Riwaya ya Kizungumkuti: Sura ya sita

KizungumkutiDar es Salaam

 Ijumaa Mei 9, 2003

 

 

“Ee bwana natoka mara moja.  Hadi saa tano hivi nitakuwa nimerudi.”

“Mshikaji mbona misele yako siku hizi imekuwa mingi sana?”

“Natafuta mke bwana.”

“Masikhara hayo Ben!”  Wote wakaangua kicheko.

“Sasa best natoka na gari yako.  Wewe si upo tu ofisini?”

“Yah!  Ila unanitisha mwana.  Hakuna noma chukua isipokuwa haina mafuta ya kutosha.”

“Usijali mwanangu.  Nita top up.”

“Nakuaminia.”

Benito akaondoka ofisini baada ya kuagana na mfanyakazi mwenzake aitwaye Nassoro.  Pamoja na kuwa na kawaida ya kuazima gari la Nassoro, hakupata kumshirikisha kilichokuwa kichwani mwake.  Alilichukua gari hilo na kuendesha moja kwa moja hadi Tabata Kimanga ilipo shule ya Kamene.

Alipofika shuleni hapo hakumtafuta moja kwa moja Hafsa wala Maulid.  Wanafunzi walionekana wamesimama katika makundi madogo dogo bila shaka wakijadiliana hili na lile kuhusiana na mitihani iliyokuwa ikiendelea.  Wanafunzi wa vidato vya chini walikuwa wakiendelea na masomo yao kama kawaida.

Benito alilipaki gari pembeni kabisa.  Akamwita mwanafunzi mmoja na kumwuliza endapo angeweza kumpata mwalimu Hafsa.

“Sina hakika kama yupo, sijamwona siku mbili tatu.  Ngoja nikamwangalie ofisini.”

“Endapo hutomkuta, tafadhali nisaidie kumpata mwalimu mwingine yeyote.”  Benito aliyatoa maneno hayo wakati mwanafunzi huyo akiondoka kuelekea ofisini kwa minajili ya kumwita mwalimu Hafsa.  Dakika chache tu baadaye, mwanafunzi huyo alirejea na kumtaarifu Benito kuwa mwalimu Hafsa hakuwepo kabisa.  Pia akamwambia imemwia vigumu kumpata mwalimu mwingine kutokana na utaratibu wa shule, mgeni lazima afike ofisi ya mapokezi.

Awali Benito alisita na kutaka kughairi.  Wazo jingine likampa hamasa aende tu.  Pamwe na shaka kiasi fulani, Benito akaenda moja kwa moja hadi zilipo ofisi za mapokezi kama ambavyo alielekezwa na mwanafunzi yule.  Alipofika alimkuta mama mmoja mtu mzima sana akichapa hili na lile kwenye kompyuta.

“Shikamoo mama.”

“Marahaba mwanangu.  Karibu sana.”

“Ahsante sana mamaangu.”  Benito alijibu huku akiwa ameduwaa kana kwamba hakijui kilichompeleka pale.

“Nikusaidie nini tafadhali?”

“Nahitaji kumwona mwalimu mmoja anaitwa Hafsa.”

“Ooh, pole sana babaangu!  Hafsa hayupo.”  Alijibu mama huyo kwa Kiswahili chake chenye lafudhi ya Kichaga.

“Hayupo, yupo nyumbani ama?”

“Hapana  kijana.  Kwani wewe ni nani yake?”

Benito akafikiria kidogo kabla ya kulijibu swali hilo, “Mi’ ni ndugu yake wa mbali kidogo.  Ni binamu yake.”

“Binamu siyo ndugu wa mbali babaangu.  Kwa hiyo wewe ni kakaake?” 

“Ni kweli mama.”

“Hafsa ameomba ruhusa kwenda kwao Iringa.  Kwani mara ya mwisho umewasiliana naye lini?”

“Ni muda mrefu kiasi.  Sikuwapo eneo lenye mawasiliano.  Ni kwa sababu gani ameomba hiyo ruhusa?”  Hapo Benito akawa na hakika na shauku ya kupata mengi.

“Amedai ni matatizo tu ya kifamilia, lakini hakueleza mengi.”

“Ok!  Nimekuelewa.  Kwa hiyo ni lini ameondoka?”

“Jumanne asubuhi ndipo alipoomba hiyo ruhusa.  Alisema anakusudia kuondoka siku hiyo hiyo.  Nadhani aliondoka.”

My God!  Kwa hiyo Jumatatu alikuwa kazini”

“Mbona unashtuka baba?”

Benito akagundua kosa lake, hata hivyo akalifukia vema shimo hilo, “Jumatatu ilikuwa nije nikaona uvivu kwani Jumapili nd’o nimerudi safarini.”

“Ahaa!  Jumatatu alikuwepo hadi saa tano tano hivi akadai anajisikia vibaya.  Akaomba ruksa na kurudi nyumbani.  Nadhani ndiyo muda huo alipata taarifa ambazo si nzuri zikamvuruga akili yake.”

“Aisii!”  Benito akajifanya kusikitika kwa kuguswa na kadhia iliyompata mwalimu Hafsa.

“Ungejaribu kuwasiliana naye kwa simu.”

“Nitafanya hivyo mama, sasa hivi nikitoka hapa.  Ahsante sana kwa taarifa.  Naomba nikuache uendelee na shughuli zako.  Ahsante sana.”

“Haya babaangu.  Ahsante sana na karibu tena eeh!”

Wakati Benito anageuka na kuanza kuondoka, yule mama akamwita.

“Aisee kijana!”

“Naam!”

“Hebu mara moja.  Kuna huyu mdogo wenu anayesoma hapa.  Huyo ndiye ameachiwa nyumba.  Nadhani pia anayo taarifa nzuri.  Umejaribu kuonana naye?”

Hapo Benito akachanganyikiwa nusura apoteze mahesabu.  Hakuwa akimfahamu mdogo yeyote wa Hafsa.  Akamaizi endapo hatokuwa makini basi angebainika ulaghai wake.  Akajipa moyo na kujibu.

“Hapana mama.  Sikuwa nimepata wazo la kumwulizia nilipofika hapa.”

“Basi ngoja uonane naye kabisa. Wewe keti pale kwenye benchi….”  Mama yule akamwonesha kwa ishara ya kidole mahali palipokuwa na fomu la kukalia wageni.  Benito alipogeuka na kuliona, yule mama akaendelea, “Namtuma kijana akamwite darasani kwao.  Atakukuta pale.  We’ zungumza naye tu hapo bila hofu.  Ni maalumu kwa wageni.”

“Ahsante sana mama.  Ngoja nimsubiri.”  Benito akaelekea pembeni kidogo palipokuwa na fomu hilo.  Moyo wake haukuwa na amani kabisa.  Hakuwa akimfahamu mhusika aliyekwenda kuitwa.  Hapo ikamlazimu kuubuni uwongo wa kuweza kukabiliana na mtu huyo ili kumsadikisha kuwa kuna undugu baina yao. Akawa anawaza na kuchanganua kwa jitihada zote. 

Mawazo yake yalikatishwa na mwanfunzi wa kiume aliyekuwa akija pale alipoketi.  Benito alishituka vibaya mno kumwona mwanafunzi huyo.  Ilhali mwanafunzi huyo akashituka sana kumwona Benito hapo.  Kila mmoja akabaki akiumauma mdomo wake kwa nukta kadhaa.

Maulid alipoitwa darasani kuwa kuna mgeni wake mapokezi, wala hakuwaza mgeni huyo angeweza kuwa Benito.  Hivyo aliondoka darasani haraka akiwa na shauku ya kumjua mgeni aliyemtembelea shuleni hapo.  Hadi anafika mahali hapo, Maulid hakuwa amezingatia jambo lolote la tahadhari.  Alipomwona Benito, akasimama ghafla.  Akataka kugeuza alikotoka.  Akafahamu kwamba kwa vyovyote vile atahitajika kujibu maswali mengi ambayo mengine hatokuwa akiyafahamu hayo majibu yake.

“Mambo vipi mdogo wangu?”  Benito alianza kumsabahi Maulid baada ya kumwona akiwa amebung’aa pasi kufahamu cha kufanya.

“Safi tu bro.  Shikamoo.”  Maulid akajilazimisha kusogea na kuketi.

“Marahaba. Vipi bwana?  Habari ya tangu siku ile?”

“Salama.”

“Nilikuja hapa kumcheki sister Hafsa.  Kwa bahati mbaya nimemkosa.  Nimeambiwa yupo safarini.  Nikaona si vibaya nikikujulia hali.”

“Ahsante bro.  Mi’ naendelea vema na shule.”

Benito akahitaji kutumia sentensi zenye kumtega Maulid ili apate kufahamu mambo aliyoyahitaji ufahamu.  Maulid naye akawa ameung’amua ujanja wa Benito.  Ingawa hakuona namna anayoweza kuukwepa.  Akaamua kuwa makini na maneno yake.  Hakufahamu Benito ameambiwa nini.  Lakini alifahamu fika kwa vyovyote vile kuna maelezo atakuwa ameyapata.  Kwa kuwa hakufahamu ni maelezo gani aliyoyapata mapokezi, akaamua kujaribu kula naye sahani moja.

Benito alifahamu kuna jambo Maulid analojaribu kulifikiria kwa makini.  Akampa muda kidogo huku naye akijaribu kuzipanga vema kete zake.  Akavuta pumzi kwa nguvu, kisha akatoa swali.

“Hivi Maulid, kwani mwalimu Hafsa kasafiri lini?”

“Mmh!  Sina uhakika sana na siku.  Ila Jumanne mida f’lani nilimwona kwa mbali.”

“Ok!  Vipi ile siku niliyokuja hukumpa salamu zangu?”

“Hapana bro.

“Kwa nini?”

“Nilizingatia maelezo yako kuwa mtu mwingine asifahamu.”

“Oh sawasawa!  Lakini uliporudi ulimwona japo kwa mbali?”

“Niliporudi kutoka wapi?”  Hapo Maulid akahisi kuna uwezekano mkubwa Benito alimwona alipomchungulia wakati akikata kona.

“Tulipoachana pale kituoni.”

“Mbona muda sikuwa nakuja shule.  Nilikwambia nakwenda Kisukulu.”

“Ok, Ok!  Nilisahau mdogo wangu.  Unajua jinsi unavyokuwa mtu mzima unakuwa na mambo mengi hadi mengine unasahau kirahisi.”

“Yah, naelewa.”

“Kwa hiyo unasema hukuonana naye tena hadi anasafiri?”

“Nimesema Jumanne nilimwona kwa mbali.”

“Pia unakumbuka kuwa leo tuna miadi ya kuonana?”

Yes, nakumbuka.  Lakini uliniambia kama nitapata nafasi.  Kwa kuwa tumekwishaonana nadhani hakuna la ziada.  Isitoshe nilipanga kukupigia simu kukujulisha nitashindwa kuonana nawe.  Jioni tunategemea kuwa na discussion na wenzangu.  Tunakaribia kuanza mitihani.”

Simu ikaanza kuita mfukoni mwa Maulid.   Maulid akapata aibu iliyochanganyika na woga kutokana na kumdanganya Benito kuwa hana simu siku ya kwanza walipokutana.  Akajaribu kuzuga hata simu ikakatika.  Benito alimtazama tu Maulid pasipo kutia neno lolote.  Aliamini kuna mahali atampata tu.

“Kwa hiyo lini unategemea kuwa na nafasi?”

“Inategemeana.  Wakati wowote ule mi’ nitakupigia simu.”

“Ok, usijali.  Tena ungenipa kabisa namba yako ya simu.  Mimi nitakuwa nakupigia mara kwa mara kukucheki kama upo free ama vipi.”  Benito aliamini huo ungekuwa mtego wake.

“Mimi sina simu bro.  Hii hapa ni ya mshikaji wangu darasani.  Niliazima ili nitume meseji.”

“Lakini pia haitokuwa vibaya endapo nitaipata hata hiyo namba ya rafiki yako ili nikupunguzie mzigo wa wewe kunitafuta.”

“Huyo jamaa hatuishi wote sehemu moja.”  Maulid alijibu huku uso wake ukiwa mkavu.

“Pamoja na hayo.  Kama utakuwa mbali naye nitakuwa nikimwachia ujumbe.”

“Sasa mbona ulisema haya mambo yawe baina yangu mimi na wewe tu?”

“Sikiliza Maulid.  Nadhani wewe unafikiri labda mimi nitamweleza huyo rafiki yako madhumuni ya mawasiliano yetu.”

“Siyo hivyo bro.  Mimi naona itakuwa kama usumbufu tu.  Nadhani jambo la msingi ni mimi kukupigia simu tu na si vinginevyo.”

“Usitie shaka Maulid.  Wewe nipe tu.  Tafadhali sana.  Please.”  Benito aliendelea kung’ang’ania kuipata namba hiyo.

Kuna watu ving’ang’anizi duniani!  Maulid aliwaza akilini mwake. 

Benito aling’ang’a hadi Maulid akakosa nguvu ya kuendelea kubishana naye.  Alichoamua ni kumpa namba yake ambayo haitumiki kwa muda mrefu.  Benito aliiandika namba hiyo kwenye simu yake.  Kisha akaagana na Maulid.  Maulid akarudi zake darasani. 

Benito akapita tena kwenye ofisi za mapokezi ili kuaga.

“Ooh!  Umemaliza babaangu?”

“Ndiyo mama.  Nakushukuru sana.  Nimepata maelezo kuhusu safari yake.”  Benito aliongea huku mikono yake kaiweka kifuani pake kuonesha heshima mbele ya mama huyo.

“Haya ahsante baba.  Bila shaka utawasiliana naye kwa simu.”

Yule mama alipoitoa kauli hiyo, Benito akaachama mdomo wake kuonesha mshangao uliosababishwa na usahaulifu fulani.  “Ooh!  Nimesahau kuchukua namba anayoitumia sasa kwa Maulid!”

Ikawa zamu ya yule mama kushangaa.  Akauliza. “Kwani amebadilisha namba yake ya simu?”

Nusura Benito akose jawabu kwa mama huyo wa Kichaga aliyeonekana kuwa mzungumzaji aliye makini.

“Hapana mama.  Ni kuwa, kuna wakati niliipoteza simu yangu na kupoteza namba za watu wengi.  Ndiyo maana nikashindwa kuwasiliana naye kwa simu kabla sijaja hapa.” 

“Ahaa!  Pole sana.  Kwa hiyo unaihitaji?”

Mungu ampe nini?  Akajibu  haraka, “Ndiyo mama.  Nitashukuru.”

Mama yule akaiandika namba ya simu ya mwalimu Hafsa kwenye kipande cha karatasi.  Akampa Benito.  Benito alifuarahi sana moyoni kwake kuona mambo yanaenda katika mstari ulionyooka.  Akaagana na mama yule na kuondoka zake.

Tangu awali, Benito alimtilia mashaka Maulid.  Alifahamu fika kuwa alimzunguka pale alipohitaji msaada wa kuitiwa mwalimu Hafsa.  Awali hakufahamu ni kwa sababu ipi hata Maulid akafanya hivyo.  Leo ndiyo akapata ufahamu kuwa kuna undugu kati ya wawili hao.  Hivyo akafahamu kuwa Maulid alipomjibu hapafahamu nyumbani kwa Hafsa alimdanganya.  Pia Maulid alidanganya pale aliposema hana simu ya mkononi.  Akahisi hata namba aliyoitoa Maulid ni ya uwongo.

Hivyo alipoingia garini akajaribu kuipiga namba aliyopewa na Maulid.  “Namba unayoipiga haipo.  Tafadhali angalia tena kwenye kitabu cha orodha ya simu……”  Hilo ndilo jibu alilokutana nalo lililotoka katika mashine ya kuratibu mawasiliano ya simu.  Hasira zikampanda hata akatamani kurudi.  Akajishauri juu ya subira kuvuta kheri.

Hakuwa na haraka na namba ya Hafsa.  Aliamini yule mama asingeweza kumdanganya.  Kitu ambacho kilimpa Benito wakati mgumu ni kutofahamu lini Hafsa angerejea.  Pia hakuwa na ufahamu juu ya mahali angeweza kumpata Ali.  Akaona anapaswa kutafuta janja ya kufahamu mahali wanapoishi.  Pia akawa bado na wakati mgumu juu ya namna ya kumfanya Maulid aseme ukweli.

Akaendelea kufikiri sana akiwa njiani kurudi kazini kwake.  Katika kufikiri kwake hili na hili akapata jawabu.

Ndiyo, akapata jawabu. 

Atalifanyia kazi.

Muda si mrefu.

Pengine.

 …………..itaendelea

Na Fadhy Mtanga

Mtanga ni mtunzi wa kitabu cha riwaya, HUBA anayepatikana Dar es Salaam. Unaweza mfatilia katika mtandao wa Twitter kupitia: @FadhyMtanga na kupata kitabu chako cha HUBA kwa namba: +255 (0)715 599 646

Leave a Comment