Riwaya ya Kizungumkuti: Sura ya 11

Kizungumkuti

Iringa

 Jumapili, Juni 8, 2003

 

 

“Mwaaah!”

“Nakupenda sana Ali”

“Nakupenda sana Hafsa.”

“Najisikia raha sana kuwa nawe hapa.  Unajua Ali nilikumiss vibaya mno.”

“Nami nilikumiss pia honey.

“Nimeufurahia sana usiku uliopita.”

“Mmh, kweli eeh?”

“Kweli Ali.  Huamini?  Nimekumbuka mambo mengi sana.”

“Yapi hayo?”

“Basi tu.  Nimekumbuka namna ambavyo huwa nakufurahia.”

“Kweli eeh?”

“Ungejua hata usingesema.  Nilikuwa nimekutamani Ali wangu vibaya mno.  Ningepata uchizi.”

“Sasa hamu imekuisha?”

“Toka huko!  Iniishe wapi?  Hamu juu yako huwa inaniisha?  Sema tu huwa unaniridhisha.  Lakini pamoja na hayo bado siishi kukutamani.”

“Usikonde.  Mimi ni wako daima.”

“Kweli eeh?”

“Ama huamini?”

“Hapana sweetie.  Naamini sana.  Isingekuwa hivyo sidhani kama tungekuwa hapa.  Najisikia raha maishani kwa kuwa unanipenda, wanijali na kunithamini pia.”

“Ahsante sana kwa hilo.”

“Nibusu basi honey.

“Hata bila kusema.  Sogea basi.”  Ali akawa anazungumza huku akimvuta Hafsa taratibu kumsogeza kwake.

Wakakumbatiana.  Ali akausogeza mdomo wake kwa Hafsa na kumbusu huku mikono yake ikiendelea kujivinjari mwilini.

Kila mmoja akisisimka tena.

Walipoamka toka kitandani ilikuwa yapata saa nne asubuhi.  Wakaingia maliwatoni.  Walipokamilisha kujiandaa, wakaelekea kupata kifungua kinywa.  Mtu na mkewe, mtu na mumewe.  Kila mmoja akiwa mwenye furaha tele na angalau kusahau kashkashi za moyo kwa siku kadhaa mfululizo.

“Tunakwenda Iringa Club.  Ndipo tutakapokunywa supu.  Ama siyo honey?

“Wewe ndiwe wangu mamaa.  Chochote usemacho hewala!”

Wakachukua teksi ilyowapeleka hadi Iringa Club ambayo ipo karibu na Chuo cha Benki cha Dr Amon J Nsekela, barabara ya Uhuru.  Mtu yeyote asiyewafahamu asingepata taabu kumaizi kuwa wanapendana kwa dhati.  Nyuso zao zilibeba ujumbe kuwa wanaifurahia ndoa yao kwa kiasi kikubwa sana.  Kwa Hafsa, furaha ya kuwa na Ali ilikuwa haimithiliki.

Baada ya mambo kadha wa kadha kuwa yamemtokea akiwa peke yake Iringa, alijiona yupo salama mikononi mwa Ali.  Kwa mantiki hiyo, akaamua kutomsimulia Ali juu ya kupigiwa simu na Benito, kuchezwa shere  na Johari na hatimaye kutorokwa na Johari nyumbani kwao.  Ali alipotaka kufahamu kama kuna lolote linalomsumbua, alidai hakuna.

Mara zote afikapo Iringa, Ali hupenda kulala hotelini.  Hivyo Hafsa alikuwa ameungana naye.  Baada ya stafutahi yao ya nguvu ndipo wakaenda  Mwembetogwa, nyumbani kwa akina Hafsa.  Huko wakapata chakula cha mchana.

Wakaondoka kwa matembezi kidogo.  Wakaenda katika mkahawa wa mhadalishi Cyber Cafe uliopo kwenye jengo la Bottom’s Up makutano ya mitaa ya Jamatikhan na Msikitini huko Miyomboni.  Huko wakafanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kupiga gumzo na marafiki wao wa kwenye mtandao.

Majira ya saa kumi na mbili jioni, wakaamua kwenda Luxury Bar, barabara ya Mkwawa mkabala na jengo la CCM mkoa.  Wakaagiza mchemsho wa mkia wa ng’ombe na vinywaji.  Watu hawakuwa wengi sana tofauti na siku zingine za mwisho wa wiki.

Pembeni ya meza waliyoketi wao kulikuwa na watu wawili.  Mmoja alikuwa ni baba wa makamo mwenye umbo lililoshiba.  Huyu aliketi upande uliomwezesha kuwaona akina Hafsa moja kwa moja.  Mwingine alikuwa ni binti mwenye umbo la kisichana hasa.  Alikuwa amesokota nywele katika mtindo wa Kimasai.  Huyu aliwapa mgongo.

Muda wote tangu Ali na Hafsa waingie, yule mzee alikuwa akijitahidi kumwongelesha mtu wake lakini hakuonekana kuwa pale kimawazo.  Kila muda alikuwa akijaribu kupiga jicho la wizi upande waliokuwapo wao.  Wao hawakubaini kuna mtu anayewatazama kwa kuwavizia.  Walizama kwenye maongezi yao.

Binti huyo alikuwa amewatambua tangu kuingia kwao.  Furaha ya mahali hapo ikamtoka kabisa.  Hofu yake ikawa endapo watamtambua.  Masikini ya Mungu, wao wala hawakua na wazo na mtu mwingine ndani ya baa hiyo zaidi ya kujali maongezi yao na vitu vilivyokuwa mezani pao.

Kuna muda yule mzee akainuka kuelekea msalani akimwacha binti huyo peke yake.

Alipogeuka tena kuwatazama, kwa bahati mbaya macho yake yakagongana na Ali.  Alikuwa ni Johari.  Ali akamkazia macho akiwa haamini kwa sababu hakuwa amemwona kwa muda mrefu kiasi.  Sura yake haikuwa imebadilika.  Kwa kuonesha hakuwa akiyaamini macho yake, akamwuliza mkewe.

“Eti sweetie, siyo Johari yule?”

Hapo ndipo Hafsa akazingatia kumtazama kwa makini mtu huyo.  Hakuhitaji kurudia tena.  Akamtambua.  Akashituka huku akionesha hali ya wasiwasi.

“Hata kama ndiye, wewe wa nini?”

“Siyo vizuri hivyo Hafsa.  Mtu tunafahamiana naye halafu tumkaushie?”

“Kufahamiana naye kitu gani?  Wewe achana naye bwana.”

Ali akastaajabishwa na mkewe.  Lakini hakujua kilichojiri, akaendelea kumshawishi.  “Acha hizo mke wangu.  Kwa nini lakini?”

“Basi tu.  Sipendi kukutana naye.  That’s all.  Nielewe kwa hilo.”

“Jamani Hafsa, yale mambo si yalikwisha miaka mingi hata mkaelewana tena.  Kwa nini lakini?”

Hafsa akazidi kugadhabika.  Ali akaamua kuacha kubishana naye.  Hali ya Hafsa ikabadilika haraka.  Akaonesha dhahiri hasira machoni pake.  Ali alichanganyikiwa.  Haya yametoka wapi?  Kumwona tu ndiyo akasirike hivi?  Maswali yakawa yanamjia Ali kichwani mwake.  Hafsa akaacha hata kula.  Macho yake yote akayakaza kwa Johari.  Mikono yake ilimtetemeka kiasi cha kumwogfya Ali.  Akaanza kuuma mdomo wake wa chini kwa meno ya juu.  Siku zote hiyo ni dalili ya kiwango cha juu ya kughafirika kwa Hafsa.  Jambo hilo likamvuta Ali uangalifu mkubwa.

“Hafsa?”

“Hafsa.”

Hafsa hakujibu kitu.  Aliendelea kumkazia jicho Johari huku akionesha kufikiri jambo kwa makini.  Yule mzee aliyekuwa na Johari akarudi kutoka msalani.  Akaungana na Johari.  Johari akainua tena macho yake.  Yakagongana na ya Hafsa.  Akayakimbiza haraka.

Bila ajizi Hafsa akaropoka.  “We’ fala!”

“Ayaaaah!  Hafsa nd’o nini tena?”  Katika maisha yake Ali hakuwahi kumsikia Hafsa akitoa neno la kumtusi mtu.  Ikampa soni nyingi.  Akamshika mkono kama ishara ya kumsihi kuzuia hamaki iliyokuwa imemjilia kwa nguvu.

“Niache Ali.  Huyu mwanaharamu hanijui mimi.”

No Hafsa!  Kama umeghafirika wacha tuondoke zetu.”

Johari alipomsikia Hafsa akimtukana hakujibu.  Alitulia tuli kama siye anayeelekezewa tusi.  Akajifanya ametingwa kimaongezi na mtu aliyekuwa naye.  Alijitahidi kadri ya uwezo wake kujipoteza.  Lakini hata hivyo amani ilikuwa imempotea zaidi moyoni mwake.  Alikuwa akiomba Mungu Ali afanikiwe kumwondoa Hafsa hapo ili iwe salama yake.

Hafsa alikuwa amebadilika sana.  Aliendelea kuuma mdomo wake kwa nguvu.  Akauondoa kwa nguvu mkono wa Ali uliokuwa umemshika.  Akainuka haraka kitini akielekea ile meza aliyokuwapo Johari.  Kitendo hicho kilifanyika haraka sana kiasi kwamba Ali alipoipoteza sekunde moja kumzuia mkewe, akawa ameshindwa kabisa.  Hafsa alipofika mezani kwa Johari.  Akaiweka mikono yake kiunoni pake.  Macho yake yote yakamkazia Johari.  Johari akatahayari na hofu tele kumjaa.  Akanyong’onyea mithili ya panya aliyebanwa vema na mtego.  Hafsa hakujisumbua kutoa salamu.

“Hivi wewe Johari, ulivyonifanyia umepata faida gani?”

Wakati Johari akiendelea kumwemwesa mdomo wake pasi kujua ajibu nini, tayari Ali akawa amemfikia Hafsa.  Mkono wake wa kuume ukawa begani mwa mkewe.  Yule mzee aliyekuwa na Johari, alipoona Johari hajibu kitu, akaitumia fursa hiyo kumvaa Hafsa.

“Binti, mbona unakosa ustaarabu?  Ama kwenu hakuna wakubwa?”

Hakujua amechokoza mzinga wa nyuki.  Hafsa akamtazama huyo mzee kwa jicho la dharau kali.  Akajipa uhuru wa kuzungumza kadiri kichwa chake kilivyomtuma.  “Wakubwa kitu gani?  Huna hata haya.  Ungekuwa mtu mzima wewe ungeiacha familia yako na kuja kuhangaishana na malaya huyu?”

Alipoisikia kauli hiyo, Johari akatokwa na machozi.  Ali na yule mzee wakapigwa na butwaa. Johari akaongea kwa uchungu.  “Hafsa?  Kweli rafiki yangu umefikia hatua ya kuniita mimi hivyo?  Kweli Hafsa?  Mimi malaya?”

“Kwa hiyo unataka kusemaje?”  Yule mzee akaongea huku akiinuka.

“Usinitishe mimi mzee mzima usiye na haya.  Unataka kunipiga ama unataka kupigana na mimi mwanaizaya mkubwa wewe?”

Johari akamshika yule mzee mkono na kumvuta aketi.  Akaketi ilhali jasho likimtoka kwa kasi na kuhema kwa nguvu.

Johari akamsihi kwa sauti ya taratibu. “Tulia dear.  Usipandwe na jazba.  Huyu ni rafiki yangu.  Mambo yaliyotokea tutayamaliza wenyewe.”  Kisha akamgeukia Hafsa aliyekuwa amepandwa na ghadhabu kubwa.

“Naomba unisikilize Hafsa.  Najua umeumia.  Nisamehe kwa hilo.  Lakini ungeniuliza kwanza ilikuwaje?”

“Kama uliona kuna umuhimu wa kuniambia kwa nini ulinitoroka?”  Hafsa alimtupia Johari swali lililowafanya Ali na yule mzee kuendelea kuwa kimya.

Johari akayafuta machozi yake kwa leso kabla hajamjibu Hafsa.  “Sikukutoroka Hafsa.  Huwezi jua ni kwanini nilifanya vile.”

“Nafahamu sababu.  Usidhani kumbukumbu yangu haifanyi kazi Johari.”

“Hapana.  Hapana Hafsa.  Achana na mambo ya zamani.”

“Hunielezi kitu mbwa wewe.”

“Sawa dada.  Vyovyote utakavyojisikia kuniita ni halali yako.  Pengine ningekuwa mimi ningefanya zaidi ya hapo”

Ali akashindwa kuvumilia.  Akamlazimu kuaga.

“Johari, sifahamu kinachoendelea.  Wacha sisi twende.  Nadhani mtatafuta siku mzungumze yaishe ili…..”  Hafsa akamkatisha.

“Azungumze na nani baradhuli huyu?  Sihitaji kuzungumza na mtu mnafiki kama huyu.  Kuna kitu anakitafuta kwangu.  Atakipata muda si mrefu hadi atamani ardhi ipasuke immeze.  Twende zetu mume wangu.”  Akageuka haraka akiwa amemshika mumewe mkono.  Ali hakupendelea kuondoka katika hali hiyo.  Fedheha na kuchanganyikiwa vyote vilimtawala yeye.  Hakuna aliyeongea na mwenzake hadi wanafika hotelini.

Walipoingia chumbani Ali akamtaka Hafsa waende maliwatoni kuoga.

“Wewe nenda tu.  Mi’ ntaoga baadaye.”

“Umeianza lini hiyo ratiba?”

“We’ nenda kaoge.”  Sauti ya hafsa alionesha bado yungali na hasira.  Ali hakupendezwa na hilo.

“Hafsa, kumbuka mimi siyo Johari.  Sitegemei kuwa unataka kuzihamishia kwangu hasira zako dhidi yake.  Tafadhali mpenzi.”

Anyway,  nimekuelewa.  Twende.”

Walipoingia bafuni, hali haikuwa kama siku zote waogapo wawili hao.  Hafsa alionekana kuwa mbali sana kimawazo.  Ali hakumwuliza kitu akiusubiria muda alioupanga kwa kazi hiyo ili kujua kisa cha sekeseke lake na Johari.  Walipomaliza kuoga, Ali alimwomba waende ukumbini wakapate vinywaji kidogo.  Hafsa akakataa kwa kudai amechoka sana.  Ali hakumlazimisha.  Akamsubiri walipopanda kitandani.

“Hafsa!”

“Mmh!  Sema.”

“Hebu niambie mpenzi wangu, kwanini imetokea vile kati yako na Johari?”

“Mpuuzi sana mwanamke yule.”

“Wewe nieleze.”

“Yatakusaidia nini mambo yake ya kishenzi?”

“Kumbuka kumtukana mtu hakuleti maana kama mwenyewe hawezi kukusikia.  Labda kama umekusudia kunitukana mimi indirectly.

“Mh!  Huko unakokwenda wala sipo kabisa mume wangu.”

“Ila?”

“Sikiliza Ali, sipendi kuyakumbuka mambo yasiyo na maana.”

“Tusibishane sana Hafsa.  Kama unaona sistahili kufahamu, tafadhali usiniambie.  Tuyaache hayo na kuzungumza mambo mengine.”  Ni wazi Ali alikasirika.

“Ah jamani honey,  sasa ndiyo umekasirika?”

“Sina haja ya kukasirika wakati unao uamuzi wako juu ya mambo yasiyonihusu.”

“Haya babaa, nisamehe kama umekwazika.  Wacha nikusimulie.  Ilikuwa hivi…”

Hafsa akaanza kumsimulia Ali kuanzia alipopigiwa simu na Benito.  Akamsimulia hata alipopigiwa simu na Johari kisha yeye kwenda na kuwakuta wakiwa pamoja.  Pia hakuliacha tukio la Johari nyumbani kwao.  Ali alisikiliza kwa makini sana.  Alijilaza kitandani huku akimtazama mkewe aliyekuwa ameegamia ukutani.  Miguu yao ilikuwa imepishana usawa wa mapajani.

Alipomaliza kusimulia, Ali naye akainuka na kuegamia ukutani ili kujipa nafasi ya kuzungumza.

“Umesema Benito alikupigia simu lini?”

“Jumatano jioni.”

“Na Johari?”

“Alhamisi asubuhi nikiwa kazini.  Akaniambia tukutane pale stendi.”

“Kwa nini hukutaka kuniambia?”

“Jumatano nilikuwa nimechanganyikiwa sana.”

“Na Alhamisi je?”

“Hapo usitake kunilaumu Ali.  Alhamisi nilikutafuta sana kwenye simu hukupatikana.”

“Na nilipokupigia kwa nini usiniambie?”

“Nilikuwa na sababu mbili.  Kwanza kwa kuwa nilikumiss sana sikutaka kukwambia mambo ya kukukosesha raha mpenzi wangu.  La pili, ambalo ni la msingi sana, ulinidanganya.”

Ali akashtuka.  Hakusema kitu akimwacha mkewe kuendelea.

“Ninavyoamini mimi, si kweli simu yako iliishiwa chaji.  Nahisi uliizima kwa sababu unazozijua mwenyewe.”

“Jamani mke wangu.  Sababu ndiyo hiyo hiyo simu iliisha chaji ghafla.”

“Ali, labda nikuulize swali.”  Ali akaitikia kwa kichwa.  “Unaweza kunitajia jina la kibanda cha simu ulipoichajia simu yako?”

Kigugumizi kikamvaa Ali.  Hakuwahi kufikiria kuulizwa swali hilo.  Hakuwa amejisumbua kuandaa majibu.  Akababaika kabla ya kujibu.  “Ni pale kwenye kona karibu na round-about ya Uhuru na Msimbazi.

“Panaitwaje?  Nataka unitajie jina lake.”

“Mh!  Silikumbuki vizuri jina.”

“Ok Ali.  Umeanza kunidanganya siku hizi.”

“Usinifikirie hivyo mke wangu.”

“Ngoja nikukumbushe jambo moja kijana.  Hilo eneo lote la round-about hakuna mahali penye kibanda cha simu.  Sasa ili nisikufikirie vibaya.  Nijibu maswali yangu.”

“Niulize tu.”  Ali alikuwa amebanwa vema katika muda huo.

“Dukani kwako umeacha kuuza simu siku hizi?”

“Kwa nini umeuliza hivyo?”

“Nijibu swali langu.”

“Sijaacha.  Bado nauza.”

“Hizo simu unazoziuza siku hizi unaziuza bila chaja zake?”

Ali akapatwa na aibu.  Akajaribu kutazama pembeni ili macho yake yasikutane na ya mkewe.  Hafsa akatulia kimya ili kumpa mumewe wasaa wa kujihukumu kwa uwongo wake.  Ali alipomtazama Hafsa, alimwona akitabasamu kwa mbali.

“Sikiliza Hafsa, niligundua simu yangu haina chaji nikiwa mtaa mwingine mbali na dukani.  Nikasahau suala la kuwa na chaja dukani.  Nilipopaona pale nikaenda kuweka na simu yangu.  Usinielewe vibaya mke wangu.”

“Ali?”

“Naam!”

“Umefanya kosa la kwanza kunidanganya.  Kama haitoshi, ili kuiridhisha nafsi yako, bado unaendelea kunidanganya.  Umeshaanza kunichoka eeh?”

“Hapana Hafsa.  Ukisema hivyo utanifanya nijisikie vibaya sana.”

“Ungejisikia vibaya kule ulikokuwa ukinidanganya mbona ingekuwa afadhali sana.”

“Siyo hivyo….”  Ali akakatishwa na mkewe.

“Nisikilize.  Sihitaji kufahamu sababu ya wewe kuzima simu.  Pia sitaki kufahamu ni wapi ulipokuwa.  Ninachokutaka wewe kufanya ni kuniomba msamaha kwa kunidanganya.”

“Sijakudanganya honey.

“Ali, unapaswa kumshukuru Mungu unaongea na mimi nikiwa sina hasira.  Tafadhali niombe msamaha.”

“Lakini Hafsa…..”

“Lakini nini?  Kama hutaki kuniomba msamaha, niambie wazi kuwa hutaki.”

Ali badala ya kujibu akafikiri kwa nukta kadhaa.  Hakujua kama aendelee kukataa ama aombe msamaha kama mke wake anavyomtaka kufanya.  Hafsa kwa upande wake akaanza kuufurahia ushindi moyoni mwake.  Akamtazama Ali, kisha akamsemesha.

“Ali, unaniomba msamaha ama la?”

“Ok, ngoja nikubali tu yaishe.”

“Siyo suala la kukubali ili tu yaishe.  Nimekutaka uniombe msamaha?”

“Haya mama.  Nakuomba unisamehe.”

“Kwa kosa gani?”

“Kukudanganya.”

“Inatosha.  Sitaki tuyajadili haya mambo tena.  Lakini ngoja nikwambie kitu kimoja mume wangu.  Take care.

“Sawa nimekusikia.”

Hafsa akawa amerejea kwenye hali yake ya kawaida.  Ila akilini mwake alikuwa amepata jawabu moja kati ya maswali mengi sana yanayokitatiza kichwa chake.  Wakavuta shuka na blanketi wakiwa wamekumbatiana.  Kila mmoja akiyafurahia maisha na mwenzake kwenye baridi kali la Iringa.

Kiasi cha saa tano kasoro dakika kadhaa usiku huo simu ya Hafsa ikaanza kuita.  Wote wakaamua kuipuuzia.  Wakaendelea na mambo yao.  Iliita mara tatu.  Ilipokatika mara ya tatu, simu ya Ali nayo ikaanza kuita.  Ikaita hadi ikakata.  Ilipokuwa ikiita kwa mara ya pili, Ali akaamua kuifuata pale ilipokuwa.  Alipoitazama namba ya mpigaji, akakutana na jina la Zuhura, dada yake Maulid.

“Vipi shem, habari za usiku?”  Ali aliongea mara alipoipokea.

“Safi kiasi.  Vipi bado upo Iringa?”

“Ndiyo shem.”

“Upo na Hafsa?”

“Ndiyo.  Shem unanitisha, kwani kuna nini?”

“Maulid yupo hospitali.  Amepigwa sana hadi amepoteza fahamu.”

“Mungu wangu!  Pole sana shem.  Mimi nitakuja kesho mapema sana.  Yupo hospitali gani?”

“Muslim Hospital.  Huku huku Tabata.”

“Pole sana mama.  Usijali sana.  Kesho tutakuwa pamoja.”

“Ahsante sana shem.  Nisalimie Hafsa.”

“Usijali zimefika.”

Simu ikakatwa.  Hafsa usingizi wote ukamtoka.  Alikuwa ameyasikia maongezi yote baina ya Ali na Zuhura.

“Amepigwa na nani?”  Lilikuwa swali la kwanza kwa Ali simu ilipokatwa.

“Sikuona haja ya kumwuliza.  Amechanganyikiwa sana.”

“Masikini Maulid.  Sijui atakuwa ameumizwa kiasi gani!”

“Atakuwa ameumizwa sana hadi kupoteza fahamu?  Lakini Maulid siyo mgomvi.  Hata pombe hanywi.”

“Ali, nimehisi kitu.”

“Kitu gani hicho?”

Anyway, wewe kesho nenda.  Mimi nitakuja Jumanne ili kesho niage kazini na nyumbani.”

“Dah, itakuwa vizuri.  Zuhura atakuwa katika wakati mgumu sana.  Uje umpe kampani.  Halafu hujaniambia umehisi kitu gani?”

“Muda ukifika nitasema.”

“Hapana Hafsa.  Sema sasa.”

“Nahisi kuna mtu anahusika.”

“Nani huyo?”

“Benito.”

“Benito?”

“Yah!  Hakuna anayeweza fanya hivyo zaidi yake.”

“Naamini.”

…………..itaendelea

Na Fadhy Mtanga

Mtanga ni mtunzi wa kitabu cha riwaya, HUBA anayepatikana Dar es Salaam. Unaweza mfatilia katika mtandao wa Twitter kupitia: @FadhyMtanga na kupata kitabu chako cha HUBA kwa namba: +255 (0)715 599 646

Leave a Comment