Riwaya ya Kizungumkuti: Sura ya 12

KizungumkutiDar es Salaam

 Jumapili, Juni 8, 2003

 

Maulid hakuwa ameonana na dada yake kwa muda wa siku mbili.  Hii ilitokana na yeye kuwa nyumbani kwa akina Ali pindi Ali alipokuwa safarini Iringa.  Alipomaliza shughuli za usafi na kufungua kinywa, aliamua kwenda kwenye mkahawa wa mdahalishi uliokuwa karibu na mahali hapo.  Huko alitumia saa moja kufanya mambo kadha wa kadha ya kwenye mtandao.

Alipokuwa anakaribia kumaliza, akapata ujumbe kutoka kwa dada yake kupitia simu yake ya mkononi.  Dada yake alikuwa akimsalimu.  Akamwambia amemkumbuka sana.  Maulid akaamua kwenda kuonana na dada yake alipotoka hapo.

“Mambo vipi bro?

“Safi best.  Shikamoo.”

“Marahaba.  Ndiyo nini kunisusa hivi?”

“Aah jamani!  Siku mbili tu nd’o unaona nimekususa?”

“We’ unaona mbili chache?”

“Sasa nyingi hizo?”

Zuhura na Maulid walikuwa wamepishana miaka mitano kuzaliwa.  Lakini tangu wangali wadogo waliondokea kupendana sana.  Walizaliwa wao peke yao kwa baba na mama yao ijapokuwa baba yao tayari alikuwa na watoto wawili wengine wakati akioana na mama yao.  Kaka zao hao, Shaban na Abdulaziz hawakuwa karibu kabisa na familia yao.  Hiyo ikawafanya kujiona kama wapweke.  Shaban alikuwa akifanya kazi kama mhasibu katika Bodi ya Pareto nchini, ilhali Abdulaziz alifanya kazi kama mkaguzi wa mahesabu wa kujitegemea akimiliki kampuni pamoja na wenzake.  Kaka hao wawili hawakuwa na msaada wowote kwa Zuhura na Maulid hata baada ya wazazi wao kufariki miaka mingi iliyopita kwa ugonjwa wa UKIMWI.  Hadi kifo chake, baba yao alikuwa meneja mkuu wa kiwanda cha kutengeneza matairi ya magari cha Vaculug mjini Iringa.  Maulid akamwona Zuhura kama baba yake, mama yake.

Zuhura na Maulid walizoweana kupita kiasi.  Ikafikia wakawa kama mapacha, wakati mwingine wakawa wanaitana Kulwa na Doto.  Maongezi yao mara nyingi sana yalikuwa yakitawaliwa na utani.  Hivyo Maulid anapokosekana nyumbani humpa dada yake unyonge kwa kiasi kikubwa sana.  Siku ambazo Maulid hukosekana nyumbani kutokana na kuachiwa nyumba na akina Hafsa, kwa Zuhura hazikuwa siku za furaha.  Isingekuwa mahusiano mazuri ya tangu na tangu kati ya Zuhura na Hafsa, Zuhura asingekubali zoezi hilo.

“We’ unaona chache eeh?  Mwenzio nilikumiss sana pacha wangu.”

“Hata mimi nilikumiss mshikaji.”

“Ungenimiss kweli usingenichunia hivyo.”

“Sikuwa na dola kwenye simu.”

“Acha uongo Doto.  Mimi sikukupa pesa?  Ali hakukupa?”

“Sasa si zina kazi nyingi?”

“Shika adabu yako.  Sisi tunaokupa, kwetu hazina kazi nyingi?”

“Aaah jamani!  Hata hutaniwi?”

“Tatizo lako hujatulia.  Unaona hasara hata kuniandikia meseji?  Hata mademu zako unawachunia hivi hivi?”

“Ushaanza.  Tatizo lako wewe nalijua.  Kila siku nakwambia.  Dawa yako ndogo sana.  Ukiolewa utaacha kunimiss miss ovyo.”

“Thubutu!  Labda siyo mimi.”

“Kwani we’ siyo mwanamke kama wengine?”

“Pamoja na hayo.  Mwanaume nitakayekutana naye nina meno yangu thelathini na mbili mdomoni?  Hata siku moja, hatoweza kunifanya nisikukumbuke kaka yangu, tuliyezaliwa tumbo moja.  Sisi wawili peke yetu.”

“Mmh!  Mara ngapi tunaona watu wakishaolewa wanawatupa ndugu zao?”

“Hao unaowazungumzia ni watu wengine.  Wewe mwenyewe ndani ya nafsi yako unaelewa vema Zuhura hawezi kufanya hivyo.”

“Aah wapi!”

“Alaa kumbe!  Nishaelewa mpenzi wangu.  Kumbe ndiyo itakavyokuwa wewe ukishaoa.”

“We, we, weh!  Wakikusikia watu watakucheka.  Mimi nikutupe wewe?  Mimi huyu huyu ama mimi fotokopi?”

“Wewe wewe!”

“Ngumu sana.  Ngumu mnoooooo!”

“Leo unasema ngumu kwa kuwa tupo pamoja.  Unanithamini, nakuthamini.  Lakini kesho utakapooa hutopata muda hata wa kuniita tena Kulwa.”

“Siwezi Kulwa.  Mimi siwezi haki ya Mungu kufikia hatua hiyo.”

Never say never.  Subiri utakapowekewa limbwata, tuone kama utamthamini tena Zuhura.”

“Najua Kulwa hiyo huwa inatokea.  Lakini utakapoona nimechange ghafla, si itakubidi uchunguze kulikoni?”

“Aka mwenzangu!  Hapo si nd’o n’takapoanza kuitwa wifi hasidi.  Nitavaliwa hadi kanga na maneno yake na taarabu niimbiwe.”

“Kama ndivyo, si bora hata nisioe?”

“Acha utoto wako Doto.  Usioe unataka nini?”

“Nisiwe mbali na wewe.”

“Utoto huo rafiki yangu.  Ukikuwa utauacha.  Kwa taarifa yako, mimi navuta muda umalize kusoma.  Ukimaliza mimi huyoooooo!”

“Mungu wangu!”

“Habari ndiyo hiyo!”

“Tatizo lako Kulwa unachonga sana.”

“Kwani we’ hupendi kunisikia ninavyochonga?”

“Pamoja na hayo.”

“Huko kuchonga ningekuwa sijibiwi nawe ningekuwa nishalifunga domo langu kitambo.”

“Unachonga hata unashindwa kunikaribisha ndani?  Muda wote tumesimama utadhani wasoma mita wa Tanesco wamekuta mlango umefungwa.”

“Mmh, we mtoto!  Mbona mdomo wako una nguvu utadhani unatumia kitunguu swaumu?”

Siku zote maongezi yao huwa ni marefu.  Wakaingia ndani wakiwa na furaha kwa kuwa pamoja.  Zuhura hakuwa ameolewa.  Alilazimika kuachana na mchumba wake Jafari mwaka mmoja uliopita.  Jafari alikutwa na Zuhura na mwanamke mwingine kwenye nyumba ya kulala wageni huko Sinza.  Jafari alikuwa na mazowea ya kwenda huko kwa kuwa ni mbali na aishiko Zuhura.  Kuna mfanyakazi mwenziwe Zuhura akawa anamwona.  Uvumilivu ukamshinda, akamtonya rafikiye.  Zuhura hakufanya ajizi.  Baada ya songombingo hilo, Zuhura akaamua kutulia kwanza.

Maongezi yakaendelea wakati wakipata mlo.

“Hivi Doto siku ile hukunimalizia vizuri.  Ulisema Benito alikuja tena shule?”

“Yah!  Lakini unajua mi’ bado simwelewi.”

“Huwezi kumwelewa mdogo wangu.”

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Kwa sababu hufahamu sababu.”

“We’ unaifahamu?”

“Wewe nawe?  Mara ngapi nikwambie naifahamu?”

“Sasa kama unaifahamu kwanini usinisimulie ili nitoke kizani?”

“Hafsa asingekuwa amekuahidi kukusimulia, ningekusimulia.  Kwa kuwa amekuahidi akili yake ikitulia atakwambia, huna budi kuvuta subira.  Isitoshe mimi sifahamu kwa undani anaoufahamu dada yako.”

“Aah jamani!  Nimegee japo kiduchhu.”

“Nitakupunguzia utamu.  Hutokuwa na hamu tena ya kumsubiri mwenyewe akusimulie.  Na atakapokusimulia, hutokuwa na shauku kubwa.”

“Niambie basi best.  Unajua mimi nakosa…..”  Maulid akakatishwa na mlio wa simu yake kuashiria ujumbe umeingia.

Sorry, ngoja nisome meseji.”

“Wow!  Kutoka kwa wifi?”

“Si mpaka awe!”

“Acha uzushi bro.

Maulid akaufungua na kuusoma.  Alipomaliza, akatabasamu.

“Vipi, mbona tabasamu kubwa?”

“Hakuna lolote.  Kuna mtu kanitumia meseji tukutane pale Lucky Pub saa kumi na moja.”

“Nani huyo?”

“Hajaandika jina ila amesema tunasoma darasa moja.  Najua ni msichana tu huyu.  Si’ unajua tena watoto wa kike skuli wananipeperushia bendera mbaya mno!”  Maulid akaongea kwa majigambo.

“Hata kama.  Mimi nakushauri usiende.”

“Ndiyo nini sasa Kulwa?  Leo hatuna ratiba ya kutoka.  Kwa nini usiniruhusu mimi niende?  Pale siyo mbali.  Nitawahi kurudi jamani.  Ama utajisikia mpweke sana?”

“Siyo suala la kujisikia mpweke.  Wewe mtu aliyekutumia meseji humfahamu.  Bado unataka kwenda kichwa kichwa?”

“Dah!”  Maulid alionesha kukata tamaa.

It’s ok.  Kama unataka kwenda, mpigie simu aliyekutumia hiyo meseji ili umfahamu kwanza kabla ya kuamua kwenda.”

“Dah!  Simu yangu haina dola.  Ngoja nikacheki vocha mara moja.”

“Acha kushobokea mambo mtoto wa kiume.  Haya, tumia simu yangu.”

Maulid akaichukua simu ya Zuhura.  Akainakiri namba iliyomletea ujumbe kwenye simu yake.  Alipoipiga ikaita kwa muda mrefu, ndipo ikapokelewa na sauti ya kike.

“Haloo!  Nani mwenzangu?”

“Unaongea na Maulid.”

“Ahaa!  Mambo vipi kijana?  Umepata meseji yangu?”

“Nimepata.  Kwani we’ ni nani?”

“Mmh!  Acha kunizingua Mau.  Ina maana hujaitambua sauti yangu?”

“Ningeitambua nisingekuuliza.”

“Haya basi yaishe.  Mi’ ni Lydia.”

“Sasa mbona umetumia namba tofauti?”

“Mi’ simu yangu imechapika.  Nimetumia ya sister angu.”

“Nami yangu ipo tee.  Nimetumia ya rafiki yangu.”

“Mbona unaongelea puani bibie. Vipi?”

“Nina mafua mwanangu usipime.  Niambie basi, utakuja nikupe ofa?”

“Umeziokota wapi faranga zinazokupa jeuri?”

“Usiulize maswali.  Wewe fuata nyuki ule asali.”

“Niking’atwa?”

“Na nini?”

“Na nyuki?”

“Utajiju.  Utakuja?”

“Bila kukosa.”

Bye!  Till then.”  Simu ikakatwa.

Zuhura akamkazia jicho mdogo wake.  Wakati anaipokea simu yake, moja kwa moja akatazama salio.  Kisha akamshambulia kwa maneno.  “Nani alikuwa?”

“Ni best yangu tunasoma naye.”

“Nd’o ukaamua kunimalizia dola zangu kwa maongezi yenu marefu yasiyo na kichwa wala miguu?”

“Siyo hivyo best.  Samahani kama umekwazika.  Sikuwa na maana hiyo.”

“Usijali.  Kwa hiyo utatoka?”

“Ndiyo.  Ama wasemaje?”

“Kuna la kusema hapo?

Waliporejea kwenye maongezi yao, habari za Benito zikawa zimesahauliwa.  Mchana ulipowadia wakapata mlo wa pamoja.  Wakashirikiana kufanya usafi wa vyombo vilivyotumika kwa chakula.

Ilipotimu saa kumi na moja kasoro dakika ishirini, Maulid akaondoka nyumbani akimwacha dada yake katika hali ya upweke.

“Usichelewe basi Doto.”

“Sitochelewa.”

“Pitia basi kuniaga kabla hujaenda Kisukulu.”

“Hata usingesema lazima ningepita kukutakia usiku mwema.”

“Ahsante mdogo wangu.”

Maulid akawa anaondoka.  Zuhura alisimama mlangoni.  Kichwa chake alikiegemeza ukutani akimtazama Maulid anapoondoka.  Alianza kuhisi hali ya upweke.  Aliendelea kumtupia jicho mdogo wake hadi alipopotelea kwenye kona baada ya nyumba ya tatu.  Zuhura akaendelea kusimama hapo kwa dakika nzima nyingine.  Akaufunga mlango na kuingia ndani.  Alijisikia mnyonge sana kiasi kwamba hakutamani kufanya kitu chochote.

Aliongoza hadi chumbani kwake.  Akajitupa kitandani.  Kichwani mwake aliyafikiria maisha yake na mdogo wake.  Alifikiria maisha yao baada ya kufariki kwa wazazi wao.  Akafikiria jinsi kaka zao walivyowatenga kama hawawajui vile.  Akafikiria habari za mchumba wake wa zamani, Jafari.  Fikra hazikwenda mbali sana, usingizi ukamchukua.

Hakuwa ameamka hadi simu yake ilipoanza kuita.  Awali alidhani anaota.  Akili ilipomkaa vema akatazama saa ya ukutani iliyokuwamo chumbani humo.  Ilisoma saa mbili na dakika ishirini na saba.  Akajiuliza kama Maulid alipita ama laa.  Akahisi pengine alipita na kumkuta usingizini na kuamua kutomsumbua.  Lakini hiyo haikuwa desturi ya Maulid.

Simu ikaendelea kuita.  Akili yake haikuwa kwenye simu bali kwa mdogo wake.  Milango aliifunga.  Kama kweli alipita, alijuwaje kuwa amelala?  Na kama aliona imefungwa, kwa nini asigonge?  Ama bado alikuwa kwenye miadi yake?  Ndilo swali lililofuatia kichwani mwake.  Na kwanini alikuwa nje hadi muda huu?  Hasira zikaanza kumpanda kichwani mwake.

Alipoikumbuka simu iliyokuwa ikiita muda mrefu pasipo yeye kuipokea, akaichukua kutoka ilipokuwa.  Akaitazama namba ya mpigaji.  Namba ilikuwa ngeni kwake.  Akasita kuipokea huku akili nyingine ikimshawishi kuipokea.  Woga ukamvaa ghafla hata asijue umetoka wapi.  Ghafla mikono yake ikaanza kutetemeka.  Akajitahidi, akaiweka simu sikioni.  Mpigaji alikuwa na haraka kweli.

“Ni Zuhura wewe?”  Akauliza akionesha kutawaliwa na mashaka.

“Ndiyo.  Kwani ni nani mwenzangu?”

“Njoo huku Bima.  Njoo Muslim hospital.”

“Hospitali?  Kuna nini?”

“Njoo haraka Maulid amelazwa.”

“Maulid?”  Aliuliza huku machozi yakiwa tayari yanamdondoka.  Alipojaribu kuuliza tena, simu ilikuwa imekatwa.  Zuhura akachanganyikiwa.  Akaanza kulia.  Akaketi chini sakafuni akijaribu kuiaminisha akili yake hiyo ni ndoto tu.  Alilia kwa takribani dakika tano mfululizo.

Aliponyamaza, akaichukua simu yake.  Akaitafuta namba ambayo Maulid aliipiga asubuhi.  Alipoipata akaipiga lakini haikuwa ikipatikana hewani.  Akaifungua droo ya meza yake ya urembo.  Akachukua kiasi fulani cha pesa.  Akaifunga vizuri milango ya nyumba.  Akaondoka kwa kasi hadi kituo cha teksi.  Teksi ikamkimbiza hospitali.

Alipojitambulisha, alipelekwa hadi chumba alichokuwa amelazwa Maulid.  Alimkuta kafungwa bandeji kichwa kizima na mkono wake wa kushoto.  Zuhura hakuweza kumtazama mara mbili.  Alijikuta akilia kwa kwikwi nyingi.  Muuguzi wa kike aliyekuwa kando yake alijitahidi sana kumbembeleza na kumsihi asilie zaidi bila mafanikio.  Baadaye wakalazimika kumwondoa chumbani humo na kumweka mapokezi.  Kilio chake hakikukoma.

Alipotulia, alijaribu kuwadadisi wauguzi juu ya masahibu ya mdogo wake.  Hakuna aliyekiri kufahamu.  Maelezo waliyokuwa nayo ni kwamba, aliletwa na wasamaria wema walipomwokota dakika chache baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana na kutupwa katika mtaro wa maji.  Maelezo ya wauguzi yakaongea kuwa Maulid ameumia sana maeneo ya kichwani na kuvunjika mkono wake wa kushoto.  Wakamwambia inawezekana alivunjika mkono huo wakati akidondokea kwenye mtaro huo.

Pamoja na kuiona hali ya Maulid, Zuhura hakutaka kabisa kuamini lile ni tukio la kweli na siyo ndoto.  Alihisi mazingaombwe ndiyo yaliyokuwa mbele yake.  Asingeweza kuamini ilhali alikuwa na Maulid hadi saa kumi na moja kasoro akiwa bukheri wa afya njema.  Alipoondoka nyumbani hakutegemewa kufikwa na mambo yale.

Hadi saa nne unusu usiku alikuwa bado ameshikwa na bumbuwazi.  Akili yake ilipomrejea vema, akakumbuka kitu kimoja.  Nacho ni kuwajulisha Ali na Hafsa ambao kwake, wamekuwa ni kama ndugu.  Simu ya Hafsa ikaita sana pasi kupokelewa.  Alipoona haipokelewi, akaamua kumpigia Ali.  Hiyo ilipokelewa ingawa baada ya kuita sana.  Alipojibiwa kuwa Ali angewasili mchana wa siku inayofuatia.  Kidogo akapata faraja.

 

 

*******************

 

 

Maulid alipoondoka nyumbani alikomwacha dada yake aliongoza moja kwa moja njia iliyotokea Lucky Pub.  Aliiona hali ya dada yake wakati akiondoka.  Akajipa moyo, muda si mrefu atarejea katika hali ya kawaida.  Haikumchukua muda mrefu akawa amefika mahala pa miadi aliyokuwa nayo.

Alipoingia akaongoza hadi kwenye kona ya upande wa kulia.  Akaketi na kuagiza soda ya Coca Cola.  Akawa anainywa taratibu akimsubiri Lydia.  Hadi soda inaisha Lydia hakuonekana.  Hakujali, akamini ni ahadi za Kiswahili, lakini lazima atatokea madhali yeye ndiye aliyepanga miadi hiyo.  Akaagiza soda nyingine.

Maulid akaitazama saa yake.  Dakika ishirini zilikuwa zimeyoyoma baada ya saa kumi na moja.  Akamwita mhudumu.  Akamwomba amnunulie muda wa hewani kibandani nje ya Pub hiyo.  Alipoletewa na kuingiza kwenye simu yake, akampigia Lydia.

“Mambo Maulid?”  Sauti ya Lydia ilikuwa yenye furaha na ya kawaida tofauti na asubuhi alipodai kuwa na mafua.

“Safi.  Ishu niaje?”

“Bomba mbaya.  Maajabu ya Musa haya.  Leo umenipigia simu?”

Maulid akashikwa na bumbuwazi.  Akafikiri haraka. “Lydia?”

“Sema handsome boy.”

“Unataka kuniambia kwamba wewe siye niliyeongea naye kwenye simu leo asubuhi?”

“Hee!  Ulinipigia?”

No.  Uliniandikia meseji, then nikakupigia kwa simu ya sister.

“Acha masihara yako Mau.”

I’m serious Lydia.”

“Mungu wangu!  Mimi sijaongea nawe leo.  Mbona sikuelewi?”

Anyway, inawezekana siyo wewe.  Kuna mtu ananifanyia ubandidu.”

“Kwani kasemaje huyo mtu?”

“Usijali tutaongea zaidi kesho.  Sina kiwese cha kutosha kwenye simu.”

“Poa bwana.  Lakini siyo vizuri hivyo.  Unaniweka roho juu.”

“Usikonde kimwana.  Ni mambo madogo tu.  Kesho.”  Maulid akakata simu.

Akaijaribu ile namba iliyotumika kutuma ujumbe.  Haikupatikana.  Akili ikamruka.  Maswali mengi yakawa kichwani mwake.  Akajiuliza sana ni nani anayeweza kumfanyia mchezo huo.  Akatazama pande zote, asione mtu yeyote mwenye kuelekeana na sauti ya mtu aliyezungumza naye asubuhi.  Hakika ikawa moyoni mwake sasa hakuzungumza na Lydia.

Akazingatia sauti ya mtu wa asubuhi, tofauti na ya Lydia.  Hivyo akatambua mtu huyo alizuga kudai ana mafua.  Alipofikiri kwa makini zaidi, hofu ikamjaa.  Akahisi kwa vyovyote vile, aliyemtumia ujumbe anayo sababu anayoijua mwenyewe, na pengine yenye madhara kwake.

Ni sababu gani hasa?  Hakuwa na jibu kichwani mwake.  Alipofikiri tena, tayari moyo wake ulikuwa ukienda mbio sana.  Wazo lililomjia ni kujaribu kuondoka mahali hapo haraka sana na kurudi nyumbani.  Tayari ilikuwa saa kumi na mbili kasoro dakika ishirini.  Akainuka kuelekea kaunta.  Akazilipia soda zake.  Akawa anayafanya haya kwa haraka haraka akiwa na hofu tele.  Akatazama tena pande zote.  Hakuona mtu wa kumtilia wasiwasi.  Akataka kuwahi kuondoka.

Alikuwa tayari keshachelewa.

 

 

*******************

 

 

Ijumaa hiyo ya tarehe tano mwezi Juni, Benito hakuamka na furaha kabisa.  Maongezi yake na Johari usiku uliopita hayakumpendeza kabisa.  Ingawa Johari alikuwa amezungumza ukweli, ambao hata yeye aliutambua, bado aliona Johari hakuwa sahihi.  Kila alipofikiri zaidi, hasira nazo zilimwongezeka.  Akaona Johari hayupo upande wake.  Kutokana na ukaribu wao kwa miaka mingi, alidhani angemsaidia kwa urahisi

Akili yake ikamvurugika zaidi pale alipompigia simu Johari ili kukamilisha mpango wao.  Johari akamjibu asingeweza kwenda kutokana na kikao cha dharura ofisini kwao.  Benito hakuamini hilo.  Alielewa fika Johari ametumia sababu hiyo kama gia ya kumkwepa.  Hakuwa na namna, isipokuwa kukubaliana na hali halisi, ingawa ni kwa shingo upande.

Akapokea ujumbe kwenye simu yake ya mkononi kutoka kwa Thomas wakati akitoka nje ya hoteli aliyofikia ili kuita teksi.  Thomas akamtaarifu wao wamekwishapita Ipogoro wakielekea Dar es Salaam.  Hii ilimaanisha tayari amelichelewa basi alilopaswa kupanda ili aungane na wenzake.  Akamwambia dereva teksi amkimbize Ipogoro utadhani anataka kuliwahi basi ambalo limekwishapita.

Alipofika kituo cha mabasi, akasubiri walau apate basi lolote.  Mabasi yote yalipita yakiwa yamejaza abiria.  Akasubiri zaidi ya saa moja.  Ndipo likatokea Shabiby la kwenda Dodoma.  Humo akabahatika nafasi.  Akaamua kupanda hilo hadi Morogoro ambako angepata mabasi ya Dar es Salaam kwa urahisi.

Alishuka Msamvu Morogoro huku njaa ikimwuma kweli.  Hakuwa ametia kitu chochote tumboni mwake siku hiyo.  Hakuwa na hamu ya kula chochote.  Hata hivyo alijikuta akijilazimisha kula kitu ili kulinusuru tumbo lake lililokuwa likiunguruma safari nzima kutokana na njaa.

Akaenda katika moja ya vibanda kituoni hapo.  Abiria walikuwa ni wengi wakisubiri usafiri kuelekea pande toafauti tofauti.  Akaagiza soda na vipande vya mkate ili kuituliza njaa.  Ndani ya kibanda hicho, msichana mmoja alimkazia sana macho Benito tangu alipoingia.  Yeye hakuwa amemzingatia wala kumwona. Akanywa haraka soda yake.

Wakati akitoa pesa kulipa, ndipo akamwona msichana huyo.  Waliangaliana kwa sekunde kadhaa.  Kila mmoja akijaribu kuvuta kumbukumbu ni wapi alimwona mwenzake.  Kumbukumbu ikagoma kichwani mwa Benito.  Akampuuzia.  Akaamua kuondoka.  Akamsikia msichana yule akimwita.

“James!”

Halikuwa jina lake.  Lakini kumbukumbu yake ikafanya kazi ya ziada.  Akalikumbuka jina hilo.  Akakumbuka kuhusiana nalo.  Akageuka na kumtazama msichana huyo.  Sasa akamkumbuka vema.  Alimwona siku aliyokwenda shuleni Kamene.  Alikuwa mmoja ya wanafunzi aliozungumza nao.

“Wow!  Mambo vipi sister……”  Akajibaraguza kama amepitiwa na jina, kumbe hakulifahamu.

“Naitwa Lydia.  Mambo safi kabisa.  Vipi wewe?”

“Mie nipo poa.  Niwie radhi hata sikukutambua.”

“Wala usijali.  Nami nilijua hujanikumbuka.  Siku ile tulikuwa wengi pale.”

“Ni kweli.  Vipi mbona upo hapa?”

“Nasubiri basi nirudi zangu mjini.  Vipi na wewe upo hapa?”

“Mie pia nasubiri basi.  Nilikuwa Dodoma, hapa nataka kuunganisha na basi jingine.”  Benito akadanganya, akiwa na sababu zake.

“Hee!  Kumbe tupo pamoja?”

“Yah.”

“Unategemea kupanda basi gani?”

“Nasubiri Hood.  Itawasili muda si mrefu kutoka gereji kwao.”

“Nadhani haitokuwa vibaya kama tukiungana kwenye safari.”

“Itakuwa poa sana.”

Mara basi likawasili kituoni hapo.  Benito na Lydia wakaungana na abiria wengine.  Wakapanda basi tayari kwa safari ya Dar es Salaam.  Wakawa wameketi kwenye siti ya pamoja.  Njia nzima wakasimuliana habari mbalimbali za maisha.  Lydia alikuwa ni mzungumzaji mzuri.  Ungeweza kudhani wanafahamiana kwa ukaribu kwa muda mrefu.  Benito akayafurahia sana maongezi safarini yaliyomfanya kufahamu pia kwamba Lydia anasoma darasa moja na Maulid.

“Enhee!  Nimekumbuka James, hivi ulishaonana na mwalimu Hafsa?”

“Hapana Lydia.  Sikupata tena nafasi.  Nilikuwa safarini tangia kipindi kile kile.”

“Pole sana.  Lakini sasa ukija hutomkuta.”

“Kwa nini?”  Benito akauliza kama asiyefahamu Lydia anamaanisha nini.

“Hayupo pale tangu wiki za mwisho za kufunga shule.  Yupo Iringa.”

“Amehama ama?”

“Mimi wala sifahamu vizuri.  Ila kwa mujibu wa tetesi zilizoenea pale shuleni,, ni kwamba anaweza asirudi tena.”

“Kwa nini sasa?”

“Kwa nini asirudi?”  Lydia akamtazama Benito kama hana hakika na swali.  Benito akatingisha kichwa ishara ya kuwa hilo ndilo swali lake hasa.  Lydia akamjibu.  “Yanaongelewa mengi sana hadi unashindwa kushika lipi na kuacha lipi.”

“Ni mambo gani hayo?”

“Achana nayo.  Maadamu hayana hakika siwezi kuyazungumzia.  Kwani wewe na mwalimu mnahusiana vipi?”

“Hakuna lolote zaidi ya kuwa nilipata kusoma naye.”

“Kwa hiyo tangu mmalize shule hamjawahi kukutana tena?”

“Hatujakutana kabisa.”

“Kwa hiyo hata hufahamu kuwa alishaolewa?”

Benito akatulia kidogo.  Akatafakari ni jibu lipi lingemfaa Lydia.  Haraka akachomoa kitambaa mfukoni mwake na kujifanya anapiga chafya.  Alifanya hivyo ili kujipa muda wa kulifikiria jibu linalofaa kwa wakati huo.  Wakati anakikunja vema kitambaa chake na kukirudisha mfukoni, ndipo akajibu.

“Hata sifahamu kabisa.  Kaolewa na nani?”

“Bradha mmoja anaitwa Ali.  Mume wake anampenda sana Hafsa hadi watu wote wanaowajua wanafahamu hivyo.”

“Aisee!  Lakini hata Biblia inamkumbusha mwanaume wajibu wake wa kumpenda mkewe.  Unajua nini?  Nyie wanawake mmeumbwa ili mpendwe.”

“Makubwa!”  Lydia akaangua kicheko cha kuridhishwa na maneno ya Benito.

“We’ unayajuwaje haya?”

“Alaa!  Mimi tena?  Kuna janki ninasoma naye darasa mmoja anaitwa Maulid.  Yeye yupo close sana na familia ya mwalimu.”

Hapo napo Benito akahitaji kutega vema nyavu zake.  Akaona hapo ndipo pa kupata habari nyingi zenye kumsaidia.  Akaendelea kujaribu kubahatisha.  “Ahaa!  Maulid namfahamu vema.  Alikuwa mdogo sana kipindi hicho.  Nilikutana naye siku moja.  Kila mtu alikuwa fasta sana.  Akanidokeza kwa kifupi kwamba anasoma Kamene.  Si unamzungumzia yule mdogo wake Hafsa?”

“Ndiye.  Lakini siyo mdogo wake toka nitoke.  Ila wamekuwa family friends tangia utotoni mwao.”

“Sasa si ndiyo undugu huo Lydia?  Wewe ulitaka wazaliwe tumbo moja ama wawe mabinamu?”

“Kumbe!  Wala sivyo udhanivyo.  Nami nafahamu hivyo isipokuwa nilitaka kutoa maelezo ya kina.”

“Usijali.  Nami nilikuwa najaribu tu kuujengea hoja undugu huo waliojiwekea.”

Furaha na matumaini yakaanza kuujaza moyo wa Benito.  Lakini bado alihitaji kutumia mbinu zaidi za maneno ili kuyafikia malengo yake.  Awali hakujua ni nini hasa anachokihitaji kutoka kwa Lydia.  Kwa hiyo jinsi maongezi yalivyokuwa yakipamba moto, ndivyo naye alivyokuwa akilimaizi hitaji lake.  Sasa Benito akafahamu anahitaji kitu gani  kufahamu huko kukamfanya kuwa mjanja na mwangalifu.  Alijua kwa uangalifu zaidi mambo yake yangejinyoosha katika mstari anaouchora yeye.  Aliamini atakipata alichokihitajialili zilikuwa hivyo.

“Halafu sasa, siku nimekutana naye akanipa namba yake.  Simu yangu haikuwa na chaji ikawa imezima.  Nikaiweka namba yake kichwani.  Nilipojaribu kuikumbuka tena sikuweza.”

“Pole sana.  Kwa hiyo hunayo tena.”

“Sikuikumbuka kabisa yaani.”

“Nikupe?”

“Aisee!  Nitashukuru sana rafiki yangu.”

Nini tena?  Tayari amefanikiwa kukipata kitu alichokihitaji kutoka kwa Lydia.  Madhali anaipata namba, mambo mengine yangejipa mbele ya safari.  Alitamani hata kupiga makofi kwa kuweza kumwua tembo kwa ubua.  Wakati Benito akishangilia ndani ya moyo wake, Lydia akapekua orodha ya namba za simu katika simu yake.  Alipoipata akampa Benito ili ainakili kwenye simu yake.  Akafanya hivyo.

“Nakushukuru sana mdogo wangu.”  Benito alishukuru wakati akiirudisha simu kwa Lydia.

“Wala usijali.”

“Lakini hujanipa namba yako.”

“Hujaniomba.”

“Haya basi naomba jamani.”

“Nipe wewe yako.”

Benito akaitoa namba yake kwa Lydia.  Alipoiomba ya Lydia akajibiwa angepewa siku nyingine.  Wakabishana kidogo.  Benito akaona hana haja ya kulazimisha.  Muhimu kwake ni namba ya Maulid ambayo tayari ameipata.  Basi nalo likawa linakamata lami kisawasawa.  Baada ya masaa mawili wakawa ndani ya jiji la Dar es Salaam.  Walishuka na kutoka pamoja hadi nje ya geti.  Walipotoka tu, Benito akamwambia Lydia.  “Unaonaje tukinywa soda kidogo hapo kontena?”

“Ahsante sana James.  Tutapanga siku nyingine.”

“Hapana Lydia, kwanini iwe siku nyingine na siyo leo?”

“Muda hauruhusu.  Nahitaji kufika nyumbani mapema.  Nitakutafuta wikendi ijayo.  Ama hutokuwa na nafasi?”

“Nitakuwa nayo.  Lini hasa?”

“Jumamosi.  Wewe jiandae then mimi nitakupigia kukwambia tuonane saa ngapi.”

“Kweli?”

“Kama huniamini shauri lako.”

“Basi naomba namba yako ili ukidelay nikupigie.”

You don’t need to have it.  Mimi sina ahadi za Kiswahili.”

“Haya bibie.  Nashukuru sana kwa kampani yako.  Nimeinjoi sana safari maana imekuwa fupi.”

The same to me.  Bye!”  Lydia akaaga kwa kupunga mkono na kuelekea kituo cha daladala za Tabata.

Benito akachukua teksi iliyompeleka moja kwa moja nyumbani kwake.  Kichwa chake kilikuwa kimeelemewa na mambo mengi.  Alianza kutathimini mambo yote aliyokutana nayo tangia awasili Iringa.  Kupata namba halisi ya simu ya Maulid ilikuwa ni habari njema sana kwake.  Hasira nyingi zilikuwa juu ya Maulid kutokana na kumdanganya kwake.  Nafsi ikamtuma kulipa kisasi kwanza kwa Maulid.  Lakini atalipaje?  Ndilo lililomtatiza zaidi.

Siku iliyofuata, Jumamosi, Benito alikwenda kazini.  Akakutana na wenzake na kutoa ripoti ya kazi waliyokuwa wamekwenda kuifanya.  Hakuna jambo lolote kuhusiana na safari yake ya Iringa alilothubutu kuwasimulia wenzake.  Hali iliyowapa kitendawili kisicho na majibu Nassoro na Thomas.  Walijua fika maelezo anayowapa ni uwongo.

Ofisini kwao walifanya kazi na msichana aitwaye Joyce.  Alifanya kazi kama katibu muhtasi.  Walikuwa na mahusiano mazuri sana.  Benito akamfikira kama mtu anayeweza kumsaidia jambo fulani kutokana na ushapu wake.  Akamfuata hadi ofisini kwake alikokuwa akiendelea na kazi zake kwenye kompyuta.

“Niaje Joy?”

“Mwanaume mbaya sana wewe!  Umerudi safari kimya kimya.  Hata umeshindwa kuniarifu nije kukupokea Ubungo?  Una roho mbaya wewe.”

“Siyo hivyo Joy.”

‘Siyo hivyo nini?  Tukiwa pamoja unajifanya unanipenda sana kumbe ukiwa mbali kisichokuwepo machoni.”

“Usinifikirie hivyo swahiba wangu.”

“Unataka kuniambia nini?  Tena nasikia umepitia hadi Iringa.”

“Mama yangu!”  Mshangao wa Benito ulikuwa mkubwa sana.  Hakutarajia habari za kupitia kwake Iringa zingefika ofisini.  Alikubaliana na wenzake iwe ni baina yao.   Siri si ya wawili, aliamini.

“Unashituka kitu gani?  Ama hukutaka nijue?  Utajiju mwanaume wewe usiyenijali.  Hebu niambie umepata nini cha zaidi huko kama si kufuja per diem zako?”

“Mimi nakujali sana mpenzi wangu.  Na mwaka huu lazima nimpindue jamaa yako nitangaze ndoa.”  Joyce akaangua kicheko.  Benito akaendelea.  “Enhee, hebu nidadavulie umbeya.  Nani kakwambia mie nilipitia Iringa?”

“Hao hao uliowaaga.”

“Kudadeki!  Wanaume wambeya wale!  Wamebakiza tu kuvalishwa kanga.”

“Tabia chafu hiyo kijana.  Juu ya nini kuwatusi wenzako?”

“Achana nao.  Kuna ishu nataka unisaidie.”

“Na wewe nawe!  Ishu gani tena hiyo wakati umeshindwa kunibebea japo mkungu mmoja wa ndizi?”

Benito akatulia kidogo.  Akaipa nafasi akili yake kuamua kama ni uamuzi sahihi kumshirikisha Joyce ama laa.  Moyo wake ukaridhia.

“Kuna dogo mmoja nataka umpigie simu.”

“Demu nini?”

“Tulia bibie.  Ni mvulana.  Tuseme kavulana ka shule.  Anaitwa Maulid, anasoma form five Kamene high school huko Tabata.  Sasa wewe jifanye Lydia.”

“Nd’o nani huyo?”

“Huyo Lydia wanasoma pamoja.  Umwambie unataka kuonana naye.  Zungumza naye kirafiki kama watu waliozoweana sana.  Panga naye appointment mkutane Lucky pub ipo Tabata Mawenzi.  Unanielewa?”

Joyce akatulia kwa nukta nyingi kiasi.  Akatafakari.  “Unadhani nitaweza?”

“Kwa nini ushindwe?  Nakuaminia hutoniangusha.  La muhimu ni kutumia lugha ile wanayotumia marafiki wa karibu zaidi.”

“We’ huyo Maulid unamtakia nini?”

“Namdai halafu ananikwepa.”

“Kwa hiyo unataka kumdunda?”

No!  Nataka tu niongee naye machache.”

“Usijemdhuru mtoto wa watu.  Maana nawe saa zingine unakuwa pwimpwi kweli.”

“Wala.  Ifanye kazi hiyo leo.”

“Leo haitowezekana.  Leo hatutotoka ofisini mapema.  Kuna kikao na bosi akitoka safari.  Amekwenda Zanzibar mara moja.  Anatarajiwa kuwa hapa saa tisa alasiri.”

“Poa.  Basi iwe kesho.”

“Basi sitompigia simu kwanza.  Nitamwandikia meseji kwa namba nyingine ninayoitumia kwa mambo kama haya.  Akiona namba geni najua tu atapiga simu.  Nitamlainisha kwa maneno we’ acha tu.”

“Yap, hayo ndiyo maneno!  Utanipa feedback kwa meseji.”

“Nyoo!  Nani atume meseji?  Nitakubipu wewe unipigie.”

“Usikonde.”

Ndivyo ilivyokuwa.  Siku ya pili asubuhi Benito aliwasiliana na Joyce kwa simu na kuambiwa Maulid amekubali mwaliko huo.  Benito akajawa na furaha isiyopimika.  Hatimaye anakwenda kumpata mbaya wake mwingine.  Akaisubiri kwa hamu hiyo jioni.

Akampigia simu kijana mmoja aliyekuwa amefanya naye mpango.  Kijana huyo, Aziz alikuwa akijulikana sana Sinza kwa vitendo vyake viovu na ubabe ubabe.  Mara nyingi alikuwa akikodiwa na watu kwa ajili ya kuwashikisha adabu wabaya wao.  Aziz alikubaliana na Benito wangekutana hukohuko Tabata majira ya saa kumi kamili.

Wakati Maulid anaingia pale wao tayari walikuwa wamekwishaketi.  Benito alikuwa amevalia kofia ya pama na miwani myeusi ya jua.  Kama ungekutana naye usingeweza kumtambua mara moja.  Maulid alipopepesa macho yake pande zote za pub hiyo hakumtambua Benito.  Wao waliendelea kunywa soda zao huku wakimtazama Maulid kila analofanya.  Wakati anamwagiza mhudumu kumnunulia vocha waliona.  Wakatulia kwani mtego wao ulikuwa umetegwa vema.  Wakati anapiga simu kwa Lydia siyo tu waliona, bali pia waliweza kusikia maneno ya Maulid.  Wakapata hakika juu ya mshangao na kuchanganyikiwa kwa Maulid.  Ndilo walilolitaka.  Kutokana na uzoefu wake wa mambo kama hayo, Aziz alikuwa amemwambia Benito kama itatokea hali kama hiyo itawawia rahisi wao kumnasa.  Alimwambia binadamu anapokuwa na hofu tele kuhusiana na jambo asilolielewa sawasawa hupoteza uwezo wake wa kufanya maamuzi ya haraka yaliyo chanya.

Benito akamwambia Aziz ale naye sahani moja wakati Maulid anainuka kutaka kutoka pale.  Benito akatoka hadi nje na kuliendesha gari  la Aziz hadi karibu kabisa na geti la kutokea mahali hapo.  Aziz akawa anatembea sambamba na Maulid katika hali ya tahadhali ili kutomgutua.  Maulid wala hakuhisi chochote.  Alipokuwa anatoka tu mlangoni hapo, akasikia sauti ikimsemesha.

Sorry bro.  Gari yangu imenisumbua kidogo, tafadhali nisaidie kidogo.”

Maulid akageuka nyuma na kumtazama mtu huyo.  Hakuwa akimfahamu kabisa.  Lakini ubongo wake ni kama vile ulikufa ganzi.  Hakuweza kufikiri kwa makini.  Hofu aliyokuwa nayo ilimharibia kabisa uwezo wa kufikiri.  Akadhania amsaidie huyu mtu ili pengine awe msaada kwake kwa jambo ambalo hata hakulijua.

“Poa.  Lipo wapi?”

“Hilo hapo.”  Aziz akajibu huku akionesha gari aina ya Toyota Corola lililokuwa na rangi nyeusi na vioo vyeusi.

Walipolifikia, Aziz akalifungua boneti la gari.  Akaangalia na kugusagusa vitu mle ndani.  Kisha akamgeukia Maulid.

“Tafadhali nichukulie toolbox hapo siti ya nyuma.”

Maulid hakufikiri.  Akaufungua mlango wa nyuma.  Kabla hajafanya lolote baada ya kuufungua mlango huo, akasukumiwa ndani ya gari.  Kisha gari ikaondolewa taratibu.  Hakuna mtu aliyekuwa amekiona kitendo hicho.  Gari haikwenda mbali sana.  Ikasimamishwa pembeni ya barabara.  Giza lilikuwa linaanza kuingia.  Benito akavua kofia na miwani.  Maulid alipomtambua tu, machozi yakamdondoka.

“Benito?”

“Unasemaje Maulid maarifa?”

“Kwa nini unanifanyia hivi bro?

“Mimi ndiye niliyepaswa kukuuliza kwa nini ulinifanyia vile ulivyofanya.”

“Nimekufanyia nini mimi?”

“Umesahau?  Ngoja nikukumbushe kidogo.  Mara ya kwanza nilipokuja shuleni nikimuulizia Hafsa ulinidanganya.  Hafsa alikuwepo shuleni.  Nadhani ni yeye aliyekufundisha unidanganye.”

“Siyo hivyo bro.”  Maulid alisema huku akilia.

“Subiri niendelee.  Kama haitoshi, nilipokuwa nikiondoka ukanifukuzia hadi kwenye kona ili uthibitishe kuondoka kwangu.  Nilikuomba namba ya simu ukadai huna simu.  Mungu hamfichi mnafiki.  Simu yako ikaita mbele yangu.  Ukaendelea kunidanganya siyo yako.”

“Nilikulazimisha unipe namba yako ya simu.  Bila aibu ukanipa namba isiyotumika.  Bado ukanidanganya hukuonana na Hafsa kabla ya kuondoka kwake.”

“Kweli bro.  Unanituhumu bure.”

“Usiendele kudhani una akili nyingi sana bwana mdogo.  Wewe ndiye uliyebaki nyumbani kwa Hafsa.  Sasa iweje aondoke bila kuonana nawe?”

“Ngoja nikwambie bro.

“Uniambie nini?  Huna jipya bwana mdogo.  Nilidhani tungekuwa marafiki wazuri.  Nasikitika kwa hatua hii tuliyoifikia. Lakini nalazimika kukufundisha adabu.”

“Nakuomba unisamehe bro.”  Maulid hakuwa na ujanja tena.  Machozi tele yalikuwa yakimtoka.  Alitetemeka mwili wote.  Katika maisha yake yote hakuwahi kukutana na msambwe kama huu.  Hakuwa na jinsi kwani hata kujinasua mikononi mwa Aziz isingewezekana kutokana na nguvu ya misuli iliyomshikilia.

“Hujui Maulid moyo wangu ukoje.  Hujui ukubwa wa hasira zangu juu ya dada yako na mumewe.  Na sasa juu yako.  Hujui kitu bwana mdogo hata kama unafahamu.”

Maulid hakuwa akimsikiliza tena Benito.  Akawa anajaribu kujiokoa mikononi mwa Aziz.  Akajikuta akimtemea mate usoni.  Akapigwa ngumi nzito juu kidogo ya jicho lake la kulia.  Kisha Maulid, kutokana na maumivu, akapayuka. “Nipigeni tu.  Masahafu ya Mtume, nakuapia Benito, piga ua galagaza nitalipa kisasi juu yako firauni wewe.”

Maulid akaporomosha mvua ya matusi ya nguoni.

Benito akawa anacheka sana.  “Nakusifu kwa ujasiri wako bwana mdogo.  Lakini kwa bahati mbaya, muda siyo wako tena.  Aziz, it’s a time.”

Lakini kabla Aziz hajafanya chochote, Maulid akaziminya korodani zake kwa nguvu.  Aziz akalia kwa hasira sana.  Kilichofuatia kilikuwa kipigo  kikubwa sana kwa Maulid.  Benito hakubaki nyuma.  Uso wa Maulid ukawa hautamaniki tena kutokana na damu iliyomtapakaa.

Walipoona Maulid hawezi hata kulia tena, wakapatwa hofu.  Benito akaliendesha gari hadi mbele kidogo palipokuwa na mtaro.  Wakaegesha gari.  Kisha kwa hadhari kubwa ili watu wasiwashitukie, wakamsukuma Maulid aliyekuwa hajitambui kabisa.  Wakaondoka taratibu kama vile hakuna jambo lilitokea.  Hata hivyo Benito akapoteza amani moyoni mwake.  Lakini akajipa moyo kuwa ameshinda kisasi

Akarudi nyumbani kwake.

…………..itaendelea

Na Fadhy Mtanga

Mtanga ni mtunzi wa kitabu cha riwaya, HUBA anayepatikana Dar es Salaam. Unaweza mfatilia katika mtandao wa Twitter kupitia: @FadhyMtanga na kupata kitabu chako cha HUBA kwa namba: +255 (0)715 599 646

 

Leave a Comment