Riwaya ya Kizungumkuti: Sura tatu

KizungumkutiDar es Salaam

Jumatano, Aprili 9, 2003

 

 

“Nami nafurahi sana kukutana nawe.”

“Dah!  Hata siamini!”

“Ndivyo hivyo Ali, kwa bahati mbaya tumekutana wakati mbaya.”

“Hapana Atu, ni kama muujiza kukutana nawe leo.”

“Wakati wote mwujiza humaanishwa kuwatokea watu katika wakati na hali wasiyoitaraji.”

“Leo nimeamini hilo.  Sijui hata nikushukuruje!”

Ali sasa akawa amerejewa na amani moyoni mwake.  Akamwita mhudumu na kuagiza bia ya Safari.  Ingawa alikuwa tayari amemkumbuka Atu na mahali walipowahi kuonana, bado shauku yake ilikuwa ni kufahamu ni namna gani Atu aliweza kutokea ndani ya daladala ile na kumnusuru.  Kiu yake ilikuwa ni kufahamu mengi ambayo pengine hakuyafahamu.  Baada ya mhudumu kuileta bia yake Ali akaendeleza maongezi. “Atu nifahamishe basi.” 

“Inategemeana na wewe unataka kufahamu nini.”

“Kwa ufupi, napenda kufahamu ilikuwaje kuwaje hadi tukawa ndani ya daladala moja.”

“Aaah!  Unanipa raha Ali.”  Atu akamtazama Ali kwa jicho la huba.  Ali akayakwepesha macho yake haraka.  Hata hivyo, bila shaka ujumbe ulikuwa umemfikia.  Atu akanywa fundo moja.  Akajipa muda wa kumeza fundo hilo.

“Unajua nini Ali?  Ni kama bahati.  Nadhani Mungu wako anakupenda sana na akapanga iwe hivyo.  Mimi sikuwa na ratiba ya kufika Mnazi Mmoja kabisa.  Kuna rafiki yangu ambaye ni nesi pale ndiye aliyenipigia simu niende kumwona.  Amerudi kutoka likizo juzi.  Sikuwa nimeonana na shosti wangu huyo mwezi mzima akiwa Moshi kwa wakweze.  Baada ya kupiga naye stori nyingi nikawa naelekea pale kituoni ili nipande zangu daladala kurudi kwangu.  Tupo pamoja?”

“Yap!  Huniachi nyuma hata kidogo.”

“Unaona sasa?  Ni kama Mungu tu alipanga.  Wakati nakaribia pale kituoni nilikuona.  Basi nikawa nakuja usawa wako ili nikusabahi.  Ile nakaribia tu, ndiyo yule jamaa yako akakukwida.  Huwezi kuamini, nilijisikia vibaya kuliko ninavyoweza kueleza.  Niliumia mno.”  Atu akaongea kwa hisia kali.  Ali alitulia tuli mithili ya maji ya mtungini huku akifikiria mambo mawili matatu kichwani mwake huku akisikiliza.  Alishaisahau hata bia mezani pale.

“Unasikia Ali?”  Ali akatingisha kichwa kuashiria wapo sambamba.  “Nikasogea hadi pale mlipokuwa.  Nikawa mmoja wa watu waliokuwa wanawatazama kwa karibu.  Uliporeact kwa kujiamini moyo wangu ukatulia kiasi.  Nikaendelea kuwa nyuma ya kila hatua uliyoichukua.  Nilipokuwa naketi tu ndani ya ile daladala pembeni yako, nikamwona Benito naye akiingia.

“Nikajifanya nipo busy na simu ili tu wewe usipate nafasi ya kuanzisha stori nami katika kutafutasymphathy.  Nilitambua fika kwa hali ya kuchanganyikiwa uliyokuwa nayo, lazima ungetaka kujihami.  Na kama ungefanikiwa hilo pengine ungenikumbuka kwa urahisi.  Na ungenikumbuka, najua ungechachawa katika kutafuta upenyo.”

“Na nilipokuuliza kituo kinachofuatia, kwa nini ulinijibu kavukavu vile?”

“Subiri Ali.  Nitafika kote huko.  Nilipokujibu vile nilikuwa na sababu mbili.  Kwanza, kama nilivyosema awali, sikutaka upate muda wa kunikumbuka.  Pili, nilijua endapo ningekufahamisha jina la kituo kama ulivyohitaji, lazima ungekurupuka kutaka kushuka.  Nilifahamu Benito alikuwemo ndani ya daladala kwa ajili yako.  Hivyo kama nisingekuwa makini, pengine siku moja ningejilaumu kwa kushindwa kukunusuru na zahama iliyokuwa mbele yako.”  Alipofika hapo, Atu akashusha pumzi kidogo.  Akanywa bia yake kidogo jambo lililomkumbusha Ali.  Naye pia akanyanyua bia yake na kupiga pafu moja refu. 

“Atu, nashindwa hata nisemeje!”

“Subiri kijana, acha upesi.  Bado sijamaliza somo.”

“Ok!  Lakini kabla hujaendelea tafadhali niruhusu nikuulize swali.”

“Yes.  Uliza.”

“Kwa hiyo hukutaka nishuke ukiwa na hakika ungenisevu kwa mtindo ule?”

No Ali!  Haki ya Mungu sikuwa nafahamu ningefanyaje kukusevu.  Nilikuwa nikiumiza kichwa changu safari nzima.  Hadi daladala inafika mwisho wa safari sikuwa nimepata suluhisho.  Muda ule namsihi Benito apunguze munkari ndipo alipocheza faulo mwenyewe.  Majibu yake yalikasirisha zaidi.”

“Ndipo ikawaje?”  Ali bado alikuwa na shauku kubwa ya kuyafahamu mambo yale.

“Anhaa!  Nilipokuwa namlipa nauli kondakta wazo likanijia kichwani.  Nikajaribu kuongea na konda akakubali.  Akaenda kwa dereva wake, wakakubaliana.”

“Ndiyo ukaamua kutudatisha kuwa tumekutukana?”

“Hujatulia wewe!  Wewe ulidhani mie ningefanyaje?  Hata hivyo huoni kuwa ni janja iliyosaidia?”

“Ni kweli Atu.  Nikiwa mkweli mbele zake Mungu, nashindwa nitoe shukrani zangu kwa namna gani.”  Ali akawa anaingiza mkono wake kwenye mfuko wa nyuma wa suruali yake.  Akatoa waleti yake ndogo na kuanza kuchomoa noti kadhaa za fedha.  Hakuwa amefika mbali kabla hajashitukiwa na Atu.

“Unafanya nini Ali?”

“Mh, nothing!

Be honest Ali.  Unafanya nini?”

“Tulia basi nimalize ndipo ujuwe nilikuwa nafanya nini.”

”Sikiliza rafiki yangu.  Naelewa unataka kufanya kitu gani.  Kama unakusudia kunirudishia pesa, utanikwaza.  Mimi ndiye nilyekuleta hapa.  Gharama zote ni jukumu langu.  Tumeelewana?”

“Ahsante sana Atu.”

Wakapeana michapo mbalimbali huku wakiendelea na vinywaji taratibu.  Kumbe Atu alikuwa amehamishiwa Dar es Salaam kikazi katika kituo cha polisi Chang’ombe.  Ali naye akamfahamisha Atu kuwa anajishughulisha na biashara.  Ali hakusahau kumweleza Atu juu ya mke wake ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari ya Kamene iliyopo Tabata Kimanga.

Muda nao ukawatupa mkono.  Wakaagana kwa miadi ya kukutana wakati mwingine.  Wakapeana namba za simu.  Wakaelekezana mahali walipokuwa wakiishi.

Ali alipowasili nyumbani kwake, tayari mke wake alisharudi baada ya kazi.  Akili ya Ali haikutulia mara tu baada ya kuagana na Atu.  Alifikiri sana juu ya Benito.   Hakuona umuhimu wa uhasama huo.  Hakuona mantiki yoyote.  Hata hivyo alikuwa na wakati mgumu kujaribu kukisia ni hatua gani zaidi ambayo Benito angetembea.  Akajitahidi kutolizungumza jambo hilo kwa mkewe mapema.  Akamwacha amalize ratiba zake za shughuli za nyumbani.

Usiku wakiwa kitandani tayari kwa kulala ndipo Ali alipomsimulia mke wake habari yote kuhusiana na yaliyojiri siku hiyo.  Alisimulia kwa tuo, kwa sauti hafifu ambayo ilidhihirisha wazi hofu yake.  Alipokuwa akimaliza tayari mke wake alikuwa amekwishadondosha machozi mengi.  Ali akajivuta na kumkumbatia mke wake.  Akampiga busu kwenye paji la uso wake.

“Hafsa mpenzi, usilie mama.  Kwani nimefanya vibaya kukwambia?”

“Ha…. ha……. hapana.”

“Basi usilie mke wangu mpenzi.  Wewe uwapo nami jisikie amani.  Mimi nakupenda wewe nawe wanipenda mimi hofu yako ni ya nini?  Jikaze mpenzi.  Benito hana la kutufanya.  Amini hivyo kidani cha moyo wangu.”

Ni kama Ali alikuwa akimliza zaidi Hafsa.  Akaacha kumbembeleza isipokuwa akawa anampapasa mwilini taratibu.  Ni mkewe.  Alimfahamu vizuri sana.  Muda mfupi baadaye Hafsa akawa anaogelea kwenye bahari ya mahaba.

Maisha yao yakaendelea kama kawaida.  Hafsa shuleni kwake na Ali dukani kwake.  Kila mmoja akijitahidi kumfanya mwenzake asahau kabisa habari yoyote kuhusiana na Benito.  Hakuna aliyekuwa tayari kumwona kipenzi cha moyo wake akiumia zaidi.

Baada ya siku tatu, majira ya jioni, Ali aliingia nyumbani akitokea kwenye moja ya shughuli zake za biashara.  Alimkuta mkewe barazani akiwa ameegamia ukuta.  Ali alihisi kuna jambo lisilo la kawaida.  Alipomkaribia mkewe alimkumbatia kwa upendo kama ilivyo desturi yao.  Akampa busu zito mdomoni kiasi cha kumfanya ashushe pumzi zake kwa nguvu na kusahau masahibu yake.

“Nakupenda sana mume wangu.”

“Nakupenda pia Hafsa wangu.”

Wakaingia ndani wakiwa wameshikana viuno.  Mapenzi bwana!  Wapendanao kwa vituko huwawezi.  Ali na Hafsa walipoingia chumbani walikuwa bado wameshikana viuno.  Mara wajigonge kwenye viti wanapotembea.  Mara Hafsa amtekenye Ali kidogo ilimradi iwe burudani raha mustarehe!  Mule chumbani vituko viliongezeka maradufu.  Kurushiana midoli iliyokuwemo chumbani mwao.  Mara kurushiana nguo.  Huyu akachojoa sarawili yake na kumrushia mwenzake.  Huyu akaichojoa shimizi yake na kumrushia mwenzake.  Sasa wakawa wanakimbizana na kupigana chenga kama wapo mpirani vile.  Ikawa huku.  Ikawa kule.  Ikawa hapa.  Ikawa pale hata Ali akamzidi ujanja Hafsa na kumdaka.  Akamtupia kitandani.  Naye akafuatia.

“Ngoja nikupe mchapo sweetie.”  Hafsa alianza kuongea wakati akijivuta pembeni ya mwili wa Ali.

“Hafsa mwenzio nimechoka.  Twende kwanza bafuni tukaoge nd’o utanipa huo mchapo.”

“Haya twende basi tukaoge.”

“Nibebe basi.”

“Mwili huo!  Mi’ nimeshakubeba sana.  Saa hizi zamu yako kunibeba mimi.”

Wakaoga.

Wakawa mezani kwa chakula.

“Basi rafiki yangu, Benito leo kaja kunitafuta.”

“Wacha weh!”

“Nd’o hivyo honey.

“Umeonana naye?”

“Wala.  Ameishia pale kituoni.  Akawakuta wanafunzi wakiwa break.  Akajifanya kuulizia ulizia kana kwamba kanisahau hata jina la kwanza.”

“Enhee!  Ikawaje?

“Wanafunzi wakamweleza ni kweli nipo.  Walipomwuliza wanifikishie ujumbe gani, unajua kawajibuje?”

“Enhee?”

“Eti wauchune ili siku atakayokuja iwe surprise.

“Itakuwa surprise kweli.”

“Sasa unanitisha?”

“Usifike huko mpenzi.  Ni nani kakufikishia stori hiyo?”

“Kuna mtoto mmoja machepele ile mbaya anaitwa Lydia.  Mwenzangu, eti kawadanganya kuwa anaitwa James.”

“Usiogope laazizi wangu.  Siku akija, wala usikubali kutoka nje ya geti la shule.  Akitaka azungumze nawe mkiwa ndani.  Ukitoka nje anaweza hata kukudhuru kwa urahisi.  Si unamjua mtu mwenye alivyo mwehu utadhani akili zake kashikiwa na mtu mwingine.  Lakini pia jambo hilo lisisumbue sana akila yako.”

“Wewe unadhani ni rahisi akili yangu kutosumbuliwa?”

“Sidhani hivyo.  Bali kuwa strong.

…………..itaendelea

Na Fadhy Mtanga

Mtanga ni mwandishi wa riwaya anayepatikana Dar es Salaam. Unaweza mfatilia katika mtandao wa Twitter kupitia: @FadhyMtanga 

Leave a Comment