Riwaya ya Kizungumkuti: Sura nne

KizungumkutiDar es Salaam

Jumatatu, Mei 5, 2003

 

 

Ndiyo kwanza wanafunzi wa kidato cha sita walikuwa wametoka kwenye mtihani wao wa kwanza ambao ulikuwa ni General Studies .  Ilikuwa ni dakika kadhaa zimeondoka baada ya saa tano kamili ya asubuhi hiyo.  Hali ya hewa haikuwa mbaya sana.  Manyunyu kiasi yalisaidia kidogo kupunguza joto la jiji la Dar es Salaam.  Wanafunzi wengi waliotoka kwenye mitihani walisimama katika makundi madogo madogo wakijaribu kujadiliana hili na lile kuhusiana na mitihani yao hiyo.

Pembeni kidogo nje ya geti la kuingilia shuleni hapo ikapaki  gari ndogo iliyokuwa na rangi nyeupe iliyofubaa kidogo.  Dereva wa gari hiyo aina ya Toyota Camry alitoka nje na kurekebisha kidogo mkanda wa suruali yake kabla hajamwita mwanafunzi mmojawapo kati ya wengi waliokuwa katika eneo hilo.  Alipotowa sauti kumwita mwanafunzi, wote walibaki kutazamana kwa sekunde chache hadi mmojawapo alipojitokeza na kuelekea kule ambako gari ilipaki na dereva wake kusimama nje yake akiwa ameliegamia.

“Mambo vipi best?.”  Mtu huyo aliyekuwa kavalia kinadhifu alianza kwa kumjulia hali mwanafunzi huyo.  Alivalia suruali maridadi ya rangi nyeusi huku ikiwa na drafti za rangi nyeupe zilizojificha kwa mbali kiasi cha kumhitaji mtu kuwa karibu zaidi ili kuweza kuzibaini.  Mkanda wa suruali ulikuwa ni wa ngozi nyeusi ukiwa na chuma cha rangi ya fedha kikiwa na alama ya herufi B kwenye sehemu yake ya kufungia.  Shati lake lilikuwa ni jeupe linalong’aa huku nalo likiwa na drafti za rangi nyeusi hafifu.  Likiwa limesindikizwa vema na tai fupi nene ya rangi nyeusi pia ikiwa imelegezwa kiasi eneo la shingoni.  Unadhifu wa mtu huyo ulikolezwa sawia na jozi nyeusi ya viatu vilivyochongoka kwa mbele.

“Safi tu bro.  Shikamoo.”

“Ok. Fine!  Samahani kwa kukusumbua.”

“Usijali bro bila samahani.”

“Yah, eti kuna mwalimu hapa wa kike anaitwa Hafsa Hashim?”

“Ndiyo yupo.”

“Na sijui nitaweza kumpata vipi?”

“Dah!  Unajua nini bro?  Watu wapo katika paper sasa walimu kibao hawajatokea shuleni”

“Ok.  Samahani kwa usumbufu mdogo wangu.  Utajali kama utakwenda labda ofisini uweze kupata uhakika kama yupo ama lah?”

“Haina shida bro.  Dakika chache tu.”

“Ahsante sana.”

Sidhani kama mwanafunzi huyo aliisikia hiyo ahsante sana.  Alipokuwa amepotelea kwenye viunga vya miti ndani ya shule hiyo, jamaa huyo pale nje aliendelea kuegamia gari lake na sasa akaingiza mkono mfukoni na kuutoa ufunguo wa gari na kuanza kuuchezea kwa kuuzungusha kwenye kidole cha shahada cha mkono wake wa kushoto.  Wakati zoezi hilo likiwa ndiyo linaanza kumnogea, yule mwanafunzi akawa anakuja huku akitembea kwa kudunda.  Jamaa huyo akawa anamtazama kwa chati sana kama vile ana kitu anachojaribu kukijenga kichwani.

“Hayupo bro.

“Ooh!  Bahati mbaya sana.  Sijui labda unapafahamu mahali anapoishi?”

“Hapana kaka.”

“Ok.  Mbona ulipokwenda kumtafuta umechukua muda mrefu?”

Swali hilo lilimshitua kidogo mwanafunzi huyo.  Hakuwa amelitarajia kama lingeulizwa kwake, kwa hiyo hata hakuwa walau ameisumbua akili yake kutengeneza jawabu la kujihami.

“Ok usijali.  Mimi ninaitwa Benito, sijui mwenzangu waitwa nani?”

“Mimi naitwa Maulid.”

“Upo kwenye mitihani siyo?”

“Hapana.  Mi’ bado nipo kidato cha tano.”

“Sasa bwana mdogo ninahitaji unisaidie jambo moja.”

“Sawa hakuna tatizo.”

“Sijui una simu ya mkononi?”

Maulid akasita kidogo kujibu.  Akafikiri haraka kisha akajibu, “Hapana bro

“Ok.  Sasa mimi nakupa namba yangu.  Ila ninachokuomba ni kwamba, siku mwalimu Hafsa atakapokuwa yupo hapa  tafadhali nenda kibanda cha simu hapo”  Benito akaunyosha mkono wake ili kumwonesha Maulid kibanda cha simu kilichokuwa kikitazamana na lango la kuingilia shuleni hapo.  “Nenda hapo unipigie simu.”  Lakini mawazo ya Maulid hayakuwa yakiyazingatia maelekezo hayo bali yalikuwa tayari yakielea kwenye bahari nyingine tofauti kabisa.  Benito alipoona Maulid hajajibu neno lolote, akaendelea.

“Nahitaji sana msaada wako mdogo wangu Maulid.”

“Basi bradha, kwanini usiache ujumbe wako pale mapokezi?”

No.  Unajua nini?  Namhitaji Hafsa na siyo mapokezi.  Pia naepuka mlolongo mrefu katika kuelezea shida yangu kwake.  Tupo pamoja?’

“Hapana.”

Benito akatabasamu kidogo, kisha akaongea.  “Listen my young bro, nahitaji sana msaada wako.  Lakini pia ni jukumu lako kuamua kunisaidia ama lah.”

“Naweza kukusaidia.  Lakini siyo dhambi nikibainisha hisia zangu.  Unanipa mtihani mgumu sana bradha.”

“Kwanini?”

“Staili uliyomuulizia na pia maagizo unayonipa yananiacha na lundo la maswali kichwani.”

My God!  Niamini mdogo wangu.”

“Yah, naweza kukuamini.  Lakini bado napata wasiwasi.  Kwani wamtafutia nini?”

“Ahaa, Kumbe ndicho!  Usikonde kabisa.  Unajua unapokutana na mtu kwa mara ya kwanza, huwezi anza kumweeleza kila kitu unachokifahamu duniani.  Kadiri ya mazoea baina yenu yanavyokuwa, hata ufahamu juu ya kila mmoja wenu nao unakuwa.  Nataka kusema nini?  Jinsi tutakavyokuwa tukizoeana ndivyo utayafahamu mambo mengi.”

Sure?’

“Hakika kweli.  Enhee, hujanijibu kama utanisaidia ama hapana.”

“Nitakusaidia.”  Maulid alitoa jibu ambalo hata hivyo hakuwa na hakika nalo.

“Kitu kingine, pamoja na kukuhitaji kunijulisha pindi mwalimu awapo hapa, pia ninakuomba uyafanye haya maongezi yetu kutojulikana kwa mtu yeyote zaidi yetu siye wawili.”

“Hilo, usitie shaka.”

Benito aliufungua mlango wa gari lake na kuingia kisha akatoa kadi yake ya biashara na noti ya shilingi elfu tano na kumpatia Maulid.

“Kuna namba yangu humo.  Pesa utaitumia kunipigia.”

“Shukrani sana.”

“Tunza ahadi.”

“Usijali bro.

Benito akaliwasha gari lake na kuondoka kwa mwendo wa wastani huku akipunga mkono wake wa kulia kumuaga Maulid.  Maulid alikimbia kiasi hadi kwenye kona ya ukuta wa shule ili apate kulishuhudia gari hilo likipotea kwenye njia inayoingia kituo cha daladala cha Tabata Kimanga.

Wakati Maulid akiwa ndiyo anaanza kuondoka kurudi tena mahali alipokuwa, simu yake ikaita kuashiria ujumbe umeingia.  Alipoufungua kuusoma, alikutana na ujumbe kutoka kwa mwalimu Hafsa ukimjulisha kuwa ameondoka kwenda nyumbani na kumtaka Maulid amfuate huko pindi atokapo shuleni.

 

 

*********************

 

Hafsa alikuwa ameliona lile gari la Benito wakati linapaki pale.  Alijikuta tu kuvutiwa kuendelea kulitazama.  Alipotoka dereva wake, Hafsa alishituka kumwona Benito.  Japokuwa hakuwa amemwona kwa miaka kadhaa sasa, alikuwa na hakika ndiye kutokana na habari zake alizokuwa amekwisha zipata siku si nyingi.  Hafsa alijikuta anaishiwa nguvu ghafla, asijue la kufanya.  Yeye alidhani kuwa Benito angeingia ndani na kumuulizia kwenye utawala.  Akaanza kupanga namna ya kumkabili itakapotokea hivyo.  Hata hivyo akawa katika wakati mgumu sana.

Alipomwona Benito anamwita mwanafunzi walau hofu ikampungua kidogo.  Wanafunzi walipokuwa wakisita kwenda kwa Benito bado jicho lake lilikuwa kwao.  Maulid alipojitokeza, alizishusha pumzi zake kwa nguvu kumshukuru Mungu.  Alichokifanya ni kuendelea kubana kwenye kona aliyokuwepo.  Maulid alipopita, akamwita.

“Enhee, niambie dogo, yule jamaa alokuita amesemaje?”

Maulid akamsimulia mwalimu Hafsa maongezi yake na Benito.  Hafsa akautumia muda huo mchache kufanya mpango na Maulid ili kumfanya Benito afahamu kwamba mwalimu huyo hayupo shule kwa siku hiyo.

Hafsa na Maulid hawakuwa na undugu hata kidogo bali walikuwa wamefahamiana kwa muda mrefu kabla.  Walipata kuishi pamoja huko Iringa wakati baba yake Maulid akiwa meneja wa kampuni ya biashara ya mkoa (RTC) wakati huo.  Baada ya baba yake Maulid kufariki dunia miaka sita iliyopita, alienda kuishi na dada yake aitwaye Zuhura afanyaye kazi shirika la umeme (TANESCO) makao makuu Ubungo kama karani wa mahesabu.

Mwalimu Hafsa hakuwa na muda mrefu tangu afike hapo Kamene High School kama mwalimu wa somo la Historia.  Alipofika akamkuta Maulid akiwa ndiyo kwanza ameanza masomo ya kidato cha tano.  Wakazoeana kama mtu na dada  yake kiasi kwamba mtu mwingine ingemuwia vigumu kufahamu kwamba hawakuzaliwa tumbo moja.

Ukaribu wao ukamfanya Maulid kuanza kuchukua tahadhari pale mtu asiyemfahamu halafu akiwa katika hali isiyotafsirika vema alipomuulizia mwalimu Hafsa.  Hakuwa anafahamu sababu ya Benito kumtafuta dada yake kwa kukamia hivyo, bali alijihisi kama anapaswa kuchukua hadhari mapema ili kumkinga dada yake endapo jambo lolote baya litakuwa linakusudiwa kumfikia.  Baada ya kuwa mwalimu Hafsa amemsihi Maulid ahakikishe kwamba Benito anaamini kutokuwapo kwake pale shule, Maulid alikuwa ameamua kuhakikisha kwamba mgeni huyo ameondoka kabisa eneo hilo.

Maulid alipohakikisha Benito ameondoka zake alikusudia kurudi pale alipokuwa amemwacha mwalimu Hafsa.  Alipoupata ujumbe wa simu kwamba amfuate nyumbani baada ya masomo, hakuwa na hamu ya kuendelea na ratiba ya shule.  Aliwaaga wanafunzi wenzake akiwaambia kwamba hajisikii vema hivyo anahitaji kurudi nyumbani mapema ili apate wasaa wa kupumzika kiasi cha kutosha.

Hakutaka kupandia daladala papo hapo shuleni kwa kuwa huwa zinapita zikiwa tayari zimejaza abiria.  Akaamua kutembea hadi pale kituoni Tabata Kimanga.  Wakati anavuka barabara kuelekea upande wa pili zinakopaki daladala za Kisukulu, aliliona gari dogo linalofanana na lile alilokuwa amekuja nalo Benito.  Lakini hakulizingatia akijiaminisha kwamba Benito aliendelea na safari zake moja kwa moja.  Pia hakushughulisha nalo kwani hakuwa hata amezikariri namba za gari la Benito.

Aliongoza hadi kwenye daladala iliyokuwa imepaki hapo kituoni.  Hakuwa amezingatia walau kutazama nyuma.  Wakati akiwa anaketi kitini alistaajabu kumwona Benito akiwa amesimama mlangoni pa daladala hiyo.

“Ooh Maulid!  Nikusumbue tena.”

Maulid alitahayari asijue hata azungumze nini. Kengele ya tahadhari ikaanza kugonga kichwani mwake.  Benito aliendelea kumtazama Maulid kwa jicho la kirafiki lenye chembe nyingi za huruma.  Alipoona Maulid anashindwa aongee nini, akapata nguvu ya kuzungumza.

“Aaaah!  Nakuomba ushuke garini tuzungumze kidogo.”

Tayari mapigo ya moyo ya Maulid yalikwishaanza kwenda kasi.  Maulid akatazama pande zote za pembeni kana kwamba anamtaraji mtu kumpa msaada.  Hofu ilitanda moyoni mwake, akahisi kwamba ameingizwa mtegoni mwa watu hawa wawili. Akapiga moyo wake konde na kuteremka kutoka katika daladala hiyo  akamfuata Benito hadi kwenye kiduka kidogo alikokuwa amelipaki gari lake.

“Vipi rafiki yangu, unarudi nyumbani?”  Ndivyo alivyoanza Benito baada ya Maulid kuketi.

“Ndiyo.”

“Kwani unaishi wapi?”

“Tabata Mawenzi.”

“Mbona unapanda daladala za huko Migombani?”

“Mmh!  Huko namfuata rafiki yangu mara moja then nd’o narudi nyumbani.”

“Je, ni muhimu kumfuata huyo rafiki yako leo?  Na pengine muda huu?”

Maulid akasita kidogo, hakufahamu kusudio la swali hilo.  Akafikiri kidogo, ndipo akajibu, “yah, ni muhimu sana.  Tulipokuwa kwenye discussion mshikaji aliondoka na funguo yangu kwa bahati mbaya.  Nd’o naiendea.”

“Utajali kama badala ya kuhangaishana na daladala nikajitolea kukupeleka?”

Hapo tena Maulid akasita, lakini sasa akiwa ameweka tahadhari ya kutosha kichwani mwake, akaendelea kujibu.

“Hapana bro.  Nashukuru sana kwa ofa yako.  Nitafurahi kama nitakwenda mwenyewe.”

“Sawa.  Pia nami ningefurahi sana endapo ungeipokea ofa yangu.  Wewe ni mdogo wangu, lingekuwa jambo la heri kama ungeupa uzito msaada wangu.”

“Pamoja na hayo…”  Maulid akauinua uso wake na kumtazama Benito aliyekuwa amemkazia macho yeye muda wote.  Benito akayapeleka macho yake pembeni.  Tendo hilo likamjaza Maulid nguvu ya kuendelea.

“Ninakokwenda hawajawahi kuniona hata siku moja nimekwenda na gari, na wanafahamu fika kwetu hakuna gari.  Bro, huoni leo nitatafsiriwa vingine tofauti na vile nilivyo siku zote?”

“Lakini ndugu yangu Maulid….”  Hapo Benito akawa anajaribu kuzungumza kwa sauti ya chini lakini yenye ushawishi.  “Huoni kuwa kutowahi kwako kwenda na gari bado hakuwezi kuwa kizuizi kwa wewe leo kwenda na gari?”

“Wananifahamu mimi siyo mtu wa hadhi hiyo.”

“Siyo suala la hadhi.”

“Bali?”

“Ni suala la wakati.  Hayo unayoyazungumza ni wakati uliopita.  Wakati uliopita hauwezi kutumika kama kigezo cha jambo fulani kwa wakati uliopo.”

“Sawa nimekuelewa bro.  Lakini at the end bado nitakwenda mwenyewe kwa daladala.  Hivyo ndivyo ninavyopenda kufanya.”

Benito akayainua macho yake na kumkazia Maulid ambaye hakujishughulisha na kukwepesha macho yake.  Benito akawa anajaribu kupambana na hasira iliyoanza kuwa dhahiri usoni pake.

“Eti, Maulid…:”

“Naam!”

“Kuna kitu unajaribu kunificha?”

“Sina jambo la kukuficha bro.

“Unadhani una akili nyingi sana, siyo?”

“Ah!  We vipi?  Maulid akashindwa kutuliza akili yake.

Maulid ni kijana anayejiamini sana anapokuwa anazungumza na mtu yeyote.  Ni mara chache mno humtokea kuvamiwa na hofu.  Ni makini sana kupangilia hoja anapozungumza.  Shuleni amekuwa aking’ara daima katika midahalo mbalimbali ya masomo ya Historia na Lugha.  Ujasiri wake ulimfanya akiubalike zaidi na wanafunzi wenzake, na walimu pia akiwamo Hafsa mwalimu wao wa somo la Historia.

Maulid alipoona Benito anataka kumburuza, naye akaghafirika.  Hata hivyo akawa amefanikiwa kuituliza akili yake haraka na kuzungumza kwa ujasiri. “Sikiliza bro.  We’ umekuja shuleni kwetu u mgeni.  Sikujui hunijui.  Si ndiyo?”

“Yah!”

“Umehitaji msaada kwangu.  Nami nikaondokea kukuamini japo sifahamu haswa dhamira yako kwa mwalimu Hafsa ni nini.  Lakini pia ukaniambia ni jukumu langu kuridhia kama nipo tayari kukusaidia ama lah.  Nakosea?”

“La hasha.”

“Nikaridhia kukusaidia. Ukanipa maelekezo uliyoyaona ya muhimu.  Tukamalizana tukaagana…”

“Lakini bwa’mdogo…”

“No.  Subiri nimalizie”

“Ok.  Endelea”

“Enhee!  Kukutana kwetu hapa kumetokea kwa bahati mbaya.  Nilikuwa na uhuru wa kuukataa wito wako.  Nimekuheshimu, nimeitikia, nimekuja kukusikiliza.  Matokeo yake unakuwa mkali kwangu kwa mambo yasiyo na msingi.”

Benito akafahamu kuwa Maulid keshakasirika.  Ikamlazimu kuwa mpole, “ok.  Nimekubali mdogo wangu.  Tafadhali niwie radhi.”

Anyway, kwangu siyo tatizo.  Niruhusu niende, muda umekwenda sana.”

“Nashukuru sana kwa muda wako.  Leo ni Jumatatu, tafadhali nitafute Ijumaa jioni endapo utapata wasaa.  Tutayazungumza haya mambo kwa kirefu.”

“Sawa hakuna noma bro.”

Thanks.

Maulid akainuka kitini na kuelekea moja kwa moja kupanda daladala.  Akiwa garini aliweza kumwoina Benito akiendesha gari lake taratibu kuondoka eneo hilo.  Mambo mengi yakawa yanamzonga Maulid kichwani mwake.  Akatamani kufahamu kilichomo ndani ya haya mambo.

Alipofika nyumbani kwa mwalimu wake, alimkuta Hafsa kaketi barazani akionekana kutokuwa na raha kabisa.  Nyumba aliyokuwa akiishi mwalimu Hafsa ni kama hatua hamsini hivi baada ya kulipita kanisa la Kilutheri la hapo Kisukuru.  Nyumba hiyo ilikuwa na mandhari ya kupendeza kutokana na kusheheni maua tele na miti kadhaa ya vivuli.  Veranda la nyumba hiyo pia lilipambwa kwa vyungu kadhaa vya maua.  Urembo wa Mwalimu Hafsa na uzuri wa mandhari ya nyumba vilififishwa na hali ya unyonge aliyokuwa nayo.

Maulid alisimama kando kidogo ya Hafsa.  Hakuzungumza neno lolote.  Aliingiwa na huruma kumkuta Hafsa katika hali ile.  Akaanza kuhisi jambo lililo mbele ni kubwa kuliko alivyokuwa akilikadiria yeye.  Alizama kwenye lindi la mawazo hadi alipogutushwa na sauti ya mwalimu Hafsa.

“Ooh!  Maulid mdogo wanguu, umekuja.  Karibu ndani.’’

“Hapa hapa panatosha.”

“Haya baba.  Kama nafsi yako i radhi.  Leo wapendelea nini?  Juisi ama soda?”

“Chochote dadaangu.”

“Halafu kila siku nakukataza kusema chochote bwana.  Haya ngoja nikupe soda.”

Mwalimu Hafsa akaingia ndani.  Si punde akatoka akiwa na chupa ya Pepsi kwenye sinia dogo lenye nakshi ya kupendeza sana.

“Karibu kakaangu.  Sijakuletea glasi najua unapenda kupiga tarumbeta.”

“Wala usikonde.  Kwa kiu niliyokuwa nayo, hapa umenipatia kabisa.”

“Enhee, dogo hebu niambie kilichojiri.”

Maulid akainywa soda yake mafundo kadhaa kisha akaiweka chupa chini.  Akaanza kumsimulia Hafsa yote yaliyotokea.  Alijitahidi kutobakiza chochote muhimu.  Mwalimu Hafsa akasikiliza kwa makini pasi kutia neno lolote hadi Maulid alipomaliza.  Kisha Mwalimu Hafsa akashusha pumzi kwa nguvu.

“Mmh, kazi ipo!”

“Kwani ni nini kisa sister?

“Maulid, we acha tu!”

“Nakuomba uniambie sister.  Unajua nami nakosa sana amani ninapokuona katika hali hiyo.”

“Wala huna haja ya kukosa amani dogo.  We’ nenepa tu.  Hakuna lolote la kutisha babaangu.”

“Sister usinipe moyo kwa vitu vilivyo naked kabisa.”

“Tuliza moyo mdogo wangu.  Naomba uniache niweke vema akili yangu.  Itakapotulia nitakwambia, usiwe na haraka.”

Mara wakasikia hatua za mtu akitembea kuelekea mahali walipo wao.  Wote wawili wakashtuka na kutazamana pasipo kuongea neno lolote.  Na mtu huyo alipojitokeza mbele yao, wote wakaishiwa nguvu.

…………..itaendelea

Na Fadhy Mtanga

Mtanga ni mwandishi wa riwaya anayepatikana Dar es Salaam. Unaweza mfatilia katika mtandao wa Twitter kupitia: @FadhyMtanga 

2 Comments

  1. Hans Amanyisye says:

    Dah kazi imeanza….safi Bro

Leave a Comment