Unaogopa sauti yangu?

shairi 3Kwani ni nani aliekuambia kua sauti yako inaweza kutusemea sote?

Au ni unyororo wake unaokufanya ufikirie mimi ni mdhaifu?

Unaogopa maumbile yangu?

Unono wa kifua changu, na upana wa nyonga yangu?

Hata kwa mtazamo naonekana shupavu,

Ushujaa sio mabavu!

Mwendo wangu wa mnyato, mithili ya simba jike,

Lakini pamoja na nguvu zangu,

Natumia kalamu, sio mateke.

Unaogopa kuumia?

Au ndio unamlipiza Mola kisasi

 kumnyofoa Adamu ubavu?

Kwa hiyo ndio kila siku unataka kunipiga ngumi za mbavu!!!!!

Kwani ni nani aliyekuambia kua alifanya makosa?

Kama alikua anataka ubabe,

Basi si angenyofoa  unyayo ili kila siku

tukanyagwe! Tukanyagwe!

Usingizi si nusu kifo, hebu fungua macho!!!

Ung’avu wa sura yangu haifanyi  yako kua hafifu.

Tusiogope usawa jamani!

Mama akiwa mwerevu hakumfanyi baba mbumbumbu,

Wala hakuna kinachopungua mwendawazimu akipoteza kumbukumbu,

Tuache mambo ya juzi,

Tusisingizie utamaduni, wala vitabu vya dini.

Hakuna kulikoandikwa kua kaskazini yazidi kusini.

Tumegawanyika sawa, nusu wewe, nusu mimi.

Mfalme hawezi potea kwa kumsikiliza malkia,

Tushirikishane kwenye maamuzi,

sisi sio ving’amuzi,

kila picha unayoleta, tunapokea!

Eti wewe mtoto wa kike, olewa tu!!

Shule ya nini.

We mama mjane, onewa tu!!

Nyumba wape.

We bibi kizee,  sogea huko!!

Hatakiwi kusikika.

 Hapana!

Sote tuna nafasi,

Kama vile jembe na mpini,

Moja halifanyi kazi bila jingine,

Kama vile jembe na mpini,

Mwanamke hafanyi kazi bila mwanaume,

Na mwanaume hafanyi kazi bila mwanamke

Tulete mabadiliko,

Tukubali mabadiliko,

kuanzia sehemu za kazi, hata huko majumbani,

Kubali mabadiliko,

Ongeza Kasi,

Mtu mke, mtu mume,

Sote tu sawa.

Na Neema Komba

Neema is a poet and author of the book “See Though The Complicated”

6 Comments

 1. gift oscar says:

  its gud..

 2. Churchill Shakim says:

  mashallah

 3. Ado Shaibu says:

  wat a superbly crafted work! keep it up.

 4. Chikulupi Kasaka says:

  Love it.

 5. Antonia says:

  I love it, u nailed it once again in kiswahili.

 6. Ramadhani says:

  This piece is amazing!!

Leave a Comment