Bunge lirekebishe sheria ya hifadhi ya jamii na kuomba radhi umma

Tunaendelea kuwasikiliza wabunge wakijishaua na kujaribu kusaka ushajaa baada ya kupitisha sheria katili dhidi ya wafanyakazi inayozuia mafao ya kujitoa. Dhambi imebuniwa na mamlaka mpya ya kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii. Hakuna mantiki inayotosheleza kuhalalisha zuio la mafao ya kujitoa.

Ieleweke hii ni mifuko ya hifadhi ya jamii na sio ya kustaafu. Tunaamini menejimenti za mifuko hii zinapaswa kubuni mafao ambayo yatahamasisha wanachama wake kuweka fedha katika mifuko hii kwa muda mrefu. Ikiwa mfanyakazi ataona kusubiri hela yake kwa miaka 20 kutampa fedha nyingi zaidi badala ya kuzichukue leo afanye hivyo kwa hiari yake. Kama mifuko inafuata kanuni za uwekezaji na za kushikilia pesa, wanachama wangelewa na sio kukimbilia sheria.

Takwimu za kiwango cha kusitisha ajira (staff turn-over) hakizidi wastani wa asilimia nane. Jaribio la mashirikia ya fedha kupigania sheria hii inashangaza na kuzua shaka. Kama fedha za wafanyakazi ziko Salama. Ni kama wanapigania kila shillingi. Tunashawishika kuamini menejimenti za mashirika ya hifadhi za jamii zimeshindwa kusimamia mifuko hii. Wamefanya maamuzi mabaya katika uwekezaji na wameshindwa kusimamia ufanisi. Gharama ya uzembe na udhaifu wa menejimenti za mifuko hazipaswi kubebwa na wafanyakazi.

Wafanyakazi wa kizazi kipya wanafanya kazi kwa malengo. Sehemu kuwa wanajiwekea kikomo cha utumishi ila hatimaye wafanye maradi binafsi au kuwa wawekezaji. Kuondoa mafao ya kujitoa ni kudhibiti uwekezaji. Mawazo ya kihuni kwamba wafanyakazi wakipewa hela mapema watatumbua ni ya kupuuzwa na yana lengo la kuwazalilisha, hayavumiliki!

Mfanyakazi alieamua kusitisha ajira akiwa ana miaka arobaini akiamua kizifungia fedha zake benki kwa miaka kumi na tano atavuna zaidi kuliko kuzichimbia kwenye mashimo ya mifuko ya jamii. Ndio maana tunasema kipengele kinachozuia mafao ya kujitoa ni wizi. Ni wakati muafaka wa kuruhusu na kuhalalisha mifuko binafsi ambayo itakuja na mafao bora itakayowaneemesha wafanyakazi.

Tulitarajia mamlaka mpya ya kusimamia mifuko ya jamii ingeanza kusimamia mifuko hii katika kuhakisha mifuko inatoa huduma bora kwa wanachama wake na kubuni mafao bora zaidi na sio kugeuka kuwadi na kibaraka wa mifuko ya jamii.

Kuondolewa kwa mafao ya kujitoa kumefanywa pasipo kuzingatia wastani wa umri wa kuishi wa mtanzania, aina mbalimbali za mikataba iliyobainishwa katika sheria ya mahusiano ya kazi ya miaka 2004 na mahitaji ya jumla ya wafanyakazi kwa wakati huu.

Mamlaka ya hifadhi ya jamii bado ina kazi kubwa kuhakikisha makampuni na taasisi zote zimesajili wafanyakazi kwenye mifuko hii na zinapeleka michango ya kwa wakati na kwa mujibu sheria. Tunaelezwa uchumi unakuwa hivyo ajira zitaongezeka na wachama watakuwa wengi zaidi hofu ya mifuko hii inatoka wapi? imefilisika?

Hakuna ushajaa wowote kwa wabunge kwa kufanya marekekebisho ya sheria husika. Hilo ni jambo la lazima. Wamefanya uzembe na kulisababishia taifa hasara. Kila dakika ya bunge inawagharimu walipa kodi mamilioni. Kupitisha sheria mbaya kisha kupigania marekebisho ni hujuma kwa ustawi wa taifa.

Tunajifunza kwamba udhaifu wa bunge umeshirikiana uzembe wa menejimenti za mashirika ya hifadhi za jamii kumuangamiza mfanyakazi. Bunge lirekebishe sheria hii na kuomba radhi umma kwa uzembe. Wamesababisha hasira, misongo na hali tete kwa sehemu kubwa ya nguvu kazi na hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa ufanisi na uzalishaji.

Vyama wa wafanyakazi na waajiri navyo havikuelimisha wanachama wao na wameshindwa kutetea na kulinda maslahi mapana ya wateja wao.

Tujirekebishe!

Na Eric Ongara

Eric ni mwanaharakati anayepatikana Dar es Salaam

4 Comments

 1. agnes says:

  ukweli fao la kujitoa ni muhimu kwa kila mwanachama kwani si wanachama wote wanakuwa na uwezo wa kufikisha umri wa miaka 55 na isitoshe watanzania wengi wanategemea kufanya kazi kwa mda mfupi ukilinganisha na ushindan wa sekta za serekali ombi lango fao la kujitoa lirudishwe halihusiani na serekali wala nini? hivyo bunge li jadili swala la mshahara na si swala ma mifuko ya wanachama

 2. Mimi ni Mhanga.Niliachishwa kazi mnamo 30/07/2012 na nilipokwenda NSSF kufuatilia mafao yangu niliambiwa mpaka nitimize miaka 55.Kwa kweli huu ni Wizi,Dhuluma na Ufisadi wa hali ya juu kabisa ktk Nchi hii.Sijaona Serikali ya kipumbavu kama hii pesa zangu ni halali yangu,nimezilipia kodi kama sheria inavyosema.Hii haiwezekani kabisa.Tunataka Fao la kujitoa lirejeshwe kwenye mifuko hii la sivyo iko siku Amani ya Nchi hii mtaitafuta Ndani ya Mifuko yenu Hamtaiona,pia ndani ya matumbo yenu yasio na shukurani Wajaa laana ninyi msiojua vibaya mnaotaka kila panapo Shilling ya Mtanzania basi ninyi mfanye Dhuluma.Mimi sasa hivi sina kazi,watoto wangu Wanne wamefukuzwa shule,maisha yangu yamekuwa si ya uhakika kabisa kwacha hakuchi kwasababu tu ya Dhuluma zenu.Nasema iko siku.Nyama kabisa ninyi.

 3. Eric Ongara says:

  Asante kadulyu. Nakubaliana nawe. Tunahitaji kuonganisha nguvu na kusukuma mabadiliko makubwa ya kimfumo.

 4. kadulyu says:

  Ndugu Eric,

  Nimetiwa moyo sana na maoni yako. Tunahitaji kuweka mikono yetu pamoja kubadilisha mifumo ya nchi hii nina maana ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

  Bunge wanafanya mchezo mbele ya wananchi. Inadhihirisha wazi kuwa wengi wao wanaenda pale kwa maslahi yao binafsi na si kuwatetea wananchi na ndiyo maana wengine wanataka hata bunge lisirushwe live kwenye luninga. Wanataka wafiche uzembe wanaoufanya pale mjengoni. Wanalala, wanatoroka wanasema mambo ya ovyo yasiyo na tija kwa wananchi waliwatuma na taifa kwa ujumla. Inaonekana hata wao wabunge wamepoteza imani na mfumo mihimili yote mitatu. Hawaoni umuhimu wa kuhudhuria vikao, kusoma miswaada inayoletwa na serikali kwa ukamilifu.

  Niliwa kusimamia mradi wa kuimarisha uwezo wa makatibu na makarani wa wabunge ili wawasaidie kuielewa miswada na kuchanganua hatimaye watoe michango ya maslahi kwa taifa, lakini kilichokuwa kinafukuziwa ni posho ya vikao na masurufu ya safari, na siyo content ya programu. Wabunge wanapigania kuchagulia ili hatimaye wawe mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wajumbe wa kamati za kudumu (za kisekta), wajumbe na wenyeviti wa board na kadhalika. wakishindwa kupata hivyo vyeo basi wao huona miaka mitano kama vile jela. Nasema wengi wako hivyo na mfumo mzima wa bunge hauko kwa ajili ya maslahi ya wananchi bali kupiga muhuri maamuzi ya serikali.

  Juzijuzi Mh. Filikunjombe alikuwa akihojiwa na BBC akasema Bunge letu limeshindwa kazi. Limeshindwa kuishauri na kuisimamia serikali. Serikali inawatisha wabunge walio wengi kwamba wasipoitetea watafukuzwa kwenye chama. Hivyo wameamua kunyamaza ndiyo maana miswada kandamizi kama hii inapitishwa. Inabidi wananchi tuamke na kuwaonya waache tabia hii. Wapo kwa ajili yetu, inashangaza wanaposhindwa kututea na badala yake wanatetea watu wachache wenye maslahi binafsi. Utakuta Dodoma wakati wa bunge imajaa wafanya biashara na ‘wawekezaji’ wakitongoza wabunge wetu wapate upendeleo fulani kwenye maamuzi ya serikali. Inatisha kuwa na bunge la namna hii.

Leave a Comment