Riwaya ya Kizungumkuti: Sura ya tano

KizungumkutiDar es Salaam

Jumatatu, Mei 5, 2003

 

 

Takribani mwezi sasa ulikwishatimu tokea Ali akutane na Benito.  Ali akawa katika maandalizi kwa safari ya Hong Kong kufunga bidhaa.  Ilikuwa ni siku ya Jumatatu huku yeye akitarajia kuondoka siku ifuatayo.  Akawa anarudi nyumbani kwake.  Kwanza, akashangaa kuliona geti likiwa wazi.  Akapatwa na hofu.  Haikuwa kawaida kwa geti hilo kuwa wazi.  Akatembea kwa kunyata hadi alipokaribia nyumba.  Akasikia sauti za Hafsa na Maulid kutoka verandani.

“Wewe!  Siku nyingine utaua mtu na masikhara yako.”  Ilisikia sauti ya Hafsa.  Hafsa alikuwa ameishiwa nguvu na mapigo ya moyo wake yakienda kwa kasi kubwa.  Akashusha pumzi kwa nguvu.  Alikuwa amepata mshituko fulani aliposikia hatua za mtu anayetembea kwa kunyata kuelekea mahali alipokuwa na Maulid.

“Pole sana honey.

“Umenishtua sana Ali.”  Hafsa akawa anazungumza kwa sauti kali iliyojaa hasira na kuchanganyikiwa.  Maulid alitulia kuwashuhudia wanandoa hao.

“Nisamehe basi mke wangu.”

“Bwana eeh!  Yashaisha.”  Hafsa aliitoa kauli hiyo katika namna ambayo haikumpendeza kabisa Ali.  Alionesha dhahiri kukasirishwa na kitendo kile.  Ali naye akakasirishwa kwa kujibiwa kwa sauti ya ukali mbele ya Maulid.  Akajitahidi kutozionesha hasira zake na kumsalimu Maulid.

“Vipi mheshimiwa.  Mambo yako?”

“Aaah!  Safi tu shem.  Shikamoo.”

“Marahaba.  Vipi shule inakwendaje?”

“Safi tu shem.”

“Ok.  Mie nipo ndani.”  Ali akaitoa sentensi hiyo huku akitembea kuelekea ulipo mlango.  Hafsa akawa ametambua kuwa Ali hakupendezwa kabisa na hali ile.  Ali si mtu wa kupenda malumbano bali ni mwenye kuhifadhi moyoni hasira zake.  Siku zote huepuka kujibizana na watu inapotokea kushindwa kuelewana.  Akaingia zake moja kwa moja hadi chumbani.  Kajitupa kitandani huku akijaribu kumfikira Hafsa na tabia aliyoionesha.  Lakini akafahamu ni lazima kuna suala la Benito katika hali aliyowakuta Hafsa na Maulid.  Wakati akiwa katika lindi la mawazo Hafsa akaingia.  Akamwendea Ali moja kwa moja na kumbusu shingoni.

“Nakuomba unisamehe mpenzi wangu.  Najua hujafurahishwa na tabia yangu.”

“Sina neno.”

“Usiseme hivyo mume wangu utaniumiza.  Nimekukosa, tafadhali nisamehe.  Usipofanya hivyo utaniumiza sana.”

“Siku nyingine uwe unatumia akili.”

Ali akamshika Hafsa shingoni kwa mkono wake wa kushoto na kumbusu taratibu juu ya mdomo.  Hafsa akawa anamwangalia Ali kwa macho malegevu mno.  Si punde wakawa nje wakiungana na Maulid ambaye alikuwa akiendelea kunywa soda yake.

Hafsa na Maulid wakautumia wasaa huo kumsimulia Ali habari ya ujio wa Benito shuleni kwao.  Ijapokuwa hakuonesha hofu yoyote kwa Hafsa na Maulid, ukweli ni kwamba hali hiyo ilimgutusha sana Ali.  Alifahamu kuwa Benito anawatafuta, lakini bado hakudhani angeweza kuwa na dhamira yake kwa kiasi kikubwa hivyo.  Hata hivyo Ali akajitahidi kumpa moyo mke wake ili kumfanya asizongwe na mawazo yatakayoendelea kumjenga hofu tele moyoni mwake.

“Maulid usitie shaka.  Ni mambo madogo tu haya, yatakwisha muda si mrefu.”  Ali akawa anazungumza wakimsindikiza Maulid kurudi kwao.

Wakati Hafsa anafunga geti, simu ya Ali ikaita.  Hafsa ndiye aliyekuwa ameishika simu hiyo.  Akaitazama kwa makini sana namba ya mpigaji.  Kwa kuwa namba ya mpigaji ilikuwa imefichwa, Hafsa hakubanduka kwa Ali.  Alikuwa na shauku tele ya kumfahamu mpigaji huyo na dhumuni lake.

“Helo!”

“Mambo vipi Ali?”

“Salama tu.”

“Mbona unajibu kwa hofu?”

“Hapana siyo hofu.  Kwani wewe ni nani mwenzangu?”

“Wewe!  Tuseme hujanitambua?  Mie ni Atu.”

“Ahaa!  Tatizo hizi private number zenu zinatuchanganya.”  Hafsa aliposikia tu kuwa ni Atu akasogeza sikio lake karibu kabisa na simu.  Lengo kuu likiwa ni kuhakikisha anayapata mazungumzo yote.

“Vipi Atu, mzima wewe?”

“Nipo gado best.  Nd’o nini kunisusa hivi?”

“Sijakususa hata kidogo.  Mambo fulani yalikuwa yamenitinga.”

“Sawa.  Nafahamu hilo.  Vipi Benito hajakutafuta tena?”  Aliposikia swali hilo, Ali alisita kidogo.  Akamtazama Hafsa, kisha akaendelea.

“Kidogo tu, wala usijali.”

“Sawa.  Nina ombi moja Ali.”

“Enhee, sema.”

“Alhamisi nitakuwa free.  Nakuomba tukutane siku hiyo mchana.”

“Ooh, sorry!  Kesho natarajia kusafiri Atu.  Itanichukua almost two weeks.

“Sawa.  Tutapanga siku nyingine.”

“Usijali.”

“Byee!”  Atu akakata simu.

Hafsa alishabadilika na macho yake yakawa mekundu.  Ali akaimaizi hali hiyo lakini hakuwa na la kufanya.  Kama hajaona lolote vile akamshika Hafsa kiunoni na kuanza kutembea taratibu kama ilivyokuwa desturi yao.  Hafsa hakuwa na furaha hata kidogo.  Akajilazimisha kutembea.  Walipofika chumbani Hafsa akaketi kwenye sofa huku akiwa ameinamisha chini kichwa chake kuashiria amezama mawazoni.  Ali akaendelea na kupanga panga vitu humo ndani akijifanya hana habari na linalomsibu Hafsa.

“Ali!”  Hafsa akaanzisha baada ya kuona Ali hana dalili za kumzingatia.

“Sema.”

“Hivi unanichukuliaje?”

“Kivipi?”

“Atu ni nani yako?”

“Sikiliza Hafsa.  Unafahamu fika mie sipendi vitu vidogo vidogo kulazimishwa kuwa vikubwa.”

“Hivi ni vitu vidogo siyo?”

Anyway.  Inawezekana siyo vidogo.  Hebu nieleze nini tatizo lako?”

“Sikiliza Ali.  Nahitaji kufahamu ukweli.  Nini kipo kati yako na Atu?  Tafadhali sihitaji unifiche kitu.”

“Wala sikutegemea kama ungefika mbali hivyo mpenzi wangu.  Kama umejisikia vibaya kwa simu aliyonipigia, pole sana mke wangu.  Wewe mwenyewe unafahamu Atu ni nani.  Kumbuka siku ile yeye ndiye aliyenisaidia hata nikamkwepa Benito.”

“Ali, usiseme siku ile.  Sema siku zile.”

“Yah!  Ni kweli kanisaidia mara hizo mbili.”

“Tafadhali Ali.  Nakuomba unisikilize.  Na pia unielewe.  Kumbuka mimi ni mke wako.  Nahitaji sana kulindwa nawe kimwili na kiakili.  Hebu jaribu kufikiria mume wangu.  Nikiwa mkweli mbele ya Mungu, sipendi, sipendi, sipendi kabisa mawasiliano na Atu.  Mawasiliano hayo yafe.  Unanielewa?”

“Nakuelewa vema.  Lakini sijajua ni kwa nini?”

“Nataka kuwa na amani moyoni.  Ni haki yangu kuwa na wivu juu yako.  Usinipe nafasi nianze kuwa na wasiwasi juu yako.  Hata kama wewe ndiye ungekuwa Hafsa ungelazimika kutafuta logic.

“Kivipi?”

“Kumbuka wewe mwenyewe ndiye uliyenisimulia kuwa Atu alishawahi kukusevu usiku ulipokutana na askari Mbeya.  Si ndiyo?”

“Ndiyo.”

“Pia akakusevu tena siku ile Benito alipokudhibiti mjini.  Japo uliniambia mlikutana by coincidence, nina mashaka nalo.  Bado kama haitoshi akakugharamia kila kitu siku hiyo utadhani wewe huna pesa.  Nikidhani yamekwisha, leo anakupigia simu kukuomba mkutane.  Inakuja kweli Ali?”

Take it easy.

No Ali!  Kuna mambo ya kuyarahisisha.  Lakini siyo usalama wa ndoa.  Nakuhitaji uwe mkweli kwangu.  Niahidi kwamba utakaporudi hutomtafuta huyo Atu.”

“Nakuahidi mke wangu.””

“Lakini ukumbuke kuwa wewe ndiye uliyenifundisha umuhimu wa kutovunja ahadi katika maisha.”

“Usijali.  Nitatunza ahadi.”

Hafsa akawa amerejewa na amani hata akambusu mumewe shavuni.  Kwa asili, Hafsa ni mpole kama alivyo Ali.  Tatizo kubwa ni mwenye wivu kupindukia juu ya mumewe.  Jambo lolote likitokea lenye kumhusisha Ali na jinsia nyingine lazima Hafsa atakasirika tu.  Ali amelifahamu hilo tangu kuanza kwa uhusiano wao.  Mara zote amekuwa akijitahidi kutomfanya mkewe akose raha. 

Siku hiyo ikaisha kama zilivyo siku zingine kwa wanandoa wapendanao.

Ali na Hafsa walikubaliana kuwa wakati Ali anakwenda safarini Hong Kong, Hafsa arudi Iringa akapumzike walau kwa muda mfupi ili kupunguza hizi rabsha ambazo pengine zingepunguza furaha katika ndoa yao.

Asubuhi ya siku iliyofuata Hafsa akaenda shule kuomba ruhusa.  Alimwacha Ali nyumbani akifanya maandalizi ya safari kwani angeondoka mchana wa siku hiyo.  Hafsa akalazimika kumdanganya mkuu wa shule kuwa ana matatizo ya kifamilia yaliyotokea huko kwao Iringa yanayohitaji uwepo wake.  Mkuu wa shule, mzee mmoja ambaye amefanikiwa kuufikisha umri uliokinakshi vema kichwa chake kwa mvi nyingi aliwachukulia walimu kama wanawe.  Kwa uzoefu wake kama mkuu wa shule mbalimbali za serikali tangu miaka ya mwanzo ya uhuru, mzee Kyamani alifahamu vema nini maana ya matatizo ya kifamilia.  Aliyachukulia matatizo ya walimu na wanafunzi kwa uzito ulistahili.  Baada ya kuwa amestaafu utumishi wa umma, aliingia mkataba na mmiliki wa shule hiyo ili aweze kuendelea kuutumia vema ujuzi na uzoefu wake.  Hafsa alipewa ruhusa bila kikwazo.

Nyumbani, Ali alikuwa akiendelea na maandalizi yake.  Wakati akimaliza kupanga nguo kwenye sanduku lake, simu yake ikaita.  Alipoiangalia, namba ya mpigaji ilikuwa imefichwa.  Lakini akaweza kukisia mpigaji.  Akaipokea.

“Mhuu!  Habari?”

“Safi tu.  Mambo?”  Sauti ya upande wa pili ilimtambulisha kuwa ni Atu.

“Swadakta Atu.”

“Unategemea kuondoka saa ngapi?”

“Saa sita kamili mchana.”

“Tunaweza kuonana kabla hujaondoka?”

“Hapana Atu.  Itaniwia vigumu.  Kuna mambo kadhaa sijayakamilisha.”

“Japo dakika tano tu Ali.”

“Dakika tano tunaweza.  Lakini hofu yangu ni kwamba hazitotosha kuzungumza hata hamu zikatuisha.  Bali zitaongeza kiu.”

“Ningependa sana kukuona Ali.”  Namna Atu alivyokuwa akizungumza, walai nyoka angetoka pangoni.

“Usitie shaka Atu.  Nitarudi, tutaonana.  Tutabonga hadi maneno yatuishe.” 

“Haya bwana maneno yako mie siyawezi.”

“Hakuna lolote katika maneno yangu.”

“Lolote lipo.  Unasema lolote?  Lipo sana.”

“Mbona sikuelewi?”

“Nakuzingua tu best.  Haya bwana, nikutakie safari njema.”

“Ahsante sana.  Nawe ubaki salama.”  Ali alipokuwa anaisema sentensi hiyo ya mwisho, Hafsa akaingia pasi hodi.

“Nani abaki salama?”  Ali akashituka, halafu akatulia.

“Kuna swahiba wangu tunafanya naye biashara.  Vipi shule umepewa ruhusa?”

“Nimepewa mpenzi.”  Hafsa akaenda hadi kitandani ilipokuwa simu ya Ali.  Akaibonyeza bonyeza bila kusema chochote. 

Ali akawa tuli akimtazama mkewe ilhali moyo wake ukienda mbio peapea.

Hafsa alipomalizana na simu akaenda jikoni kuandaa chakula.  Alishagundua Ali ametoka kuzungumza na Atu.  Mara hii akaamua kubaki kimya ili asionekane mwenye kukurupukia mambo.  Lakini ndani ya moyo wake lilimchoma vilivyo.

Baada ya kumaliza kula, Ali akaondoka.  Hafsa alimpeleka hadi uwanja wa ndege.  Wakati akirudi, Hafsa alizongwa na simanzi tele akiufikiria upweke atakaokuwa nao hadi Ali atakaporudi.

…………..itaendelea

Na Fadhy Mtanga

Mtanga ni mtunzi wa kitabu cha riwaya, HUBA anayepatikana Dar es Salaam. Unaweza mfatilia katika mtandao wa Twitter kupitia: @FadhyMtanga na kupata kitabu chako cha HUBA kwa namba: +255 (0)715 599 646

2 Comments

  1. Fadhy Mtanga says:

    Ahsante sana kaka Raphael. Unaweza kupata vitabu vyangu kwa kuagiza moja kwa moja nikatumia. Namba yangu ni +255 715 599 646

  2. Raphael Nyakundi says:

    Raha iliyoje! Hapa nchini Kenya nawezaje pata vitabu vyako?

Leave a Comment