwenye ungo alioupakata.

Ali akawasalimia wakati akiendelea kutembea kuingia katika mlango alioongozwa na mwenyeji wake.  Chumba kilikuwa na ukubwa wa wastani.  Kulikuwa na seti moja ya sofa.  Kabati kubwa lililosheheni vyombo.  Meza ya kioo pamwe stuli zake.  Ali alifurahishwa na uzuri wa sebule hiyo ambao uliendelea kupambwa na seti ya televisheni kubwa ya inchi 29 na redio kubwa ya kisasa ya kuweka santuri tano za diski.  Kama haitoshi, jokofu refu la milango miwili na jiko la umeme la kuoka.

Ali alibaki kutumbulia macho kwa kufurahishwa na maendeleo hayo.  Kwa kazi ya uaskari, alitarajia kuona vitu vya kawaida tu.  Ndani ya moyo wake alijaribu kukisia kama ni jitihada binafsi, ama mfuko wa mtu uliokuwa tayari kutoboka ili kumridhisha mrembo huyu wa Kinyakyusa.

Wakati Ali akiendelea kutafakari, Atu akamsemesha.

“Karibu sana Ali.  Nimefurahi mno kwa kuitikia kwako mwaliko wangu.  Unajua nimefurahi hadi naishiwa maneno.”

“Nadhani mimi nimefurahi kukuzidi.  Nakushukuru sana kwa kunialika kwako.”

“Usijali.  Enhee, tena nisije nikasahau.  Umewaona mabinti hao hapo nje?”

“Yah.”

Take care rafiki yangu.”

“Kwani umenionaje?”

“Aaaaah!  Usikasirike dear.  Ni lazima nikupe tahadhari.  Watoto hao ni machepele moto wa kifuu una nafuu.  Wasione suruali hawana dogo.  Na ukizingatia umekuja na gari, basi balaa.  Ni wazuri mno kwa kuwatazama, lakini ni sumu.  Wawili hapo tayari wamethibitika kuwa na ngoma.  Tafadhali, mezea tu kama mate yatakujaa mdomoni.”

“Sidhani kama…..”  Ali alikatishwa na hodi iliyopigwa.  Akaingia msichana mojawapo wa wale watatu.  Alikuwa amejifunga kanga hadi juu kifuani.  Sehemu ya juu ikiwa wazi.  Kanga hiyo iliishia usawa wa magoti.  Iliuchora vema mwili wake.  Kwa rangi yake ya machungwa, mate yangemjaa yeyote.  Alipoingia tu hakuisha kupepesa macho yake huku na kule.

“Samahani da’Atu.  Naomba niazime kisu chako nimenyee nyanya.”

“Mbona nimekiacha hapo karoni!”

“Ahaa!  Basi ahsante.”  Akaondoka kwa madoido utadhani yupo katika mashindano ya ulimbwende akishindana mikogo na wenzake.  Ali akamtazama Atu aliyekuwa akitabasamu kwa mbali.

“Nimeamini maneno yako Atu.”

“Umeamini eeh?  Mana ungedhani kuna kitu nakubania.  Ni bora umejionea mwenyewe.”

Atu akaendelea kuandaa chakula mezani ilhali Ali akinywa bia aliyoandaliwa.  Maongezi ya hapa na pale yalikuwa yakiendelea.

“Ushawahi kufika mitaa ya huku Ali?”

“Mara nyingi sana.  Nikitoka uwanja wa Taifa kucheki mechi huwa kunakuwa na foleni sana.  Hivyo uwa naua boda la huku.  Naingilia pale katikati ya kituo cha mafuta na kambi ya jeshi, kisha natokea hapo Temeke hospitali.  Kisha huyo zangu hadi Yombo, kisha Vingunguti halafu napasua Tabata Baraccuda boda kwa boda hadi Kimanga.”

“Kumbe nd’o maana hujapotea.”

“Tanzania hii hii?  Siwezi kupotea Tanzania hii.  Ukimuuliza mtu njia anakuelekeza bila shida.”

“Na kweli.”

“Hivi Atu, hapa unaishi peke yako ama?”  Uvumilivu ukamshinda, akaamua kuuliza.

“Peke yangu kivipi?  Sijakuelewa.”

“Namaanisha mdogo wako ama msichana wa kazi.”

“Nipo alone.  Msichana wa kazi wangu wa kazi gani?  Sina mume wala mtoto, huyo housegirl aje kufanya nini?”

“Ukiwa kazini nani anakusaidia kazi za ndani?”

“Kazi zenyewe zipi? Kufua?  Kusafisha nyumba?  Kupika?  Mimi ni mtoto wa kike bwana.  Nikitoka kazini siwezi shindwa kuzifanya.”

“Na ukirudi umechoka?”

“Naziweka pending hadi uchovu upungue.”

Chakula kikawa tayari mezani.  Atu akamnawisha Ali mikono.  Akampa kitambaa kisafi cheupe kujifutia mikono.  Akampakulia ndizi zilizopikwa vema kwa kuchanganywa na nyama ya ng’ombe.  Kisha akampakulia vipande vya kuku vilivyokaangwa.  Wakati akiendela kupakua, tayari mate yalikuwa yamemjaa Ali mdomoni.  Zilikuwa ndizi Uganda, chakula akipendacho zaidi.  Atu alipomaliza kupakua sahani ya kwanza, akasogeza stuli mahali alipoketi Ali na kuiweka.

“Karibu chakula Ali.  Nimekupikia chakula cha kwenu Mbeya.”

“Ahsante sana dear.”  Aliposema hivyo, Atu akashituka kidogo.  Pengine hakuamini, akataka kuthibitisha.

“Eeh?”

“Ahsante sana Atu.”  Ali hakusema neno hilo tena.

“Haya baba, ahsante sana kushukuru.”  Atu akawa anapakua sahani nyingine kwa ajili yake.

“Atu, umesema umepika chakula cha kwetu Mbeya.  Kwani we’ mwenzangu kwenu wapi?”

“Iringa.  Sijui mtaa unaitwaje vile?  Niambie basi pale kwa wazazi panaitwaje?”

“Kwa hiyo unamaanisha nini?”

“Nakutania mwaya.  Usije ukakasirika bure furaha yangu ikatoweka.  Kwetu Mbeya, kwani we’ hujui?”

“Nilitaka tu nikusikie ulichokikusudia kukisema.  Aisee Atu, hiki chakula ni kitamu mno.  Sijui utamu wake niulinganishe na nini?”

Atu hakujibu neno.  Alipomaliza kupakua chakula chake, akaenda kuketi pembeni ya Ali.  Chumba kikawa kimya kwa muda fulani.  Kila mmoja alikazana kuzungumza na sahani yake.  Ali aliufurahia sana mlo huo, uliomkumbusha Mbeya kwa mama yake.

“Umejifunzia wapi mapishi matamu kama haya?”

“Kwetu baba.”

“Hongera nyingi kwa waliokufundisha.”

“Zimefika.”

Muda mfupi baadaye wakawa wamemaliza kula.  Atu alipomaliza kuondoa vyombo mezani akarudi kuketi akiwa ameongeza vinywaji vingine.  “Ahsante sana Atu, naona leo umeniandalia dhifa ya kirafiki kweli.”

“Nafurahi kama umefurahia.   Hujaniambia Ali, safari yako ya kesho ipo ama tutatoka?”

“Mmh, ipo.  Ila hata Hafsa sijamwambia kama nakwenda.”

“Kumbe hata hajui kama unakwenda.  Kwa nini usighairi ili uende wiki ijayo?”

“Kwa nini basi nawe usiighairi hiyo kesho ikawa wikendi ijayo?”

“Mimi nipo hapa na wewe upo hapa.  Ama hufahamu kuwa fimbo iliyo mkononi ndiyo iuayo nyoka?”

“Ukimaanisha?”

“Nini?  Ninachomaanisha ni kwamba,”  Atu akavuta pumzi kwanza,akaendelea, “Kwa kuwa mimi nimekuomba tangu jana basi ungelizingatia ombi langu.  Siyo kwamba siyo muhimu wewe kwenda.  Bali,as long as Hafsa hafahamu unatarajia kwenda, sidhani kama itakuwa vibaya.  Kwa sababu hutohitaji kutoa sababu za kwa nini hukwenda.”

“Atu.”

“Beeh!”  Atu akatazamana na Ali.

“Usifikiri ni rahisi hivyo kumshawishi  Hafsa aelewe kitu kama hicho.  Ratiba yangu ya kazi anaifahamu.”

“Haya Ali umenishinda.  Usijali, tutatoka pamoja siku nyingine.  Nimekuelewa.”

Ikawa imetimu saa tatu unusu.  Ali akaaga aondoke akapumzike mapema ili aweze kuwahi safari yake.  Alipoinuka kitini Atu akamkumbatia na kumbusu kwenye paji lake la uso.  Alipomaliza akashusha pumzi zake kwa nguvu.  Ali hakusema kitu.  Akaunyanyua mkono wa kulia wa Atu.  Akaubusu nyuma ya kiganja.

“Ahsante Ali.”  Atu alishukuru kwa sauti hafifu mno.  Ali hakujibu kitu.  Wakati wanatoka, Atu alimshika Ali mkono wake wa kushoto kwa mkono wake wa kulia huku wakitembea.  Pale uwani waliwakuta wale mabinti wakila chakula.  Miguu yao waliitandaza sakafuni hata kuzuia njia. Ali ana Atu walipokuwa wanapita, wakaikunja miguu yao haraka haraka huku mmoja wao akiyaanika mapaja yake kwa sehemu kubwa.  Ali na Atu hawakupoteza muda wao kwao.  Ali akatoa tu kauli ya kuwaaga.

“Karibu tena shemeji.”  Utadhani wametambulishwa kuwa ni shemeji yao.  Ali na Atu tayari wakawa kwenye korido refu wakielekea nje. Walipolifikia gari, Ali akaliegemea na kuishika mikono ya Atu.

“Ahsante sana Atu.  Nimeifurahia sana jioni ya leo pamoja.”

Atu hakujibu.  Macho yake yote yakimtazama Ali.  Hisia kali sana zikiupeleka puta moyo wake.  Walitazamana kwa nukta kadhaa.  Ali akajikuta naye moyo wake ukienda joshi.  Akamvuta Atu kifuani kwake.  Akampiga busu muruwa juu ya mdomo wake.  Akamwachia haraka.  Akafungua mlango wa gari lake na kujitoma ndani akimwacha Atu akiwa haamini kilichotokea.

Atu akasimama ameganda akimtazama Ali anapoondoka.  Machozi yakiwa yanamlenga lenga, akashindwa kuunyanyua mkono wake kupunga mkono wakati Ali akifanya hivyo kumuaga.

Ilikuwa ni siku nzuri sana kwake.

…………..itaendelea

Na Fadhy Mtanga

Mtanga ni mtunzi wa kitabu cha riwaya, HUBA anayepatikana Dar es Salaam. Unaweza mfatilia katika mtandao wa Twitter kupitia: @FadhyMtanga na kupata kitabu chako cha HUBA kwa namba: +255 (0)715 599 646

 

Leave a Comment