Riwaya ya Kizungumkuti: Sura ya nane

Kizungumkuti

Iringa

Alhamisi, Juni 5, 2003

Hafsa hakuwa na kipindi cha kufundisha darasani.  Akawa ameamua kushinda pale nyumbani.  Asubuhi mnamo wa saa mbili na nusu akapokea ujumbe mfupi kutoka kwa Johari.  Johari alimlaumu kwa kwa kitendo cha kumdanganya siku ya jana yake.  Hafsa hakujisumbua kuujibu huo ujumbe.  Akawa anaendelea na shughuli zake za pale nyumbani.

Saa tatu asubuhi.

Alipomaliza kupata kifungua kinywa akishirikiana na Debora.  Mawazo fulani yaliendelea kukitawala kichwa chake.  Wakati Debora akiwa karoni akiosha vyombo, Hafsa akakichukua kijembe kidogo hadi bustanini kulikokuwa kumepandwa jamii kadhaa za mboga mboga na miti ya matunda.  Bustanini akawa anapalilia matuta ya mboga.  Redio  yake ndogo ikimliwaza kwa muziki laini kutoka katika kaseti iliyokuwa na mchanganyiko wa nyimbo za muziki wa country zilizokuwa zimeitingisha sana dunia.  Sauti nzuri za waimbaji zilizojaa mahaba na mpangilio mzuri wa vyombo wenye kumfanya msikilizaji asahau masahibu yote ya dunia na kuelea katika bahari ya ulimwengu mwingine kabisa.

Huku akiendelea kupalilia na kulimalima matuta hayo, muziki huo ulikuwa ukimkumbusha mapenzi yake na Ali.  Muziki huo ukamfanya amhisi Ali kuwa karibu naye.  Mara kadhaa akawa ananusurika kujichimba na kijembe hicho kidogo maalumu kwa bustani kutokana na kunogewa na muziki huo.  Hakutaka kuyapa nafasi mawazo yenye kumwondolea furaha.

Alipomaliza kulima lima akaanza shughuli nyingine ya kupandikiza miche mipya ya mboga iliyokuwa imewatikwa mumo humo bustanini.  Wakati akiendelea kupandikiza miche hiyo, ujumbe ukaingia kwenye simu yake.  Akanawa maji yaliyokuwa yakimwagika kwenye mpira uliokuwa ukileta maji bustanini hapo kutoka bomba kuu uani.  Akaufungua ujumbe huo na kukuta umetoka kwa Johari akitaka kujua imekuwaje amekuwa kimya akishindwa kujibu ujumbe wake wa awali.  Hafsa akairudisha simu mahali ilipokuwa na kuendelea na kazi yake ya bustani.

 

Saa nne asubuhi.

Ujumbe mwingine tena kutoka kwa Johari ukaingia.  Sasa akawa anamhitaji Hafsa wakutane.  Akamwambia kuwa amekwisharudi kutoka Mafinga anakodai alikwenda tangu jana yake.  Hafsa akajikuta anapandwa na hasira na kuamua kuendelea kutojibu.

Akawa amemaliza shughuli zake za bustani.  Wakati anaibeba redio yake apate kuondoka bustanini hapo, ujumbe mwingine kutoka kwa Johari ukaingia.  Safari hii akawa anataka kufahamu kama yeye Hafsa yupo nyumbani ili aje yeye waongee.  Ulipoingia ujumbe huo, Hafsa akaingia majaribuni na kutaka kuujibu kwa kumwambia yeye hayupo nyumbani.

Akaanza kuuandika hata akamaliza.  Lakini kabla hajautuma, nafsi yake ikasita.  Akajiambia haikosi namna.  Katika kuendelea kuwaza akajikuta akiushtukia mtego.  Hapo akahisi kuwa Johari kauandika ujumbe huo akiwa kweli anahitaji kufahamu mahali alipo.  Na kwa kuwa mara zote tatu za awali hakuwa amejibu, kwa vyovyote ujumbe huu angeujibu.  Kwa kujibu kwake ingekuwa rahisi kwa Benito na Johari kufahamu yupo nyumbani na kufanya lolote wanalolikusudia juu yake.  Akachukua uamuzi wa kuendelea kutojibu.

Akamwita Debora na kumpa maagizo kuwa endapo mtu yeyote atakuja kumwulizia, amjibu kwamba hayupo.

 

Saa tano asubuhi.

Hafsa akawa anatoka bafuni alikoingia baada ya kazi zake za bustanini.  Alipotoka bafuni akakutana tena na ujumbe wa Johari kwenye simu yake.  Johari akamlaumu sana kwa kutojibu ujumbe wake hata mara moja na kumjulisha kinachomsibu hata akawa kimya hivyo.  Kama kawaida hakuujibu ujumbe huo.

Akaingia jikoni na kuanza kuandaa chakula cha mchana.  Akatingwa kupika jikoni huku akijaribu kujenga taswira ya anapokuwa akimpikia mumewe.  Mawazo juu ya Ali yakazidi kukiandama kichwa chake.  Akazidi kuzitamani nyakati za upamoja wao uliosheheni furaha na raha pasi karaha.  Wakati fulani mawazo hayo yalitibuliwa na mawazo juu ya Benito, Atu na sasa mtu mwinge, Johari.

Akiwa katikati ya kukatakata nyanya, ujumbe mwingine ukaingia katika simu yake.  Aliinyanyua haraka haraka kwani sasa alifahamu fika na lazima utakuwa umetoka kwa Johari.  Kama alivyobashiri, ujumbe huo ulitoka kwa Johari.  Na sasa Johari alimwandikia kuwa angemtembelea jioni ya siku hiyo.  Akamsisitiza endapo ana ratiba yoyote ya kutoka, basi asitoke.  Hafsa akatabasamu.  Akaupuuzia ujumbe huo na kuendelea na mapishi yake.

Akatoka hadi uani kumwaga maganda ya nyanya.  Akaikuta ndoo ya kuhifadhia takataka imejaa pomoni.  Akaichukua hadi nje kabisa ambako ghuba la takataka la manispaa liliwekwa.  Akazimwaga takataka na kuondoka kurudi ndani.

Wakati anarudi akawa hana hili wala lile huku akiimba wimbo uitwao ‘mapenzi matamu’ ulioondokea kupendwa na watu  wengi.  Wimbo huo umeimbwa na msanii wa kike Rehema Chalamila almaarufu Ray C.  Mwanamuziki huyo mwenyeji wa mji huo wa Iringa alikuwa ameibuka kwa kasi mwanzoni kabisa mwa mwaka huo.  Hafsa naye akaondokea kuwa shabiki wake mkubwa.

Alipokuwa anauvuka mtaro uliochimbwa pembezoni mwa nyumba yao akashituka ghafla kukutana na Johari ana kwa ana.  Hafsa aliduwaa kwa takribani dakika nzima bila kuzungumza kitu chochote huku akiwa amemtolea macho Johari.  Mapigo yake ya moyo yakaanza kwenda kwa kasi sana.  Hofu tele ikamjaa moyoni huku kichwani akiwa haelewi chochote.  Akahisi miguu yake haina nguvu tena huku akijisikia kizunguzungu. Akajivuta kidogo ili akaegamie ukuta.  Hakufika mbali nguvu zikawa zimemwishia kabisa miguuni mwake.  Akajikuta amekaa chini pasipo kutarajia.  Ndoo yake ikaangukia ndani ya mtaro.

Johari ambaye muda wote huo hakuwa akijua la kufanya alijisikia vibaya sana.  Akajikuta dhamira yake ikimsuta sana.  Akajisikia huruma sana juu ya Hafsa.  Akamsogelea hadi pale alipokuwa ameketi.  Alipomshika tu mkono,  Hafsa akaanza kulia sana.  Akaweka mkono wake wa kulia chini huku amekikunjua kiganja chake ili kiwe egemeo.  Akautumia mkono wake kama nguzo na kujitahidi kuinuka.  Johari akaendelea kusinyaa mithili ya kifaranga cha kuku kilichotandikwa na mvua ya asubuhi.

Alipofanikiwa kuinuka akamwangalia Johari aliyekuwa amemkodoloea macho kama vile mtu aliyeshikwa ugoni.

Wakaangaliana huku machozi yakianza kulengalenga machoni mwa Johari.  Nukta chache tu, yakaanza kudondoka kwa kutengeneza mkondo wa mto mashavuni mwake juu ya lokalia aliyojipaka.  Hafsa akamshika Johari mkono wake wa kulia kwa mkono wake wa kushoto.

“Karibu ndani Johari.”  Johari hakujibu bali akawa natembea sambamba na Hafsa hadi walipofika barazani.  Johari akaketi katika moja ya masofa barazani hapo.  Hafsa akamwomba Johari dakika chache na kurudi pale mtaroni ili kuichukua ndoo ya takataka.   Alipokuwa akiitoa ndoo mtaroni, pia kaiona simu yake.  Ikamwashiria kuwa simu yake naye ilidondokea mtaroni humo.  Alichoshukuru mtaro huo haukuwa na maji.

Akiwa na mawazo yaliyochanganyika na hasira akarudi uani na kuiweka ndoo mahali pake.  Aliporudi barazani akamwona Johari akiwa amejiinamia kuonesha yupo mbali kimawazo.  Hafsa akapita kimya kimya hadi ndani kwenye ukumbi wa chakula.  Akalifungua jokofu na kutoa chupa mbili za soda.

Akazibeba kwenye kisinia kilichokuwa kimenakshiwa kwa urembo wa kupendeza mno.  Akaambatanisha na bilauri mbili ndefu maalumu kwa soda.  Akapita jikoni na kupakua vipande kadhaa vya kuku wa kukaangwa.  Akapakua na makaroni kidogo.  Hupenda kukipika chakula hicho kwani humkumbusha Ali ambaye hukipenda sana.

Alipojiridhisha amepakua kwa kiwango cha kutosha, akaweka na vikorombezo vingine kama nyuma za kulia, vichupa vidogo vilivyokuwa na chumvi na pilipili ya unga, vijiti vya kuchokonolea kwenye meno na sosi ya nyanya itengenezwayo Dabaga mkoani humo humo.  Akawa anaelekea barazani alikomwacha Johari.

 

*********************

 

 

Benito alipotoka shuleni Kamene alirudi moja kwa moja hadi kazini kwake.  Alikuwa akijaribu kupanga mbinu namna ya kumlazimisha Maulid kusema ukweli juu ya kile anachokihitaji kuhusiana na Hafsa.  Pia alihitaji kufahamu mahali anapoishi Hafsa na mumewe.  Zaidi, alihitaji kufahamu ni wapi ambako Ali anapatiakana  kwa urahisi.

Alikuwa amechelewa sana kurudi ofisini.  Alipokuwa anaingia aliliona gari aina ya Toyota Lexus ambalo hutumiwa na mjomba wake ambaye ndiye bosi wake.  Kupaki kwa gari lile kilikuwa ni kiashirio tosha cha uwepo wa mjomba wake eneo hilo.  Hali hiyo ilimkosesha raha kabisa.  Alifahamu kuwa kama hatokuwa na majibu ya kuridhisha, basi angefokewa kama mtoto mdogo kwa kosa la kutokuwepo kazini.

Nguvu zikamwisha zaidi alipokutana na Nassoro aliyemwambia juu ya uwepo wa mjomba wake tangu mapema sana, mara tu alipoondoka.  Wakati Benito akiendelea kuzungumza na Nassoro, msichana mmoja anayefanya kazi hapo kama mtunza kumbukumbu akatoka na kumwita Benito kuwa anahitajika ofisini kwa mkuu wao haraka sana.  Kijasho chembamba kilimtoka Benito.  Akatembea kwa mwendo wa haraka hadi ofisini kwa mkuu wake.

“Shikamoo mzee.”  Benito alisalimia huku akiwa amepoteza uchangamfu wote.  Mzee Ndauka, Mkurugenzi Mtendaji wa Ngoni Constructions Limited alionesha dhahiri hasira yake.  Alimtazama Benito kwa kumkazia macho.  Ndipo, badala ya kujibu salamu, akauliza swali.

“Ulikuwa wapi?”

“Nilienda ofisi za ardhi kufuatilia ramani.”

“Zipo wapi hizo ramani?”  Mzee Ndauka aliongea huku akiendelea kumkazia macho Benito.  Benito akababaika asijue la kujibu.  Mzee Ndauka akafahamu Benito anajaribu tu kumdanganya.  Baada ya kuona Benito ameshikwa na kigugumizi akaendelea kuongea.

“Ok.  Najua unanidanganya.  Nafahamu fika kuwa siku hizi hushindi sana ofisini.  Kama umeanza kuridhika shauri lako.  Kumbuka haya ni maisha mwanangu.  Kuna leo na kesho.  Siipendi hiyo tabia.  Nataka ujirekebishe.  Sawa?

“Sawa nimekuelewa uncle.

“Nilichokuitia hapa ni kwamba, tunatarajia kujenga minara ya simu kwenye maeneo mapya huko mkoani Mbeya.  Kazi iliyo mbele yetu ni kufanya utafiti juu ya maeneo hayo.  Baada ya hapo, kama kawaida tunaingia mikataba na wamiliki.  Sijui unanielewa?”

“Nakuelewa.”

“Maeneo hayo ni Ipinda huko wilayani Kyela na Makongorosi wilayani Chunya.  Mnachopaswa kufanya ni kuangalia maeneo yenye idadi kubwa ya watu.  Ramani kwa ajili ya maeneo hayo zimekwishaandaliwa.

“Mkishayapata maeneo hayo mnazungumza na uongozi wa serikali ngazi za vijiji.  Kwa hiyo, kama ambavyo tumekuwa tukifanya katika maeneo mengine, mtaingia mikataba kwa niaba ya kampuni na wamiliki wa maeneo hayo ili ujenzi uanze mara moja.”

“Tunapaswa kuondoka lini?”

“Lini?  Kesho asubuhi mtaondoka kwa basi wewe, Nassoro na Thomas.  Nawaombeni sana mfanye kazi haraka na kwa ufanisi mkubwa.  Nawategemea kwamba hamtotumia zaidi ya wiki moja kwa kila eneo.”

Benito alinyong’onyea mno.  Baada ya maelekezo kadhaa, akatoka ofisini kwa Mkurugenzi.  Hakuwa na raha kabisa kiasi cha kuwafanya wenzake kudhani amekaripiwa sana kwa utoro kazini.  Wenzake wote wasingekuwa na wazo kuwa taarifa ya safari ndiyo iliyomkosesha raha.  Kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo, habari ya safari ndiyo habari njema kuliko zote.  Safarini hupata posho nyingi mno ambazo huwasaidia sana kuweza kumudu vema gharama mbalimbali zinazowakabili.

Benito hakutarajia kupata safari katika kipindi hicho.  Kwake taarifa ya safari aliihesabu kama taarifa isiyompendeza hata kidogo.  Kuna mambo mengi alikuwa amepanga kuyatekeleza katika kipindi kifupi kijacho.  Aliona kusafiri na kuwa nje ya Dar es Salaam kwa zaidi ya majuma mawili kungemchelewesha ama kumrudisha nyuma kabisa katika kazi ya kuwasaka wabaya wake.

Akaonelea ni akheri kuzikosa posho zote ambazo angelipwa.  Akafanya mpango na mfanyakazi mwenzake ambaye hakuhusishwa safari hiyo ili aende kwa niaba yake.  Mara nyingi wafanyakazi wamekuwa wakifanya hivyo pindi mtu awapo na dharura.  Wakakubaliana vizuri.  Lakini pendekezo la Benito lilipofika ofisini kwa Mkurugenzi lilikataliwa katakata.

“Usiwe mpumbavu Ben.  Nimekupanga wewe kwa sababu maalum.  Kwanini unapenda kuwafaidisha watu wengine?  Unadhani hao wengine sikuwaona?  Utakwenda.  Mimi sipo tayari kumwona mtu mwingine anafaidika halafu mtoto wa dada yangu anakufa njaa.”

“Unajua uncle…”

“Acha mambo yako Ben!  Unajua nini?  Kila siku huwa nakwambia, bila mama yako mimi nisingefika hapa dogo.  Mimi nakwenda shule, nikirudi nakuta amenipikia tayari.  Kipato chake kwa kufanya vibarua  ulinisomesha mimi sekondari.  Halafu wewe leo unaniletea habari gani?”

“Hapana uncle…

“Hapana nini?  Mimi najua kwa nini unakataa safari.  Na ndio sababu hiyo hiyo hushindi ofisini.  Mi’ nakwambia lazima umepata mwanamke anayekuburuza akili yako.  Sasa ngoja nikwambie kitu kimoja.  Kama huyo mwanamke anakupenda kweli, mwambie akuvumilie wiki mbili ukafanye kazi kisha utarudi.  Sawa bwana mdogo?”

“Sawa.”  Hiyo sawa ya Benito ilimtoka bila mwenyewe kuitegemea.  Kwa shingo upande akakubaliana na mjomba wake.

Siku iliyofuata,  Jumamosi asubuhi, Benito akawa ndani ya basi la Scandinavia na wenzake safarini kwenda Kyela.

Alizongwa na mawazo safari nzima.  Akashindwa kabisa kuifurahia safari hiyo.  Bado alisumbuliwa na mawazo ya namna gani ataweza kumkabili Maulid.  Namna atakavyoweza kukutana na Ali na hatimaye kumpata Hafsa.

Ilikuwa ni safari ndefu iliyowachukua kiasi cha masaa kumi na mawili.  Walipowasili mjini Kyela, wenzake walikuwa na furaha tele kufika katika mji huo.  Mji maarufu kwa mchele unaonukia zaidi kuliko wowote nchini.  Hali ya hewa haikuwa na utofauti wowote na Dar se Salaam.  Walipowasili hakukuwa na mvua, lakini hali ilionesha wazi kwamba muda mfupi uliokuwa umepita kulinyesha mvua kubwa sana.  Joto kali lilianza kuwapa maudhi.  Hali hiyo walianza nayo tangu eneo la Stamico, njia panda ya kwenda mgodi wa makaa ya mawe Kiwira.  Eneo hilo kama ambavyo hutenganisha wilaya za Rungwe na Kyela, vivyo hivyo hutenganisha ukanda wa baridi na wa joto.

Wote watatu walikuwa wanafika Kyela kwa mara ya kwanza.  Lakini mawazo yao hayakuwa sawa.  Wakati Nassoro na Thomas walivutiwa na Kyela na watu wake, Benito bado alikuwa mbali.  Wenzake walipendezwa na mandhari ya wilaya ya Kyela, mimea kama migomba, miembe mirefu sana mithili ya milingoti, minazi, mikorosho, michikichi na mikakao.  Mimea hiyo ilileta hali ya kuvutia sana.

Mjini Kyela walivutiwa sana na wingi wa baiskeli barabarani utadhani kila mtu ana yakwake.  Uchangamfu wa wenyeji wa mji huo uliwapa hamasa kubwa sana. Walipochukua vyumba Pattaya Guest House, hawakujilaumu.  Walivutiwa na mazingira masafi na wahudumu wakarimu.  Walichukua nyumba hiyo ya wageni kwani haikuwa mbali kutoka stendi ya Scandinavia na stendi ya kwenda Ipinda kama walivyokuwa wameelekezwa.

Chakula cha jioni wakakipata katika hoteli ya Steak Inn iliyopo barabara ya Posta.  Isipokuwa Benito ambaye mambo yake yaliendelea kumwandama kichwani, wenzake waliufurahia sana mlo wa jioni hiyo.  Ladha ya samaki aina ya Mbasa iliwapa hamu tele ya chakula hicho.  Samaki huyo maji baridi huvuliwa ziwani Nyasa, ni mwenye mafuta mengi na ladha ya kupendeza mno mdomoni mwa mlaji.

Baada ya chakula wakatembeatembea kuzunguka mitaa ya karibu.  Wakapata nyamachoma katika baa ya Mzomozi iliyopo barabara ya Itungi Port.  Wikiendi hiyo iliwafanya wakazi wengi wenye nafasi kuwa nje ya nyumba zao wakiungana na ndugu, jamaa na marafiki katika kupata moja moto moja baridi na mambo mengine.    Kwa maana hiyo maeneo ya starehe yalijaa sana huku vurugu za hapa na pale zikiwepo.

“Mwanangu Kyela kuna watoto, hebu ona pale.”  Thomas alizungumza wakati wakiwa Mzomozi baada ya kuwaona wasichana wanne warembo wakiwa wameketi katika meza ya peke yao.

“Tatizo huku mwanangu nasikia ngwengwe nje nje.”  Nassoro akazungumza ili kumtahadharisha mwenzake kuhusiana na hali ya maambukizo ya UKIMWI katika mji huo.

“Usiniambie mwanangu.  Wewe umejuaje?”

“Tatizo lako Thom hupendi kusoma machapisho yenye kuelimisha.  Wewe kila siku ni mambo ya starehe tu.  Kwa taarifa yako hii ni moja ya wilaya zinazoongoza kwa maambuziki.  Hii place iko so rotten kaka.  Take care mwanangu, mi’ nakujua.”

“Kwa kuwa umesema kaka, mi’ sitafuni mtu.”

“Hilo nd’o ulilosahau kusema.”  Wote wakaangua kicheko kiasi cha kumgutusha Benito aliyekuwa maili alfu lela kimawazo.

Ilipotimu saa sita usiku wakarudi kulala.

Jumapili mchana wakapanda pick-up tayari kwa safari ya kwenda Ipinda.  Mvua kubwa iliyokuwa imenyesha asubuhi iliwachelewesha kuondoka.  Safari ya kwenda Ipinda iliwakera sana kutokana na utelezi mwingi sana njiani.  Walilazimika kushuka mara kwa mara na kutembea umbali fulani kutokana na njia hiyo kuharibiwa sana na mvua za masika.

Walipokuwa wanapita bonde la mpunga hadi Tenende tayari walikuwa wamechafuka vibaya mno kutokana na matope tele.  Utanashati wao wa ujana wa kimjini mjini ulifunikwa vilivyo na hali hiyo.

Pamoja na usumbufu huo mwingi wa njiani, panapo saa tisa unusu waliwasili Ipinda.  Nassoro na Thomas ukiachilia usumbufu wa njiani, walionekana kufurahia mazingira waliyoyakuta.  Eneo hilo ndilo njiani hadi kwenye ufukwe maarufu wa Matema.  Ufukwe huo wa ziwa Nyasa ni moja ya fukwe nzuri za maji baridi duniani.  Upo pembezoni mwa safu za milima ya Livingstone.

Kuanzia Jumatatu vijana hao watatu walifanya kazi kwa juhudi na maarifa makubwa.  Baada ya siku tatu tu, kazi yao ikawa imekwisha.  Ipinda lilionekana eneo zuri sana kuwa na mawasiliano kutokana na idadi ya watu.  Shughuli kubwa ya uchumi ikiwa ni kilimo cha mpunga, michikichi na kakao na hivyo kuwa eneo lenye biashara kwa kiwango kikubwa.  Eneo hilo linazalisha kakao kwa wingi kuliko eneo lolote la ukanda huu wa kusini, kati na mashariki ya Afrika.  Kutokana na umuhimu huo kibiashara, wakazi na viongozi wao hawakuwa na ugumu katika kutoa maeneo.

Nassoro na Thomas waliibaini hali tofauti ya Benito.  Mara kadhaa walijaribu kumdadisi ili kujua kinachomsibu.  Hawakufanikiwa.  La zaidi alilowaeleza, hakupendezwa na eneo hilo.  Ushawishi wao haukumfanya Benito abadilike hali ya moyo wake.  Walifahamu fika kawadanganya.  Wakaamua kumwacha madhali naye ni mtu mzima ajuaye alitendalo.

Waliondoka Ipinda siku ya Ijumaa moja kwa moja hadi Mbeya.  Nassoro na Thomas walipenda kujirusha wikendi mjini Mbeya.  Wamekuwa wakisikia mara nyingi sifa za mji huo kwa upande wa burudani.  Wakataka kujichanganya baada ya kazi nzito.  Benito hakuwa na wazo hilo.  Hivyo hata wenzake walipomshauri kwenda disko ili kustarehesha akili, alikataa na kuamua kubaki hotelini walikokuwa wamefikia.  Alikuwa akitafakari jambo atakalolitenda pindi warudipo Dar es Salaam.

Alfajiri ya siku ya Jumapili ikawashuhudia wakiwa ndani ya Pajero kuu kuu kwa safari ya kwenda Makongorosi wilayani Chunya.  Walipandia gari hilo Mwanjelwa ambako ndiko walikokuwa wamelala katika nyumba ya wageni ya Ntebela iliyopo mkabala na stendi ya Chunya.  Njia nzima baada ya kupita Seventh Day ilitawaliwa na vumbi tele.  Tofauti ya njia hii na waliyoipita kule Ipinda ilikuwa ni moja tu.  Wakati kule waliteswa na matope, huku waliteswa na vumbi.  Zote zilikuwa njia chafu kuliko walizowahi kuzipita awali.

Baada ya kuimaliza Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Kawetere walifika Airpoint.  Hapo ni kilele cha upeo wa mwisho.  Mahali hapo ni barabara iliyo juu zaidi nchini.  Ukisimama hapo unaweza kulionda Bonde la Ufa lote kuanzia bonde la Usangu hadi bonde la ziwa Nyasa pamoja na safu za milima ya Kipengere, Uporoto na Livingstone zilizopo katika mikoa ya Iringa na Mbeya.  Pia unauona mji wote wa Mbeya na vitongoji vyake.  Unaiona Reli ya Uhuru inavyozunguka mithili ya nyoka.  Ni eneo linalokupa hisia za raha kwani unatazama hadi upeo wa mwisho wa macho.  Hilo ndilo pekee lililomfurahisha Benito.

It’s so wonderful.”

Nassoro na Thomas wakatazamana kwanza.  Kutokana na hali ya mwenzao, hawakumtarajia kuvutiwa na eneo hilo.

“Inasisimua kweli.”  Thomas akachangia.

“Nikirudi lazima niandikie makala.”  Nassoro akasema kutoka na kupenda kwake kuandika juu ya mambo yanayomsisimua.

Wakati safari inaendela wakaipita kona kali sana.  Upande mmoja una mlima mkali, na upande mwingine una gema kali sana.  Mama mmoja akawafahamisha hiyo inaitwa kona ya mkoa.  Akasema inaitwa hivyo kutokana na ukali wake na inawaogopesha madereva wote.

Mawazo ya Benito yakahama tena hadi kwenye taamuli nzito kuhusiana na ghasia kichwani mwake.  Hadi wanawasili Chunya, Benito hakuwa na hamu tena na safari hiyo.  Wakanywa chai hapo wakati wakisubiri usafiri mwingine kwa ajili ya kufika Makongorosi.  Kutokana na maelezo ya wenyeji wakati wakinywa chai, ingewagharimu kiasi cha saa moja unusu hadi kufika huko.

Kiasi cha saa sita mchana wakaondoka tena kwa kupanda Toyota Land Cruiser.  Njia hiyo ilikuwa na vumbi zaidi hasa maeneo ya Matundasi ambapo iliwalazimu abiria kuziba pua zao kwa vipande vya nguo.

Mnamo saa saba unusu wakawa ndani ya Makongorosi.  Kama ilivyokuwa kwa Ipinda, wakazi wa Makongorosi walionekana kuwa na uchangamfu sana.  Biashara kubwa waliyoelezwa hapo ni madini ya dhahabu ambayo kimsingi ndiyo yaliyouzaa mji wa Mbeya.  Kitu kilichowashangaza watatu hao, ni umasikini wa eneo hilo tofauti na thamani ya dhahabu.  Miundombinu mibovu, hakuna hospitali wala shule ya sekondari na huduma zingine za jamii si zenye kiwango cha kuridhisha.

“Hili eneo na huko mbele kunakoitwa Lupa Tingatinga ndo kumeuzaa mji wa Mbeya.”  Alianza kuwaeleza mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Lake Tanganyika aliyejitambulisha kwa jina la Juma.

Nassoro akavutiwa.  Akauliza, “Namna gani mheshimiwa?”

Juma, pasi hiyana akamjibu, “Zamani pale Mbeya mjini kulikuwa na pori tu.  Kulikuwa na kakijiji Mbalizi tu.  Sasa Wahindi wakagundua kuna dhahabu kwenye mlima Loleza na huko Lupa.  Wakawa wanakuja huku kuchukua dhahabu.”

“Wahindi hao wakitokea wapi?”  Nassoro akajikuta akiendelea kudadisi.

“Kutoka Dar es Salaam na India.  Basi Wahindi hao wakifika pale ilipo Mbeya sasa wakawa wanaweka mahema pale.” Juma akajibu.

“Kwa hiyo Wahindi ndo wakaleta jina Mbeya?”  Thomas akauliza baada ya kuvutiwa na simuliza ya Juma.

“Hapana, kiasili jina hilo limetokana na neno la Kisafwa Ibheya linalomaanisha chumvi.  Eneo lile pia lilikuwa na chumvi nyingi hivyo wafanyabiashara wengine walikuwa wakija kubadilishana mazao na chumvi.  Mwaka 1927 wakoloni Waingereza wakauanzisha mji rasmi.  Wakashindwa kutamka Ibheya, wakajikuta wakitamka Mbeya.  Hata leo ukiwa Mbeya, eneo la katikati ya mji, tuseme mtaa mkongwe zaidi pale mjini unaitwa Lupa Way.”

“Daah!”  Nassoro na Thomas walishangaa kwa pamoja.  Nassoro akazungumza, “Sijawahi kukutana na mhudumu wa nyumba ya wageni mwenye wingi wa maarifa kama wewe.  Bravo kaka!  Ntakutafuta unisimulie vizuri.”

Benito hakuwa na wazo na mazungumzo hayo.  Akili yake iliwaza mengine.

Siku zilizofuata walifanya kazi kwa kasi kama ilivyokuwa Ipinda.  Jambo walilojifunza wakati wakiendelea na zoezi lao ni biashara kubwa ya ulanguzi wa mafuta.  Biashara hiyo ya magendo hufanywa kati ya vijana wa pale na madereva wa malori makubwa yabebayo tumbaku kutoka Lupa Tingatinga kwenda Mbeya.  Mafuta hayo huuzwa kwa kiasi kikubwa kwenye mabasi yaendayo Singida, Tabora hadi Mwanza.

Walitarajia kurudi Dar es Salaam mapema iwezekanavyo.  Walichoshwa sana na kazi nzito waliyokuwa nayo.  Hata Benito ilimchosha sana.  Akawa aanza kukosa muda wa kuwaza mambo yake.  Maana akifika kitandani alijitupa mzima mzima na kupitiwa na usingizi.  Wakasafiri kupitia njia ya Mkwajuni.  Kutoka Mkwajuni walilazimika kusafiri kiasi cha kilometa sabini kwenye barabara mbovu mno.

Walipofika Mbalizi walikutana na ujumbe katika simu ya mkononi uliowachosha zaidi.  Waliagizwa kutorudi Dar es Salaam bali kusafiri hadi wilayani Mbozi kwa juma jingine kwa ajili ya kazi hiyo.

Wakaenda hadi Vwawa, makao makuu ya wilaya ya Mbozi.

Siku tatu kabla ya kuondoka kurudi Dar es Salaam, Benito aliwaomba wenzake hisani ili aondoke mapema na kuwaacha wao.  Akawaambia ataungana nao Iringa.  Aliwaomba akiwaeleza anahitaji kupita Iringa kwani ana mambo fulani muhimu kwake.  Wenzake wakamkubalia.  Wakamwahidi kumkatia tiketi basi watakalopanda wao ili asipate taabu.

Nassoro na Thomas walipata sasa majibu ya kitendawili kilichokuwa kikiwasumbua muda mrefu.

“Ni demu tu atakuwa amempata ndiye anampa uchizi.”

“Lazima tu.”

…………..itaendelea

Na Fadhy Mtanga

Mtanga ni mtunzi wa kitabu cha riwaya, HUBA anayepatikana Dar es Salaam. Unaweza mfatilia katika mtandao wa Twitter kupitia: @FadhyMtanga na kupata kitabu chako cha HUBA kwa namba: +255 (0)715 599 646

Leave a Comment