Mlioingia kwenye mabaraza msiende kubarizi!

Katiba

“La Mgambo, La mgambo!” mbiu ikalizwa,

Kwa makeke jipembe likapulizwa,

Kijiji kikaamka likasikilizwa,

Likalia siku nzima bila kukatizwa,

Ha!kumbe ni suala zima la katiba,

Wananchi watoe maoni kupata mpya katiba,

Lakini wengine wakawa hawajui ni nini maana ya katiba?

Wengine wakadhani ati ni mtu ndo aitwa katiba!

Wakasema “tumemchoka katiba huyu, tunamtaka mwingine!”

“Aje atuongoze kwa staili nyingine, kivingine!”

Au walipotoshwa hawa pengine?

Mana’ke kila mjanja hutoa maana nyingine!

Maoni yakatolewa na kupokelewa,

Mchakato ukaendelea taratibu zikatolewa,

Kuwa mabaraza yataundwa na watu watachaguliwa,

Vijana,wazee,wanawake, walemavu wakasisitiziwa,

Nao damu hawakuilaza kwa barua kuziandika,

Viongozi wa Kata vikao vikakalika,

Kuchuja na kura zikadondoka ili mchakato kukamilika,

Mabaraza yakaundwa kila wilaya husika,

Sasa mlioingia mabarazani niwaambieni,

Kila mtu aweke uzalendo kwake moyoni,

Sio kujali eti yale marupurupu ya vikaoni,

Na kusahau aliyoyatetea mwanzoni,

Kumbukeni mmeingia sio kubarizi,

Wala sio katiba kuidarizi,

Bali kupata itakayofaa vizazi hata vizazi,

Imani yangu kwenu kuifanya vema kazi.

Na Naamala Samson

Samson ni Makamu Mwenyekiti wa shirika la TYVA.

Leave a Comment