Riwaya ya Kizungumkuti: Sura ya Saba

KizungumkutiIringa

Jumatano, Juni 4, 2003

 

 

Yakiwa yametimu majuma manne kamili tangu Hafsa awasili mjini Iringa, habari za Benito zilianza kutomwumiza kichwa sana.  Ilikuwa ni siku ya Jumatano, nyakati za jioni, Hafsa alijipumzisha nyumbani kwao eneo la Mwembetogwa.  Siku nne zilikuwa zimekwenda tangu kuanza kwa mwezi Juni.  Baridi likuwa kali mno iliyopenya hadi kwenye mifupa.  Huu ndiyo wakati kwa wakazi wa mji huu kuunda ujamaa mkongwe na makoti pamwe masweta mazito.

Jumapili iliyokuwa imepita, siku tatu nyuma, Ali alirejea Dar es Salaam kuendelea na shughuli zake za biashara.  Ali alikuwa amekaa ughaibuni kwa takribani majuma mawili kama alivyokuwa amepanga.  Baada ya kurudi nchini, aliratibu kwanza shughuli zake na kuziacha katika utaratibu mzuri.  Baada ya hapo akasafiri hadi mjini Iringa kwa mkewe kipenzi.

Si Hafsa wala Ali aliyekuwa amebugudhiwa tena na habari za Benito.  Siku chache alizozitumia Iringa, Ali alijitahidi kumfanya Hafsa aamini zile zilikuwa ni mbio za sakafuni tu ambazo daima huishia ukingoni.  Kama ilivyokuwa kwa Ali, Hafsa naye akafikiria na kuamini lazima Benito apoteze morali baada ya kugundua yeye hayupo tena Dar es Salaam.

Hafsa alipowasili Iringa alikwenda hadi shule ya sekondari ya Mwembetogwa kuomba nafasi ya kufundisha hapo.  Kutokana na heshima ambayo baba yake alikuwa amefanikiwa kuijenga mjini hapo kwa miaka mingi, lisingekuwa jambo rahisi kwa Hafsa kukosa nafasi.  Baba yake Hafsa, mzee Kalinga amekuwa kiongozi wa chama na serikali kwa miaka mingi hadi kustaafu kwake miaka minane iliyopita.  Hadi anastaafu utumishi wa umma, alikuwa ni katibu tawala wa mkoa wa Iringa.  Kwa mantiki hiyo aliendelea kupata heshima kwa wakazi wengi wa mji huo ambao ni moja ya miji mikongwe na maarufu zaidi toka enzi za ukoloni wa Wajerumani na hatimaye Waingereza.

Baada ya kuwa ameipata nafasi hiyo, Hafsa aliamua kuendelea kuwepo mjini hapo kwa muda fulani.  Hafsa na Ali waliafikiana Ali aendelee kuishi Dar es Salaam lakini akiwa anamtembelea mkewe mara kwa mara.

Jumatano hiyo ilikuwa na baridi kali sana tofauti na siku zinginezo.  Hafsa alikuwepo nyumbani akisoma magazeti na majarida mbalimbali.  Ratiba ya  shule haikumghasi sana kwani wanafunzi walikwenda likizo isipokuwa vijana wa kidato cha nne ndiyo waliobaki kwa ajili ya maandalizi ya mitihani yao ya mwisho.  Hafsa naye akapewa vipindi viwili kwa wiki katika kidato hicho.  Hivyo muda wake mwingi aliutumia nyumbani.

Wakati akiinuka barazani alipokuwa ameketi muda mrefu ili akaongeze koti jingine kutokana na baridi kali, simu yake ikaita.  Hakuwa ameitarajia simu yoyote nyakati hizo.  Muda mfupi uliopita alikuwa ametoka kuongea na Ali.  Zaidi ya simu ya Ali ambayo aliiwekea mlio wa peke yake, hakuwa na kawaida ya kupokea haraka simu zingine.  Akaingiza mkono wake katika mfuko wa suruali ya jinsi aliyokuwa ameivaa.  Akaitoa simu hiyo.  Alipojaribu kuitazama namba ya mpigaji, kioo cha simu kikaonesha namba ya mpigaji imefichwa.

Wazo la kwanza likamwambia Hafsa kwamba mpigaji ni Atu.  Anataka nini?  Ndilo swali lililomjia kichwani mwake.  Hakutaka kuipokea simu hiyo.  Akaingia zake chumbani huku simu ikiendelea kuita kuonesha mpigaji wake hakati tamaa.  Akalivaa koti lake na kurudi pahala alipokuwa ameketi awali.

Simu iliendelea kuita na kuita.  Moyo wa Hafsa haukuwa na amani kabisa juu ya simu hiyo.  Hata hivyo ikafikia akawa hana namna, ikawa kero kwake.  Akaamua kuipokea.

“Haloo!  Habari?”

“Safi tu.  Habari yako Hafsa?”  Hafsa alipoisikia sauti ya upande wa pili wa simu, almanusura aidondoshe simu hiyo chini.  Ni kama wazimu fulani ulimpanda.  Hakuwa na uwezo wa kufikiri kwa nukta chache.  Akajikuta anabwata mithili ya mbwa aliyelengwa vema na shabaha ya mlengaji mwenye siha ya kutosha.

“Nini unachokitaka lakini?  Nini unakitaka mwanaume wewe?  Nini lakini?  Kwanini unanifanyia hivi Ben?  Unajisikia raha eeh? Haya sema sasa unachokitaka kwangu.”

Kabla hajajibiwa, kikasikia kicheko kikali sana kutoka upande wa pili.  Kicheko hicho cha Benito kiliambatana na dhihaka fulani iliyomjaza hofu Hafsa.  Kisha Benito akazungumza kwa sauti ya taratibu.

“Punguza jazba mrembo.  Nadhani haitokuwa vibaya kama utaniambia kuwa umesharudi Dar.”

“Nikueleze ili iweje?  Niache Ben.  Niache na maisha yangu jamani.  Leave me alone please!

Ingawa sauti ya Hafsa ilikuwa ikitoka kwa ukali, Benito akaendelea kuzungumza taratibu.  “Nadhani pia baada ya kunikwepa sana, sasa utakuwa tayari kukutana nami na kuzungumza.”

“Hivi wewe una kichaa?”

 

“Nadhani pia….”

“Nakuuliza we fala umeugua kichaa?”

“Nadhani pia utakubali tuyamalize haya mambo kwa kuzungumza.”

“Ben nisikilize mbwa wewe!  Ulishaninyanyasa sana.  Mwanaume wewe una roho mbaya kama mkaanga sumu.”

“Nadhani tutakapozungumza, tutafikia mwafaka mzuri sana.”  Sauti ya Benito iliendelea kuwa yenye masihara.

“Ben!  Stop it!

“Nadhani pia tutakapoufikia muafaka huo utakuwa umenipa nafasi kuliko ilivyowahi kutokea.”

“Ben!  Jiheshimu tafadhali.  Nitakuporomoshea matusi ya nguoni hutokaa unisahau.”

“Nadhani wakati huo yule fala wako Ali atakuwa akiyalipia yale aliyonifanyia.”

“Mbwa wewe!  Kamtamkie mama yako aliyekuzaa huo upumbavu wako.  Nenda Songea kamwambie mama yako shetani mkubwa wewe!”

“Nadhani utakapokuwa unajaribu kunitukana zaidi utagundua sipo hewani tena.”

“Na ulaaniwe kuliko mashetani wote wa Jehanamu!”  Hafsa alikuwa akiendelea kuongea kwa sauti ya juu mno na yenye kujawa na hasira isiyomithilika.  Akagundua simu imekatwa.  Akashusha pumzi kwa nguvu zote.  Alipoushusha chini mkono uliokuwa na simu, tayari kilio kilikuwa kimemshika.

Akaondoka mahali hapo ili aende chumbani kwake.  Alipokuwa akipita koridoni akakutana na baba yake ana kwa ana.  Mzee Kalinga alimtazama Hafsa kwa makini lakini asitie neno lolote.  Akamwacha Hafsa aingie chumbani kwake.  Mzee Kalinga akiwa chumbani kwake, aliisikia sauti ya Hafsa iliyoonesha dhahiri alikuwa akilumbana na mtu.  Akaamua kupuuzia.  Maneno ya mwisho ya Hafsa ndiyo yaliyomwinua kitandani alipokuwa amejipumzisha ili akaone yaliyojiri.

Hakufahamu ni malumbano kwenye simu.  Alichodhani, Hafsa alikuwa akilumbana na mtu ana kwa ana.  Mzee Kalinga alikwenda hadi nje na kujaribu kutazama huku na kule pasi kumwona yeyote wa kumtilia japo shaka.  Akarudi chumbani kwake na kuendelea kupumzika.

Hafsa alifika chumbani kwake na kujitupa kitandani mzimamzima.  Alikuwa akiendela kulia sana.  Akaanza kulia kwa kwikwi nyingi huku maumivu moyoni kwake yakiongezeka maradufu.  Muda mfupi tu, foronya ya mto wa kulalia ilikuwa chapachapa kwa machozi.  Akalia kwa muda mrefu sana huku akiyafikiria mambo mengi kichwani mwake.

Msichana wao wa kazi, Debora alikuwa amemwona dada yake wakati akiingia ndani huku akilia.  Akajaribu sana kugonga mlango wa chumba chake, hakupata majibu.  Baada ya kusimama mlangoni kwa muda mrefu akaamua kuingia ndani.  Alimkuta Hafsa ameketi kitandani akiwa ameipakata fremu iliyokuwa na picha ya marehemu mama yake huku akiendelea kulia.

“Dada, kwani umepatwa na nini?”

Hafsa alipoisikia sentensi hiyo, akaanza kulia tena kwa  nguvu.  Debora akaenda hadi kabatini.  Akachukua kanga iliyokuwa na maandishi ‘Mungu ndiye mfariji’ ambayo kwa mujibu wa Hafsa mwenyewe, alipewa na shangazi yake wakati wa msiba wa mama yake.  Amekuwa akiitunza sana na kuitumia nyakati moyo wake ujawapo na simanzi.  Akalifunga kabati vema na kurudi kitandani kwa Hafsa.  Akapiga magoti chini na kuanza kumfuta Hafsa machozi kwa kuitumia kanga ile.  Debora hakuzungumza neno lolote.  Taratibu Hafsa akawa anapunguza kulia.

Mara Hafsa akanyamaza.

Hafsa alijihisi kupatwa na nguvu za ajabu.  Debora naye pasipo kuongea akaichukua foronya ya mto na kulitandua shuka.  Akabadilisha foronya na shuka safi kutoka kabatini kwa Hafsa.  Akaondoka zake kimya kimya.  Alipofika nje akaviloweka katika beseni la kufulia.  Akamtayarishia maji ya kuoga.

Hafsa naye, baada ya Debora kutoka aliirudisha ile picha kwenye kabati baada ya kuibusu.  Akaanza kukunja vizuri ile suruali aliyokuwa ameivaa.  Mlango wa chumba chake ukagongwa.  “Karibu.”

“Dada nimekwishakutayarishia maji ya kuoga.”

“Jamani!  Ahsante sana dada Debo.  Usijali dada yangu nakwenda sasa hivi kuoga.  Pia usihofu kuhusu mimi.  Nipo salama.”  Aliongea huku akimtazama Debora.

Debora akatoka chumbani mule akiwa na amani zote.  Hafsa akabaki akiwa amepigwa na bumbuwazi.  Akaendelea kusimama kwa sekunde kadhaa.  Pasipo kujitambua akavikutanisha  viganja vya mikono yake huku akitingisha kichwa kukubali jambo.  Akajikuta ameropoka, “Mapenzi yana nguvu kuliko mauti.”

Akawa amerejea katika hali yake ya kawaida.  Akaoga.  Kisha akaungana na Debora katika kuandaa maakuli ya jioni hiyo.  Si punde, chakula kikawa tayari.

Walipokutana wote mezani kwa ajili ya mlo wa jioni, Hafsa alikuwa katika hali yake ya kawaida.  Mzee Kalinga akatamani kumwuliza jambo kuhusiana na mushikeri uliokuwepo.  Lakini akaamua kuahirisha hadi siku nyingine.  Hakutaka kumfikirisha bintiye jambo ambalo pengine lingeweza kumwumiza.  Baada ya chakula na maongezi mawili matatu ya kifamilia, wakaagana kila mmoja akielekea kujipumzisha chumbani kwake.

Faraja ambayo Hafsa aliipata kutoka kwa Debora ikamfanya adharau kumjulisha Ali.  Akaona hana sababu ya kujipa maumivu kwa ajili ya suala dogo kama hilo.

Siku iliyofuata, Hafsa alikuwa na kipindi kimoja tu cha Historia kwa wanafunzi wake wa kidato cha nne.  Ilipotimu saa nne asubuhi akawa ametoka darasani.  Akabaki ofisini kwake akiendelea kusahihisha zoezi alilokuwa amewapa wanafunzi wake.  Kutingwa huko kulimnyima nafasi ya kuifikiria tena simu ya Benito.  Kuna wakati, mara moja moja, alikuwa akijiwa na jambo hilo.  Mara zote akafanya jitihada ya kulipuuzia kabisa.  Akafanikiwa kulidhibiti jambo hilo lisisafiri zaidi katika ubongo wake.

Simu yake ikaita.

Akapatwa na kigugumizi kuiinua kutoka pale mezani ilipokuwapo.  Ikaita hadi ikakatika.  Akawa anaishika tena kalamu yake ya wino mwekundu ili kuendelea kusahihisha, simu ikaita tena.  Kwa hofu akaitazama namba ya mpigaji.  Akaona ni namba ya simu ya mezani na inaonesha inapigwa kutoka mjini hapo.  Nafsi yake ikapata ahueni kidogo.  Ijapokuwa hakumfahamu mpigaji, akaamua kuipokea.

“Haloo, habari?”

“Safi tu Hafsa.  Jamani mbona hatuonani wakati nasikia umerudi hapa Iringa?”  Ilikuwa ni sauti ya kike, na mpigaji alimchangamkia sana.  Bado Hafsa hakuweza kumtambua mpigaji.

“Kweli nipo Iringa.  Lakini sijakutambua ndugu yangu.”

“Wewe!  Vibaya hivyo Hafsa.  Nimeamini kisichokuwepo machoni na moyoni hakipo.  Mimi ni Johari.”

“Mungu wangu!  Nisamehe bure rafiki yangu.  Vipi mbona kama una mafua?”

“Msimu mama!  Hujui huu ndo msimu wenyewe wa mafua?”

“Pole sana best.  Enhee, niambie lini utakuja kwetu kututembelea?”

“Umeshaanza.  Unapenda sana utembelewe wewe.  Wewe mbona hutembelei wenzako?”

“Yashakuwa hayo?”

“Tusifike mbali.  Upo wapi muda huu?”

“Nipo Mwembetogwa hapa shuleni.  Si unapajua?”

“Nisipajue wakati nd’o ilikuwa njia yangu?  Sasa naomba kuonana nawe.”

“Njoo basi mpenzi.”

“Huko?  Sasa tufanye kitu kimoja.  Mi muda huu nipo hapa stendi, nataka kwenda Mafinga.  Nahitaji sana kukuona mara moja.”

“Mmh!  Nini tena?”  Hafsa alishtuka, maana si kawaida.

“Chonde chonde.  Kuna jambo nataka unishauri.  Nilikuwa nikupigie simu nikasikia upo hapa.  Wewe nd’o nakuamini.  Utanipoteza bure mwenzio.”

“Kwa nini tusishauriane ukirudi?  Kwani warudi lini?”

“Narudi kesho ama keshokutwa.  Please Hafsa, ndilo ninaloendea Mafinga na siwezi kughairi nasubiriwa mimi.  Nisaidie rafiki yangu.”

Hafsa akafikiri kidogo.  Kisha akakubali.  “Ok.  Kwa ajili yako.  Nipe dakika ishirini tu nitakuwa hapo.”

“Poa nakusubiri.”

Simu ikakatwa.  Hafsa akaimalizia karatasi aliyokuwa ameianza.  Akavihifadhi vizuri vitu vilivyokuwepo mezani kwake.

Akawaaga walimu wachache waliokuwemo ofisini humo.  Akaondoka zake.

Alipokuwa akipita usawa wa uwanja wa mpira wa kikapu akakutana na teksi ya dereva anayefahamiana naye sana.  Dereva huyo maarufu kwa jina la Sungura.  Sungura alipomwona Hafsa akasimamisha gari lake.  “Vipi sister, wapi?”

“Nafika stendi hapo mara moja.”

“Twen’zetu.”

Hafsa akaingia ndani ya gari hilo Toyota Mark II  baluni.  Ikawachukua kiasi cha dakika tatu kufika stendi hapo.

Wakati Sungura analipaki gari lake kwenye stendi ya teksi karibu na hoteli ya MR, Hafsa akamwona Johari akiwa kwenye duka la kaseti linalotazamana na MR hoteli.  Hafsa akataka kushuka.  Wakati anafungua mlango, akakiona kitu kilichomfanya aufunge mlango ghafla na kushusha pumzi kwa nguvu.  Alimwona Benito sambamba na Johari dukani humo.  Akashikwa na bumbuwazi kwa dakika nzima.  Akataka kumwomba Sungura ageuze gari na kurudisha nyumbani.

Alipofikiri kidogo akaona bora awe na subira ili kufahamu kinachoendelea.  Akamwomba Sungura amruhusu kuendelea kubaki mumo humo.  Akakubaliwa.

Akawa anaitazama saa yake kila wakati.  Zilipotimu dakika ishirini alizokuwa ameahidi, akamwona Johari akitoka dukani humo na kuvuka barabara hadi MR Hotel.  Akaingia ndani ya kibanda cha simu za kadi za Rafiki.  Akawa anamtazama anavyoitumbukiza kadi yake na kubonyeza namba kadhaa.  Simu yake ilipoanza kuita wala hakuupoteza muda wake.  Akaipokea haraka huku akimwangalia Johari.

“Vipi best, ushafika?”

“Ushanisahau nilivyo mtunza muda?  Nd’o nafika.  Nipo hapa usawa wa kontena la Vodacom.  Kwani we’ upo wapi?”

“Mimi nipo maeneo ya sokoni.”

Uwongo huo!  Hafsa akawaza, kisha akauliza, “sasa mimi nitakuonaje?”

“Wewe nisubiri papo hapo.  Nataka nichukue teksi mara moja nikupitie hapo itukimbize nyumbani fasta nimesahau kitabu changu cha benki.”

Lazima kuna jambo baya linakusudiwa juu yangu, na ndiyo sababu ananidanganya akidhani sijawaona, ndivyo alivyowaza Hafsa kabla hajajibu.  “Ok.  Basi niendelee kupandisha ili tukutane hapo kwenye teksi za MR?”

“Hapana usijisumbue.  Mimi nachukua huku huku.  Nisubiri hapo Kontena.  Dakika moja tu mpenzi.”

“Usijali nasimama hapa nakusubiri.”

“Ahsante.  Nakuja hivyo.”

Simu ikakatwa.  Hafsa akacheka sana.  Badala ya kusikitika ikamlazimu kucheka tena.  Sungura aliyekuwa akiyasikia maongezi huku akimwona mpigaji wa simu akacheka naye.  Akahisi kuna jambo zaidi ya jambo.  Wote wakamtazama Johari akishuka ngazi na kutembea hadi upande wa pili.  Akamshika Benito mkono.  Wakawa wanakuja usawa wa teksi.

Kwa kufuata maelekezo ya Hafsa, Sungura akaiwasha teksi yake kuashiria inaondoka ili kutowapa nafasi Johari na Benito kutaka kuikodi hiyo.  Wao wakaongoza hadi kwenye teksi nyeupe iliyokuwa na vioo vyeusi tupu, maarufu kama tinted.  Joharo akaingia kiti cha mbele huku Benito akiingia nyuma.  Ile teksi ikaondolewa kwa kuizungukia barabara ya Mkwawa.

Hafsa akaizima simu yake.  Akamwambia Sungura ampeleke nyumbani kwake.

Alipofika alioga.  Akapata chakula.  Kisha akaingia chumbani kwake kulala.  Hakupata japo lepe la usingizi.  Aliumiza sana kichwa chake pasipo kupata ufumbuzi wa jambo hilo.  Aliumizwa sana na kitendo cha Johari kumcheza shere.  Baada ya kufikiri sana, akaamua kumfahamisha Ali.

Alipojaribu kuipiga namba ya Ali, haikupatikana.  Jambo hilo si kawaida hata siku moja.  Akaanza kuumiza kichwa tena juu ya masahibu gani Ali atakuwa amekutana nayo.  Akawa anaandamwa na mawazo tele.  Akahisi kuchanganyikiwa zaidi.

Katikati ya mawazo hayo, Atu naye akajitokeza.  Hafsa alimchukia Atu kwa nafsi yake yote tangu siku ya kwanza alipozisikia habari zake.

Kutokana na maelezo aliyokuwa ameyapata kwa Ali kuhusiana na Atu, ni dhahiri Atu anampenda Ali.  Hakuwa tayari kwa hilo.  Kitendo cha simu ya Ali kutopatikana hewani kilimwumiza roho mno kuliko kadhia aliyokutana nayo mjini.  Akaacha kulizingatia tena suala hilo.  Mawazo yake yakawa ni nini kilichomsibu Ali na anafanya nini wakati huo.  Ikafikia hatua akaanza kulia kutokana na maumivu makali ya moyo wake yaliyoambatana na wivu.

Akatamani kuondoka Iringa muda huo huo ili akawe karibu na mumewe.  Akajikuta anamhitaji Ali kwa kiasi kikubwa kuliko kawaida.  Mara simu yake ikaita.  Mlio wa simu ulimfanya akurupuke kuipokea.

“Oooh!  Jamani Ali!  Mwaah!”

“Mambo vip mpenzi?  Samahani mpenzi wangu kama ulinipigia simu ukanikosa.  Niliishiwa chaji nikiwa ofisini halafu kumbe chaja niliiacha nyumbani.  Ikanibidi kwenda kuiweka kibanda cha simu kuichaji.  Nikaizima.  Saa hizi nd’o nimeiwasha mpenzi wangu.  Pole mama.  Ulinitafuta eeh?”

Mbona maelezo mengi bila hata kuulizwa?  Swali lilimjia Hafsa ghafla.  Akataka kuropoka kwa hasira.  Akajishauri kutuliza moyo.  Akajibu kwa taratibu kama kawaida yake aongeapo na Ali.  “Hapana sweetie sikukutafuta.  Mi’ mwenyewe nilitingwa shuleni acha kabisa.”

“Jamani mke wangu unatingwa hadi unashindwa kunitafuta mwenzako?  Utaniua bure mtoto wa mwanamke mwenzio.”

Yamekuwa hayo?  Ana lake jambo.  Hafsa ndivyo alivyowaza.  Akawa mpole, “Nisamehe mume wangu.  Mwenzio nimekukumbuka sana.”

“Usijali mke wangu.  Ujuwe mi’ nakupenda sana.”

Thanks sana.  Nami nakupenda sana laazizi wangu.”

“Mwaah!”

Wow!  Thank you!  Take care huko uliko Ali.”

Yah, I do.

“Nimekumiss sana honey.

“Nimekumiss pia mke wangu.  I love you.”  Sauti nzito ya Ali iliingia masikioni mwa Hafsa mithili ya radi.  Akahisi amepigwa na shoti ya umeme mwili wote.  Akajitupa kitandani na kuukumbatia mto kwa nguvu.  Kwa sauti legevu akaongea, “Ali…”

“Mmh, sema sweetie.

“Mwenzio naomba nitumie basi.”

“Nini?”

“We nitumie tu, usiulize nini jamani.”

“Sasa nitatumaje?”

“Utajua mwenyewe utatumaje.  Mi nataka niipate.”

“Haya nakutumia.”

“Kweli eeh?”

“Mmh!.”

“Haya ahsante. Bye!”  Hafsa alikuwa hoi.

“Mwaaah!”

Ali akakata simu.

…………..itaendelea

Na Fadhy Mtanga

Mtanga ni mtunzi wa kitabu cha riwaya, HUBA anayepatikana Dar es Salaam. Unaweza mfatilia katika mtandao wa Twitter kupitia: @FadhyMtanga na kupata kitabu chako cha HUBA kwa namba: +255 (0)715 599 646

2 Comments

  1. Fadhy Mtanga says:

    Ahsante sana kaka Raphael

  2. Raphael Nyakundi says:

    Kazi nzuri

Leave a Comment