Riwaya ya Kizungumkuti: Sura ya Tisa

KizungumkutiIringa

 Jumatano, Juni 4, 2003

 

Benito aliwasili mjini Iringa akiwa na matumaini tele.  Alipokuwa akipanga safari ya Iringa, alifanya mawasiliano na msichana mmoja, Johari.  Benito na Johari wana historia ndefu ya kufahamiana tangia wakisoma shule ya sekondari ya Mkwawa miaka kadhaa iliyopita.  Johari pia alifahamiana vilivyo na Hafsa kwa mtindo huo huo.

Johari baada ya kumaliza kidato cha sita alichukua stashahada ya uhasibu katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kampasi ya Dar es Salaam.  Kisha akaajiriwa na Halmashauri ya Manispaa kama mhasibu msaidizi.  Johari na Hafsa walikuwa na desturi ya kutembeleana sana wakati huo Hafsa akisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua shahada ya Sanaa na Elimu.

Benito alimtaarifu Johari juu ya kuhitaji msaada wake pindi afikapo Iringa.  Lakini akamsisitiza endapo atawasiliana na Hafsa asimtaarifu juu ya ujio wake.  Ingawa Johari alikuwa na uelewa wa kutosha juu ya mambo yaliyowahi kutokea, hakuwa na hisia zozote hasi kutokana na ujio wa Benito.  Johari hakuwa na haraka ya kutaka kujua nini kinaendelea kati ya Hafsa na Benito.  Aliamini angefahamu pindi watakapokutana.

Benito aliwasili Iringa kiasi cha saa tano asubuhi.  Alifahamu angekutana na Johari nyakati za jioni baada ya kutoka kwake kazini.  Hivyo muda wa mchana ulimfanya Benito kujipumzisha hasa kutokana na uchovu wa kazi mfululizo na safari.  La zaidi muhali ulikuwa umepungua sana kutokana na imani kuwa ndani ya Iringa mambo yote yakwenda sawa.

Hakuwa amepanga kuwasiliana na Hafsa hadi pale atakapokutana na Johari.  Alitegemea kumwomba msaada namna ya kukutana naye.  Lakini alifahamu ugumu wa kumshawishi Johari hasa kuhusiana na mambo fulani yaliyowahi  kutokea.  Kwake hakuona hilo ni tatizo sana.  Imani kubwa ilikuwa angemalizana na Hafsa kwa mazungumzo baada ya kukutana.  Kuwepo kwake Iringa kulimfariji na kuihakikishia nafsi yake ushindi mwepesi.  Ombi lake kubwa moyoni ni kupata nafasi ya kukutana naye.

Muda ulikwenda sana hata kufikia saa kumi na mbili jioni pasi kukutana na Johari.  Uvumilivu ukamshinda.  Tarajio lake lilikuwa kuonana na Hafsa mapema iwezekanavyo.  Hakuweza kuwa na subira zaidi.  Akaichukua simu yake.  Akaenda katika menyu ya mpangilio wa simu.  Akachagua mpangilio wa kufichwa kwa namba yake. Akaificha namba ili isionekane kwa anayepigiwa simu.   Kisha akampigia simu Hafsa.

Maongezi yake na Hafsa hayakuwa mazuri hata kidogo.  Mazungumzo hayo yalimchanganya zaidi Benito kutokana na majibu ya hasira aliyoyapata.  Hakutegemea ingekuwa hivyo.  Akauona sasa ugumu uliokuwa mbele yake.  Suluhisho lake likawa endapo Johari ataridhia mpango wake wa kuwakutanisha kwa hila.

Si punde akapata simu kutoka kwa Johari.  Akamtaarifu kuwa wakutane Hotel Aashiana iliyopo Akiba House kwa chakula cha jioni itakapotimu saa mbili za jioni hiyo.  Benito akachachawa kwa sababu anamfahamu Johari ni mtu wa matumizi.  Hivyo ni lazima atatoboa tu mifuko yake.  Hata hivyo hakujali sana.  Mfukoni alikuwa na kiasi cha kutosha cha pesa kutokana na posho kubwa aliyolipwa kwa safari mkoani Mbeya.

Saa mbili kasoro dakika ishirini hivi Benito akawa tayari barabarani akitembea mwendo wa wastani.  Hotel Aashiana ipo karibu kabisa na stendi kuu hivyo hakuona umuhimu wa kuchukua teksi.  Kwa kawaida ya Benito, hachelei kuwa nadhifu nyakati za mitoko kama hii.  Jioni hii alikuwa ndani ya suruali nyeusi ya kitambaa kizito kiasi  huku kiatu chake kikiwa kimeng’arishwa vizuri na mng’arisha viatu maarufu nje ya hoteli aliyofikia.  Alivalia shati la mikono mirefu la rangi nyeupe, akijikinga baridi kali ya Iringa kwa koti la ngozi lenye rangi ya kahawia. Iliyokolea.  Utanashati wake na mwendo wa wastani ulimfanya ang’are mithili ya mcheza filamu wa Kifaransa.

Saa mbili kasoro dakika kumi ilimkuta akipandisha ngazi za jengo hilo kuingia Aashiana.  Wakati akimsubiri Johari aliagiza soda aina ya Sprite.  Wakati huo alikuwa akiangaliaangalia mandhari ya hoteli hiyo maarufu mjini hapo kwa vyakula vya bara la Asia na Afrika.  Wageni wengi wa tamaduni tofauti hupapenda mahali hapo kutokana na ubora wa huduma zake.

Johari aliwasili dakika tano baada ya saa mbili kamili.  Benito alimwona wakati akimalizia kupandisha ngazi.  Akakwepesha macho kama hajamwona.  Uzuri wa Johari haukuwa umeng’arishwa na rangi yake tu, bali pia umbo la kimahaba alililojaaliwa.  Mrefu kiasi cha futi tano unusu.  Tumbo lake dogo likisindikizwa na nyonga pana.  Kidari chake  kilijaaliwa chuchu zenye kuuthibitisha ujana wake ingawa umri wake haukufanya ajizi kusonga mbele.  Suruali yake ya jinsi nyeusi ilimkaa vema na kulichora sawia umbo lake.  Vifungo vya koti lake jeusi la jinsi havikuwa vimefungwa.  Vikakipa nafasi kinguo cha juu cha pinki kuonesha vema umbo la kifua chake kilichokuwa kikitishia kukitoboa kinguo hicho.  Kichwani alisuka rasta maarufu za Kimasai na kuongeza uzuri wake.  Mvuto huo ulisindikizwa na viatu vya kambakamba vyenye rangi ya pinki kufanana na rangi ya kitopu chake.  Pochi yake, maarufu kama kipima joto ikiwa na rangi ya pinki pia.  Kama alikuwa amefahamu pengine, madhari ya ndani ya hoteli hiyo yalikuwa yametawaliwa na upinki zaidi.

Hadi Johari anawasili mezani pale, Benito alikuwa angali akimstaajabia urembo wake.  Akasimama na kumlaki.  Kila mmoja akaonesha kumfurahia mwenzake.  Mhudumu alipofika, wakaagiza vyakula na vinywaji.  Chakula hicho kilichukua dakika ishirini kuandaliwa na kuletwa mezani kwao.  Mlo wa Johari ulikuwa ni wali na samaki wa mchuzi.  Samaki hao watokao bwawa la Mtera mpakani mwa mkoa wa Iringa na Dodoma.  Benito yeye aliagiza ugali kwa samaki haohao isipokuwa wake alikuwa wa kukaangwa.  Wakati Johari akisindikiza mlo wake kwa bia ya kopo ya Heinneken, Benito ambaye si mnywaji wa pombe, alikuwa na soda ya Sprite.

“Niambie Ben, unatupa jongoo na mti wake!”

“Hapana Joha, ni maisha tu.”

Anyway, tuyaache hayo, najua I’m none of your interest…”

No Johari, unakwenda mbali.”

It’s ok!  Yetu tutazungumza siku nyingine.  Niambie mshikaji ushawahi kuonana naye hivi karibuni?”

“Nani?  Hafsa?”

“Sasa tunamzungumzia nani kama siye?”

“Sijawahi.”

“Sasa umejuwaje kama yupo Iringa?”

“Nilifahamu kupitia mshikaji wangu mmoja.”

“Mimi sijaonana naye pia.  Kwanza kwanini hujafanya utaratibu wa kumwambia kuwa unakuja Iringa?”

“Sikiliza Johari, wewe unafahamu fika undani wa yote.  Suala la kukutana na Hafsa siyo jepesi kivile.  Inahitaji umakini.  Nilifahamu kama ningemtafuta mimi angegoma.  Hii ndiyo sababu nahitaii wewe unisaidie kuonana naye.”

Come on!  Unadhani mimi nitakusaidiaje?”

“Kwako itakuwa rahisi.  Utampigia simu kwamba unahitaji kuonana naye.  Najua atakuja tu.  Mimi nitakuwepo mahali hapo.  Nadhani pia utanisaidia kuzungumza naye.”

Think twice Ben.  Siwezi kuwa chambo.  Nadhani unataka nami anichukie.”

“Hawezi kukuchukia from nowhere.  Tafadhali kuwa tayari kunisaidia.”

“Umesahau?  Hebu tufikie mahali Ben tukue.  Unasema hujawahi kukutana naye miaka yote.  Jaribu kufikiria jamani.”

“Achana na hayo.  Niambie upo tayari kunisaidia ama hupo tayari?”  Benito alijitahidi kuficha hasira.  Lakini Johari alielewa hasira imeshamvaa.

“Aah!  Tatizo lako Ben, you always only think of yourself.  Unachokitaka kiwe lazima kiwe.  Hapa badala ya kucompromise, unakasirika.  Hatuendi hivyo bwana.”  Johari akamtazama Benito, alipoona hasemi kitu, akaendelea.

“Najua tatizo lako.  Hafsa si ndiye umpendaye zaidi?  Haya sema unataka kukutana naye wapi nimlete?”

“Labda pale hotelini kwangu.”

No.  Nahitaji isiwe hotelini.  Tutakaa sehemu ya wazi yenye watu wengi.  Nakufahamu wewe.  Usije ukawa na dhamira za kumdhuru ukanipa nami matatizo.”

“Usifikirie kote huko.  Mimi sina nia naye mbaya.  Hata hivyo nakushukuru.”

Let me tell you one thing.  Sijakubali kwa moyo wangu kupenda.  Ni kwa shingo upande kwa sababu unang’ang’ania.  Lakini ukae ukijua moyo wangu haupo radhi kwa hilo.”

Potelea mbali!  Ndicho kilichomjia Benito akilini kwake.  Hakujali  kama jambo hilo litampendeza Johari ama la.  Alichojali ni kufanikiwa kwa dhamira yake.

“Lakini Ben, hebu jaribu kuwa mkweli.  Tatizo la binadamu, saa hizi utasema kwa unyenyekevu.  Lakini kesho utakapokuwa kama mbogo aliyejeruhiwa hutokumbuka ahadi uliyoitoa hapa.”

“Mbona sikuelewi sasa?”

“Nd’o nataka kukwambia, kama una nia naye mbaya, tafadhali kabisa usinihusishe kabisa.  Yaliyotokea kipindi kile yalinitosha.”

“Mimi sipo hivyo.”

“Unadhani nimekusahau Benito?”

“Ni zamani zile.  Kadri nyakati zibadilikavyo, watu pia hubadilika.”

“Si hadi uwe?”

Wakaendelea na maongezi ya kawaida hadi saa nne usiku.  Benito akarudi hotelini kwake baada ya kuwa amemsindikiza Johari nyumbani kwao Kihesa.  Makubaliano yake na Johari yalirejesha matumaini yaliyotoweka baada ya tukio la simu.

Akaawa anapanga maneno atakayoyatumia pindi atakapokutana na Hafsa.

Akajipa moyo itakuwa rahisi.

 

********************

 

Johari alipofika nyumbani alipitiliza hadi bafuni kisha akaingia kulala.  Alikuwa akiishi na wazazi wake.  Kutokana na ukubwa wa nyumba yao, alipewa vyumba vya uani vilivyokuwa vikijitegemea kila kitu.  Alikutana na wazazi wake mara nyingi wakati wa chakula cha jioni, isipokuwa mara moja moja akiwa na mtoko.

Alijitupa kitandani akiwa na uchovu mwingi kutokana na shughuli nyingi kazini kwao.  Ilimuwia vigumu kupata usingizi mapema.  Mawazo mengi yalianza kukiandama kichwa chake.  Akamfikiria Hafsa.  Akamfikiria Ali.  Pia akafikiria juu ya Benito.  Alikuwa njia panda.  Hakujua nini kilicho mbele yake.

Ni muda mrefu umepita.  Akawaza hivyo.  Ni muda ambao ungemtosha kabisa Benito kuyasahau mambo yote na kuyapuuzia.  Pengine haijawezekana.  Akashangaa.  Akadhani anaweza kusaidia pengine.  Ni vipi ataweza kama itambidi kushiriki?

Akamfikiria Hafsa, binti mtaratibu asiye na makuu hata kidogo.  Mwepesi wa kusamehe.  Mwenye wivu kupindukia.  Mwenye msimamo anayesimamia kidete maamuzi yake.  Picha ya Hafsa ikamjaa akilini mwake akimtazama kwa macho yake mapole mithili ya njiwa mwenye kutaka kuonewa huruma.  Vipi kama kuna jambo baya dhidi yake?  Lakini itakuwaje kwa Benito?  Kwa nini aendeleze mambo yaliyopitwa na wakati?

Potelea mbali.

Liwalo na liwe.

Aliposhituka usingizini, tayari ilikuwa imetimu saa kumi na mbili asubuhi.  Kipindi cha amka na BBC ndiyo kilikuwa kinaanza kurushwa hewani na redio ya BBC.  Kama ilivyo desturi yake, akafanya kidogo mazoezi ya viungo kabla hajaingia bafuni kujisafi.  Hata hivyo kichwa chake hakikuweza kuutua mzigo mkubwa wa mawazo.

Alipofika ofisini kwake yapata saa moja unusu, alifanya kazi zake muhimu haraka hadi saa tatu.  Kisha akampigia simu Benito wakutane muda huo.  Wakakubaliana kukutana stendi kuu, upande ilipo MR hoteli.  Walipokutana ndipo Johari akampigia simu Hafsa kwa kumshawishi ili wakutane.

“Akifika tutakwenda kuongea naye pale Mtakuja restaurant.”  Johari alimwambia Benito baada ya kukubaliana na Hafsa.

“Usihofu Johari.  Kila kitu kitakwenda sawa.  Akiingia ndani ya teksi nitamwomba akubali tukae mahali tuzungumze.  Najua hawezi kukataa.  Nakushukuru sana kwa kuacha kazi zako kwa ajili yangu.”

“Usihesabu Ben.”

“Halafu nilitaka kusahau.  Jamaa zangu wamenipigia simu kesho wanaondoka Mbozi.  Napaswa kuungana nao Ipogoro kwa safari ya Dar.  Nashukuru kwani nitaondoka na mafanikio.”

“Itakuwaje incase leo maongezi yasilete hitimisho unalilitarajia?”

“Mi’ mwenyewe nawaza sana hata nisijue la kufanya.”

“Kwa nini basi usiondoke hata Jumapili?”

“Haitowezekana hata kidogo.  Ofisini kwetu tunafanya kazi hata siku za Jumamosi.  Hivyo keshokutwa tunapaswa kuwa ofisini ili tutoe ripoti ya kazi tuliyokwenda kuifanya.”

Johari alipokwenda kupiga simu mara ya pili, hakujua anaonwa na Hafsa.  Aliporudi pale dukani akamwambia Benito waende kukutana naye.  Johari alitaka waende kwa miguu.  Toka awali Benito alisisitiza ni lazima wachukue teksi.  Johari alikataa, Benito alipong’ang’ania sana akalazimika kukubaliana naye.  Mashaka yakampata huenda Benito ana dhamira ya kwenda nao mbali na si Mtakuja ambayo ipo upande wa pili wa stendi barabara ya Mashine Tatu.

Wakachukua teksi.

Walipofika kontena la Vodacom hawakumwona Hafsa.  Johari akashuka garini na kujaribu kumtazama Hafsa pande zote bila mafanikio.  Akaingia ndani ya kioski kilicho mkabala na kontena hilo, hakumwona.  Roho ikamdunda kwa kasi.  Akahisi halikosi jambo.  Akarudi hadi garini.

“Hakuna cha Hafsa wala nini!”

“Haiwezekani.  Wacha masihara yako!”  Benito alionesha dhahiri kushtushwa na jambo hilo.

“Masihara ya nini tena?”

“Hebu jaribu kumpigia simu ili ujuwe yupo wapi.”

Johari akaitoa simu yake kutoka kwenye  mfuko wa koti zito la manyoya za sufi alilokuwa amelivaa.  Akajaribu kuipiga namba ya Hafsa.  Mashine ikamjibu namba haipatikani.  Akabaki kinywa wazi.

“Nini tena?”  Benito aliuliza alipoona Johari ameachama mdomo.

“Haipatikani Ben.”

Sure?”

Johari hakujibu kitu isipokuwa aliendela kumtazama Benito kwa macho ya kumsuta mno kana kwamba kuna jambo amelisababisha.  Benito naye akazidi kuchanganyikiwa.

“Sasa Johari unadhani kwanini akudanganye halafu azime simu?”

“Mimi nd’o nikuulize wewe hilo swali.”

“Ki vipi?”

“Umeniingiza kwenye mgogoro ambao sikuuhitaji.  Sijui hata kwa nini nilikubali.”

“Hayo yametoka wapi?”

“Siyo suala la yametoka wapi Ben!  Wewe unafahamu fika kuwa kuna uhasama baina yenu.  Umekuja ili nikusaidie.  Lakini ulisahau Hafsa si mtu wa kukurupuka kufanya kitu asicho na hakika nacho.  Nina wasiwasi kwa machale yake lazima aliingia wasiwasi, ama ametuona.”

“Ki vipi?”

“We’ uliza tu maswali.  Lakini uliyakoroga mwenyewe.  Wala leo tusingekuwa hapa.  Nina uhakika katuona mahali na nd’o sababu katucheza shere kisha akazima simu.”

“Hapana Johari.  Nina hakika hajatuona.  Wewe uliniambia yupo Mwembetogwa.  Na ulipompigia mara ya pili akakwambia anakuja.  Akajua mnakutana stendi sasa iweje uhisi katuona?”

“Kama amekuja kwa teksi lazima atakuwa ameingilia MR kwa kupitia Mkwawa Road.”

“Ngumu kuwa hivyo.  Ninavyomfahamu, siyo mtu wa kupenda raha hivyo.  Hapo Mwembetogwa ni pa kutembea dakika kumi tu mtu unafika stendi.”

“Siyo unavyomfahamu, sema ulivyokuwa ukimfahamu.  Wewe mwenyewe jana umeniambia, kadri nyakati zinavyobadilika na watu nao hubadilika.”

“Mmh!  Hilo nalo neno.”

“Sasa Ben unadhani kwa nini amenidanganya?”

“Nami pia nakosa majibu.”

“Na kama Hafsa ametuona, na anajua unamfuatilia, lazima atajenga kisirani dhidi yangu.  Nimejiponza mwenyewe.  Mara ya kwanza alinisamehe, sasa hatoweza.”

“Usifike huko.”

“Umenifikisha mwenyewe.”

Baada ya kubishana sana, wakaamua kwenda Mwembetogwa sekondari.  Huko walijibiwa na mtu wa mapokezi kuwa Hafsa aliaga anakwenda stendi kukutana na mtu.  Wakarudi hadi stendi.  Wakaangaza pande zote na bado hawakuweza kumwona.

“Benito, hebu niambie ukweli.  Tangu ufike hapa hujampigia simu?”  Johari aliuliza baada ya juhudi zao za kumtafuta kugonga mwamba.

“Nilimpigia.”

“Ayaaa!  Hapo ndipo ulipo haribu kabisa.  Mbona tulikubaliana usiwasilianae naye?  Tena wewe nd’o ulisema hivyo.  Yalikushinda yepi tena?”

“Yashatokea.  Kwanini tusiende kwao?”

“We we we we weeeee!  Thubutu yako.  Huko sikushauri kabisa.”

Wakaagana.  Wakaachana.

Johari akarudi kazini kwake.  Ni kama aliyavuruga zaidi mawazo yake.  Alihisi haikosi namna, lazima Hafsa atakuwa amemshtukia tu.  Kama itakuwa hivyo, aliendelea kuwaza, basi itakuwa ni bahati mbaya sana kwake.  Hata hivyo akajipa moyo kuwa hata kama atakuwa amemwona, bado yeye atakuwa na wigo mpana sana wa kujitetea kuwa hakujua kilichokuwa kikiendelea.  Johari hakujua kuna kitu kipya kinaendelea kwa Hafsa kwa upande moja, na kwa Benito kwa upande mwingine.

Hakuweza kabisa kufanya kazi kwa siku nzima.  Hakupata hata chakula cha mchana.  Hakuwa na hamu ya kufanya hivyo.  Alikuwa na miadi ya kukutana na Benito kwa chakula cha jioni.  Japokuwa hakuwa na raha kabisa kutokana na mambo hayo, aliona kuna umuhimu wa kuitimiza miadi hiyo ili aweze kuzungumza na Benito kwa kirefu kuhusiana na mambo hayo yaliyozidi tu kumpa kizunguzungu.

Walipanga kukutana Adon Restaurant iliyopo mtaa wa Haile Sellassie, Gangilonga.  Hivyo ilipotimu saa mbili jioni, tayari Benito na Johari walikuwa ndani ya Adon kwa chakula cha jioni.  Johari bado alikuwa na wakati mgumu kwa mambo yaliyotokea mchana huo.  Vivyo hivyo hali ilikuwa tete zaidi kwa Benito.

Johari akamwuliza. “Kwa hiyo umeamuaje Ben?”

“Kesho lazima kuondoka.”

“Suala lako la kukutana naye?”

“Naomba tufanye kesho.  Basi litapita Ipogoro saa sita mchana.  Itakuwa poa kama tutamtafuta asubuhi ili walau saa tano unusu niwe njiani kwenda Ipogoro.”

Johari hakujibu neno.  Akamtumbulia Benito macho kiwango cha kumfanya Benito ayakwepeshe macho yake pembeni.  Johari akaendelea kumtazama Benito kwa chati.  Akaacha hata kula.  Akaonesha wazi kuna kitu anachokifikiria sana.

Benito alipogeuza macho yake na kumtazama Johari, akabaini kuwa amezama katika lindi refu la mawazo.

“Unawaza nini bibie?  Kula basi, chakula kinapoa.”  Johari akashituka kutoka mawazoni.  Akamtazama Benito kwa macho ya upole sana.

“Nakula Ben.  Unajua hiki chakula ni kitamu sana.  Nakifeel ndiyo sababu nakula kwa mapozi.”

“Punguza basi mapozi, chakula kitapoa halafu utashindwa kukifeel tena.”

Johari hakujibu kitu, isipokuwa aliyanyanyua macho yake na kumtazama Benito.  Benito alitingwa na chakula chake.

Alipoona Benito hana habari naye, akaamua kumwongelesha.

“Ben?”

“Naam!”

“Nikuulize swali?”

“Uliza tu.”

“Hivi ni kwa nini umeamua kunishirikisha mimi mambo yako na akina Hafsa?”

“Kwa nini umeniuliza hivyo?”

“Aulizaye ataka kujua.  Hujajibu swali langu.  Wewe nijibu, then kama una swali ndipo utauliza.”

“Ok.  Nimekushirikisha kwa sababu naamini utanisaidia.”

“Unaamini kweli naweza kuwa msaada kwako?”

“Kwanini nisiamini?”

“Mbona unapenda sana kuuliza maswali kabla ya kujibu unayoulizwa wewe?”

“Ndivyo nilivyozowea.  Ni kweli naamini utanisaidia.”

“Nikikataa kukusaidia utanichukia?”

“Mmh!”  Benito aliguna kwanza.  Kisha akajibu. “Hapana sitokuchukia.  Lakini kwa nini ukatae kunisaidia?”

“Kwa sababu sioni umuhimu.  Ni kama unapoteza muda wako tu.  Ben, jambo unalojaribu kulifanya haliwezi kuzaa matunda asilani abadani.”

Benito akabadilika ghafla.  Akaonesha kugadhabika.  Johari aliliona hilo.  Hakuwa na budi kusema ukweli.  Baada ya kuwa amefikiria sana kutokana na tukio la mchana, akaona ni ujinga kwa jambo analolifanya Benito.  Kwa muda uliopita tangu uhasama huo utokee, hakuona kama kuna haja ya kuuendekeza.  Johari akamgutusha Benito kutoka alikokuwa amezama kimawazo.

“Ben?”

“Sema.”

“Samahani kama umekwazika.  Lakini nadhani nawiwa kukwambia ukweli.”

“Nafurahi kusikia hicho kitu unachokiita ukweli.”

“Sasa rafiki yangu Ben, kwa mtindo huo hatutofika.  Usipende kukasirika kasirika juu ya vitu vidogo.”

Benito hakujibu chochote.  Akamwita mhudumu ili alete bili.  Johari akamsikitikia Benito.  Akajipa ushindi kwamba ujumbe wake umefika kama alivyoukusudia.  Bili ilipoletwa, Benito akaanza kulipa kabla hajakatishwa na Johari.

“Wacha mambo yako wewe!  Mimi ndiye niliyekualika hii dinner.  Napaswa kulipa mimi.  Then nalipa mimi.”

Johari akalipa.

Wakawa nje ya Adon wakipanda teksi kila mmoja kurudi kwake.  Ndani ya gari, kila mmoja alikuwa mbali kifikra.  Hakuna aliyezungumza hadi walipokuwa wanaiacha barabara ya Kawawa kuingia ya Uhuru.  Ndipo Johari alipozungumza.  “Leo ninakupeleka kwanza kwako Ben, kisha nitakwenda Kihesa.”  Alipoona Benito hajibu kitu, akaendelea.  “ Dereva, tupeleke kwanza White Staff Inn ya stendi kisha utanipeleka Kihesa.”

Dereva hakuwa na hiyana.  Akawapeleka.

Walipofika Johari akamwomba dereva amsubiri kidogo.  Akaongozana na Benito hadi chumbani kwake.  Walipofika humo bado Benito alionekana kutokuwa sawa kwa hali yake ya moyo.  Walipoingia. Johari akaurudisha mlango kisha akauegamia.  Akaushika mkono wa Benito na kumvuta karibu hata akawa sambamba naye.

“Ben, rafiki yangu usimind mambo haya.”  Benito hakujibu.  Johari akaichukua mikono ya Benito na kuiweka mabegani mwake.  Wakawa wamekumbatiana.  Johari akampiga Benito busu zito juu ya mdomo wake.  Benito akashusha pumzi kwa nguvu.

“Ahsante Johari.”

“Usijali.  Bado nakupenda Ben.  Kwa heri.”  Johari aliposema hivyo, akamwachia Ben na kufungua mlango.  Akaondoka kwa mwendo wa haraka.  Nje akapanda ile teksi iliyokuwa ikimsubiri.

Kama ulivyokua usiku uliopita, haikuwa rahisi kwake kupata usingizi.  Mawazo ya raha ya dakika ya mwisho na Benito yaliyochanganyika na hatia, ndiyo yaliyokiandama kichwa chake.

Akapitiwa na usingizi.

Alipoamka siku ya Ijumaa ratiba yake haikutofautiana na siku nyinginezo.  Ilipotimu saa mbili akaamua kumtumia ujumbe Hafsa.  Hakupata majibu.  Akawa anatuma ujumbe kwa Hafsa kila baada ya muda fulani.  Kila mara hakujibiwa.  Hali hiyo ikaendelea kumchanganya zaidi.  Akawa haishi kuhisi lazima lipo jambo linalomfanya Hafsa kuwa vile.  Jambo hilo likamchanganya sana.

Benito alipompigia simu wakutane kwa minajili ya kwenda kwa Hafsa kama walivyopanga, akaamua kumdanganya hawezi kukutana naye kwani anahudhuria kikao muhimu kilichoitishwa ghafla na Mkurugenzi wa manispaa.  Ikambidi Benito kukubaliana na hali halisi.  Akaondoka zake hadi Ipogoro kuungana na wenzake.

Hadi kufikia saa tano asubuhi hiyo, Johari alikuwa ametuma ujumbe zaidi ya mara sita kwa Hafsa bila majibu.  Akajikuta hana namna.  Maadamu alianzisha mwenyewe, akawa hana budi kuyamaliza mwenyewe.  Akaamu kwenda nyumbani kwao ili akuzungumze naye na kuupata upande wa pili wa sakata hilo ambalo yeye aliliona lisilo na kichwa wala miguu.

Alipofika Mwembetogwa, nyumbani kwa akina Hafsa, alimwona Hafsa akielekea kumwaga takataka.  Akaongeza kasi na kumfikia.  Mapigo ya moyo wake yalikwenda kwa kasi kubwa sana.  Alipotokea Hafsa mbele yake na kushituka, Johari akathibitisha kuwa Hafsa amekirihika dhidi yake.  Akahisi kitu chenye ncha kali kama ya sindano kikimchoma moyoni mwake.  Pale Hafsa alipokaa chini,  Johari naye akaishiwa nguvu.  Akajikaza.

Hafsa alipomkaribisha, Johari alikuwa tayari amechanganyikiwa mara alfu ya awali.  Akalazimika kuingia ndani kwa kuwa alikuwa ameshikwa mkono na Hafsa.  Akatamani kughairi na kuondoka zake ili kuendelea na mambo mengine.

Hafsa alipomwacha Johari ameketi barazani, Johari alikuwa katika kipindi kigumu zaidi.  Pamoja na kumfahamu Hafsa kama mtu asiyependa mambo ya magomvi, hapo alihisi walakini.  Akahisi kuna jambo baya Hafsa anakusudia kulitenda.  Akazingatia pale ni nyumbani kwao, endapo angedhuriwa kwa lolote asingeweza kujitetea.  Alifuata nini?

Kwa muda mfupi tu, akawa amejiuliza maswali mengi sana yasiyokuwa na majibu.  Alipoona Hafsa anachelewa kutoka ndani, hofu ikamjaa zaidi.  Akajishauri kama ni kuzungumza, basi watazungumza siku nyingine wakati hali imepoa.  Akainuka taratibu kutoka alipokuwa ameketi.  Akanyata hadi kulifikia geti.  Akalifungua taratibu na kuondoka zake.

Alipofika nje alitembea kwa mwendo wa kasi sana.

Akadhani ndiyo atapata amani moyoni.

…………..itaendelea

Na Fadhy Mtanga

Mtanga ni mtunzi wa kitabu cha riwaya, HUBA anayepatikana Dar es Salaam. Unaweza mfatilia katika mtandao wa Twitter kupitia: @FadhyMtanga na kupata kitabu chako cha HUBA kwa namba: +255 (0)715 599 646

 

Leave a Comment