AYA MOJA: Dengue ndo pacha wa malaria?

Mbu

Mara homa kali,
Mara joto kali,
Mara maumivu makali,
dengue, ndo pacha wa malaria?

Twaambiwa dawaye panadoli,
Yani homa kali unatibu kwa panadoli?
Au ndo mwatugeuza sie midoli?
Dengue,ndo pacha wa malaria?

Dalili ni kama za malaria,
kuenezwa na mbu kama wa malaria,
Ila haiponi kwa “diclo” za malaria!?
Dengue,ndo pacha wa malaria?

kujikinga ua mazalia ya mbu,
Mchana usikae palipo na mbu,
Na usiku pulizia dawa ya mbu,
Dengue,ndo pacha wa malaria?

Nasikia dokta bingwa umemuondoa,
inamaana panadoli haikumuokoa??
Na lini anazikwa tuje kudondoa?
Dengue,pacha wa malaria?

Umeshayasikia ya malaysia?
Mbegu za papai ndo zinawasaidia!
zinawakinga kwa asali kuchanganyia!!
Dengue,pacha wa malaria?

Dengue isiwe kiini macho,
dengue isitusahaulishe tutakacho,
Dengue isiikumbe katiba ya kizazi kijacho,
Dengue,ndo pacha wa malaria?

Ukilala lala,dengue!!
Ukichoka choka,dengue!!
Hadi ukicheka cheka,dengue!??
Dengue,ndo pacha wa malaria?

Dengue kaingia mjengoni,
wanashindwa kuutaja hakyanani,
Mara Denge,Dengu,Dengi sijui nini,
Dengue,ndo pacha wa malaria?

Tuambieni ugonjwa umeanza lini?
Kama tangu zamani,tathmini ya nini?
Au mtaunda tume kula kodi zetu jamani?
Dengue,ndo pacha wa malaria?

Haya wale wenzangu wa misimu,
wakina MC Dengue time imeshatimu,
Imbeni kuhusu Dengue kama mu timamu,
Dengue,ndo pacha wa malaria?

Na Naamala Samson

Samson ni Makamu Mwenyekiti wa shirika la TYVA.

Leave a Comment