Riwaya ya Kizungumkuti: Sura ya Pili-Sehemu ya II

Kizungumkuti 

Dar es Salaam

 Jumatano, Aprili 9, 2003

 

Benito  aliishusha mikono yake chini huku bado akiwa haamini kilichotokea.  Aliiangalia sana ile daladala ilivyokuwa ikiondoka.  Akaichukua simu yake na kuandika namba za ile gari.  Alipandwa na hasira akawa anaung’ata mdomo wake wa chini kwa meno yake ya juu.  Hakuwa na namna ya kumpata Ali.  Hata hivyo akajipa moyo.

Hakuona haja ya kuendelea kuumiza kichwa chake.  Akaanza kutembea taratibu kuifuata barabara hiyo inayokwenda Tabata Mawenzi.  Njia nzima alikuwa akijaribu kumfikiria dada yule aliyemcheza shere wakati akizozana na Ali.  Benito akakosa jawabu la moja kwa moja kama dada yule alikuwa safari moja na Ali ama walikutana mumo humo. 

Kilichomshangaza zaidi ni kuwa muda wote alikuwa akimkazia jicho Ali, hakuona dalili yoyote ya wawili wale kufahamiana.  Hata Ali alipomwongelesha yule dada kwa kumwuliza kituo kilichokuwa kikifuatia, Benito alilisikia vema jibu lililotolewa.  Jibu lile lilimfurahisha sana Benito na kumpa hakika Ali angebabaika katika kushuka hivyo kumwia rahisi kukumbana naye.

Mawazo mengi kichwani mwake yalimsukuma umbali mrefu sana.  Akajikuta amefika Tabata Mawenzi.  Njaa ikawa imemwuma sana.  Akafikiria kwenda mahali kula chakula.  Akaongoza moja kwa moja hadi baa ya Mawenzi Garden akitaraji kula walu chipsi na mishikaki.

Alipokuwa anaikaribia ngazi ya kuingia pale ukumbini ambako sauti za muziki unaopigwa moja kwa moja zilikuwa zikisikika, kwa bahati mbaya akakanyaga maji yenye matope.  Mvua kubwa ilikuwa imenyesha na kuacha madimbwi chungu mbovu.  Benito alikitazama kiatu chake cha mguu wa kulia kilichokuwa kimechafuliwa na matope yale.  Alijisikia udhia mno.  Hamu yote ya kuingia mahali hapo ili kupata chakula ikamwondoka.  

Akageuza njia kwa soni hadi alipovuka barabara.  Akaenda kwenye kijiduka kilichoandikwa Muno Shop. Akanunua chupa ndogo ya maji ya kunywa pamoja na leso ya kitaulo.  Akaketi kwenye fomu nje ya kijiduka kile.  Akakisafisha kiatu chake huku akijawa na aibu tele kana kwamba watu wote wanamstaajaabia yeye.  Haikumgharimu muda mrefu hata akawa amemaliza.  Hakuwa na jambo tena la kumbakiza huko.  Akapanda daladala ya Ubungo ili aweze kufika nyumbani kwake maeneo ya Afrika Sana barabara ya Shekilango.

Benito hakuwa ameoa.  Nyumbani kwake alikuwa akiishi na mdogo wake wa kike, Mary.  Mary alikuwa amemaliza kidato cha nne.  Matokeo yake hayakuwa mazuri sana.  Hivyo alikuwa hapo katika maandalizi ya kurudia mitihani yake.

Benito alipowasili nyumbani alionekana mnyonge sana.  Ingawa alijaribu kadri ya uwezo wake kuficha hali yake, Mary aliweza kugundua haraka utofauti uliokuwepo.  Mary hakuwa akielewa jambo lililomsibu kaka yake.  Kabla hajafanikiwa kumdadisi, tayari Benito alikuwa keshajifungia chumbani kwake.  Alilala hadi jioni sana alipotoka kwa ajili ya kutazama taarifa za habari katika televisheni.  Kila mara Mary alijaribu kutaka kumwuliza kaka yake kilichomsibu.  Kwa hulka yake ya upole ilimuwia vigumu kufanya hivyo.

Baada ya chakula cha jioni Benito aliingia tena chumbani kwake.  Akajitupa kitandani.  Kichwa chake kilizongwa na mawazo tele.  Aliwaza hili na lile ilimradi tu akijaribu kuyatafsiri matukio ya mchana wa siku hiyo.  Suala la Ali kumponyoka katika hali ambayo hakuwa ameitaraji lilimchanganya sana.  Wakati mwingine akawa anatazama kisa haswa.  Kuna wakati akajishauri kuwa ni utoto kufanya hivyo.  Lakini baada ya yote, akili yake bado ikamwambia kuwa ni lazima nadhiri yake itimie.

Pamoja na kwamba hakupafahamu mahali alipokuwa akiishi Ali, akaanza kujipa moyo walau ameupata mwanga kidogo.  Jambo lililomsumbua ni janja gani angeweza kuitumia ili kufanikisha.  Hakufikiria kumshirikisha mtu yeyote.  Hakutaka kumwingiza ama rafiki yake ama mdogo wake, Mary.

Hakuwa mwenyeji sana wa jiji la Dar es Salaam.  Alikuwa na mwaka mmoja tangu ayaanze maisha ndani ya jiji akitokea kwao Songea.  Ugeni wake bado haukumfanya aone ugumu wa kazi ya kumtafuta Ali.  Mawazo hayo yalimfanya kukesha hadi usiku wa manane pasi hata lepe la usingizi.  Hata hivyo, alfajiri ilipokuwa ikibisha hodi, Benito alikuwa amepitiwa na usingizi mzito huku akiwa hajashusha neti wala kubadilii nguo, sembuse kujifunika shuka.

Siku mbili zilizofuata, Benito aliutumia muda wake kufanya kazi za ofisini alikoajiriwa.  Alikuwa akifanya kazi katika kampuni ijishughulishayo na ujenzi wa minara ya simu, Ngoni Constructions Limited.  Kampuni hiyo ilishikilia zabuni nyingi za ujenzi wa minara hiyo.  Yeye alifanya kazi kama mwakilishi wa kampuni jukumu lake kubwa likiwa ni kutafuta, kukodi na kufanya mikataba ya maeneo mapya ambako minara ilikusudiwa kujengwa.

Benito alipokuwa amemaliza kidato cha sita alijiunga na kozi mbalimbali kwa njia ya mtandao.  Alifanikiwa kupata stashahada ya masoko yenye kutambulika kimataifa.  Alipata kazi katika kampuni ya Ngoni kwa sababu ilimilikiwa na mjomba wake.

Siku hizo mbili, Benito hakuwa amefanya kazi zake kwa ufanisi.  Kichwa chake kiliendelea kuwa kizito kupindukia.  Hivyo, ilipotimu siku ya tatu, Benito aliomba ruhusa ya siku nne.  Alidanganya anasafiri hadi Mbeya kumwona mdogo wake wa kiume anayesoma huko.  Hakunyimwa ruhusa kwa sababu ya mambo mawili.  Mosi, si mwombaji ovyo wa ruhusa kazini.  Pili, pengine kubwa zaidi, mtoto wa bosi.

Hakwenda Mbeya kama alivyoaga ofisini.  Joto kali la jiji la Dar es Salaam lilimwunguza huku akikata mitaa ya Tabata Mawenzi hadi Kimanga.  Aliamini Ali kwa vyovyote vile atakuwa akiishi mitaa hiyo ama ya jirani.  Hakuwa akifahamu Ali alijishughulisha na nini, lakini alikuwa na taarifa Hafsa ni mwalimu wa shule ya sekondari maeneo ya Tabata.  Ugeni wake ukijumlisha na ukubwa wa eneo la Tabata pamoja na wingi wa shule za sekondari alitambua wazi ugumu wa jambo hilo.

Akiwa kwenye kituo cha daladala Tabata Kimanga alikutana na wanafunzi wengi.  Kwa kuwa ilikuwa ni majira ya saa nne asubuhi, Benito alielewa wanafunzi hao wapo kwenye mapumziko.  Hakusita, hakupoteza muda akaungana nao na kuanzisha soga.

“Washikaji mambo vipi?”

“Poa!”

“Bomba!”

“Freshi tu!”  Sauti zilisikika kutoka kwa wanafunzi hao.  Walionekana wachangamfu sana.  Ndivyo watoto wa mjini walivyo.  Wanajiamini daima.  Ndivyo alivyofikiri Benito.  Akakumbuka alivyokuwa yeye wakati akisoma shule.  Akawakumbuka rafiki zake aliokuwa nao wakati huo.  Akakitonesha kidonda moyoni mwake ambacho kimegoma kupona miaka yote hiyo.  Akatambua fika kama ataziendekeza kumbukumbu hizo kwa wakati huo basi asingeweza kuzungumza tena na wanafunzi hao.

Akaachana na fikara hizo ili kuendeleza soga.  “Niambieni mabest shule niaje?”

Mwanafunzi mmoja wa kike aliyekuwa ameegemea kibanda cha kupumzikia abiria akajibu, “shule…. shule poa tu kaka!  Si’ unajua ni lazima uikubali nd’o uienjoy!”

Benito akamtazama binti huyo aliyekuwa na rangi asilia nyeusi na macho makubwa yaliyokuwa yakirembua.  Mwenye umbo nene huku akiwa amejaliwa wowowo babkubwa.  Ingawa alikuwa ndani ya sare za shule, bado uzuri wake ulijidhihirisha na kung’aa mbele za watu.  Benito akaachana na hayo na kuendeleza maongezi.

“Shule mnayosoma inaitwaje?”

Mwanafunzi mmoja wa kiume ambaye wakati Benito anawasili ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkubwa huku akiyasherehesha maongezi yake kwa vichekesho na kuwaacha hoi kwa vicheko wasikilizaji, alikuwa na haraka ya kumjibu Benito.  “Kamene High School”

“Ooh!  Ipo wapi sasa?”

“Siyo mbali bro.  Si unaona hiyo kona hapo inayoongoza mkono wa kulia….”  Mwanafunzi huyo sasa akawa anamwelekeza Benito kwa kunyoosha kidole chake cha shahada cha mkono wa kulia.  “Basi unaingia nayo kulia, mbele kidogo unapiga kona kushoto, geti lipo barabarani tu.  Yale majengo yote yanayoonekana nd’o skuli yenyewe.  Bonge la shule!”

“Kumbe hata siyo mbali”

“Yah!”

“Kuna sister mmoja nimesoma naye kitambo, ni mwalimu.  Sijui atakuwa hapa?”

“Mh!  Nani huyo?”

“Sina kumbukumbu nzuri ya jina lake, lakini ni somebody Hashimu.”

“Si’ umesema sister, sasa niaje aitwe Hashimu?”

Kabla Benito hajajibu wala kufikiria ajibu nini, mwanafunzi mwingine wa kike akadakia.”Na wewe nawe!  Unakuwa kama hujui!  Si anaweza akatumia Hashimu kama ubini.?”

Benito akatabasamu, kisha akachangia, “Sawasawa anti.  Hashimu ni jina lake la pili.  La kwanza limenitoka kidogo.”

Mwanafunzi mwingine aliyekuwa akinywa maji ya chupa, aliushusha mkono wake kutoka mdomoni na kuitupa chupa iliyokuwa tupu.  Wakati wenzake wakiangaliana, akapata nafasi ya kulimeza fundo la maji.  Kisha akaongea,  “Siyo Hafsa huyo?  Nyie hamumjui mwalimu Hafsa jina la pili ni Hashimu nd’o maana huwa anaandika HH?  Kwani bro’ huyo unayemzungumzia yukoje?

Benito hakuweza kuyaamini masikio yake.  Ni kweli tangu wakiwa shule Hafsa alipenda kuandika jina lake kwa kifupi HH.  Akataka kujibu haraka kuelezea wajihi wa Hafsa lakini moyo wake ukasita.  Akaona hana haja ya kukurupuka.  Kwa mantiki hiyo, akadanganya.

“Dah!  Unajua ni muda mrefu sana  hata simkumbuki vema.”

“Aggrey!  Kwani ni nani unayemzungumzia wewe?”  Mwanafunzi mwingine akamtupia swali mwenzake.  Aggrey hakusita kujibu.

“Acha wewe!  Unataka kuniambia yule mwalimu wa history wa advanced humnyaki?  Yule anayeongea kwa mapozi.  Mwenye umbo la kirembo rembo.”

“Aah!  Kumbe yule tunamwita Miss Tanzania!

“Sasa nd’o unasema humkamati?”

Benito akatulia tuli akiwashuhudia wanafunzi wale wanavyozinguana.  Hiyo ndiyo kazi iliyompeleka Tabata.  Mambo yanapojiweka kwenye mstari, ana haja gani ya kuwa na papara?  Benito akajipa jawabu kuwa Hafsa anafanya kazi pale.  Akaendelea kutulia huku wanafunzi wakiendelea kumjadili mwalimu wao.

“Kama ni huyo nampata.”

“Sasa huyo nd’o anaitwa Hafsa Hashimu.”

“Kwa hiyo bradha unataka kumwona tukupeleke?”

“Hapana jamani.  Nitamtembelea tu siku nyingine maadamu nimefahamu kuwa yupo.  Leo nimebanwa kidogo na ratiba.”

“Kwa hiyo tumwambiaje?  Yule mwanafunzi mrembo mweusi akauliza.

“Hapana.  Wala msimwambie kitu chochote.  Siku nitakayokuja nataka iwe surprise kwake.  Nawashukuruni sana. Naomba nisiwapotezee muda zaidi.  Wacha niende.”

“Jamani bro, hata jina tu?”  Yule binti akasema.

“Ooh!  Very sorry!  Naitwa James.”

Akawadanganya jina lake akiwa na sababu yake ya msingi.  Akawaaga na kuvuka upande wa pili kwa minajili ya kupanda daladala madhali kazi yake imeleta mafanikio.  Wakati akiondoka akawasikia wanafunzi wale wakijadiliana.  Alibahatika kusikia sentensi chache.

“Lakini mbona mwalimu Hafsa ameolewa?”

“Si ndiyo hapo!”

“Msiwe mafala nyie!  Kwani kuolewa kitu gani?”

Akawa ndani ya daladala.  Dereva na utingo wake waliporidhika, wakaondoa gari.  Ndani ya gari kukiwa na Benito aliyezama kwenye lindi la mawazo.  Akijaribu kukokotoa hesabu kadha wa kadha kwa kanuni alizozijua yeye mwenyewe. 

Lakini akawa na faraja sasa.

Akawa amepata jibu.

Atajua la kufanya.

Atafanya tu.

Ndivyo alivyowaza.

…………..itaendelea

Na Fadhy Mtanga

Mtanga ni mwandishi wa riwaya anayepatikana Dar es Salaam. Unaweza mfatilia katika mtandao wa Twitter kupitia: @FadhyMtanga 

Leave a Comment