Tukomeshe ukatili huu dhidi ya wanawake

Mwanamke ni nguzo kubwa na muhimu sana katika maisha na maendeleo ya mtu binasfi, jamii na taifa kwa ujumla. Mwanamke ndio nguzo mama katika uzalishaji na ujenzi wa taifa katika kuongeza rasilimali watu na pato la taifa katika nyanja za uchumi hasa kilimo. Mafanikio yoyote yapatikanayo katika taifa na kwa mtu binafsi basi nyuma ya mafanikio hayo lazima yu mwanamke.

Mwanamke ndio mlezi mkuu wa familia na jamii. Jamii inapokuwa na maadili mema basi juhudi na kazi kubwa imefanywa na mwanamke akishirikiana na mwanaume.

Licha ya umuhimu mkubwa alionao mwanamke katika maisha ya kila siku ya mwanadamu, jamii na Taifa, mwanamke hapewi umuhimu mkubwa katika jamii hasa katika mtazamo wa usawa. Siku zote tunaamini kuwa binadamu wote ni sawa kati ya mwanamme na mwanamke.

Hii inatokana na Maazimio na maandiko mbalimbali ya kisheria kama Tamko la Ulimwengu Juu ya Haki za Binadamu ya1948, Mkataba wa Afrika Juu ya Haki za Binadamu ya 1968. Katiba za nchi mbalimbali kama sheria mama zinatambua kuwa binadamu wote ni sawa.  Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Sehemu ya Tatu ibara ya 12 inatamka kuwa binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa.

Ukatili mkubwa unaofanywa siku hizi ni ukatili dhidi ya wanawake. Ukatili huu kwa kiasi kikubwa humuathiri mwanamke kimwili na kisaikolojia. Hivi karibuni vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake vimeshamiri kwa kasi ya ajabu. Vitendo hivi vya ukatili ni pamoja na kupigwa, udhalilishaji toka kwa wanaume, ubakaji, ndoa katika umri mdogo na ukeketaji.

Vyama mbalimbali vya wanawake Tanzania vinapigania sana kutokomeza unyanyasaji, udhalilishaji na ukandamizaj wa wanawake. Vyama kama TGNP, TAWLA, TAMWA na vinginevyo vinapigania sana haki ya kikatiba ya ibara ya 12 hasa ibara ndogo ya 2 inayosisitiza stahili ya heshima na kutambuliwa utu wa kila mtu hasa haki ya mwanamke.

Thamani ya mtu ipo katika utu wake. Hivyo wanawake daima wanapigania heshima ya utu wao. Makala hii inapinga vikali ukatili na udhalilishaji wa wanawake toka kwa wanaume wao. Tunasema maendeleo ya mwanaume yanachangiwa kwa asilimia kubwa na mchango wa mwanamke.

Bibi Aisha (si jina kamili), mkazi wa Mbulu wilayani Babati mkoani Manyara, ni mmoja wa waathirika wa ukatili mkubwa dhidi ya wanawake. Alipatwa na mkasa wa kugongwa na gari na mumewe na kisha kufungwa chini ya gari na kuburuzwa umbali wa kilometa 1 mpaka mahali panapofahamika kama sokoni. Mama huyu alipata madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kuvunjika mguu, kuvunjika mbavu saba na majeraha makubwa mgongoni yaliyotokana na ngozi yote kutoka mpaka kusababisha nyama na mifupa ya ndani kuonekana.

Huu ni ukatili uliopitiliza ambao haulingani na kosa lolote kustahili adhabu hiyo kwa binadamu mwingine. Hii yote inatokana na mfumo dume unaoamini kuwa ukioa mke ni mali yako na unaweza fanya chochote juu yake.

Ukatili kama huu ulitokea miaka kama miaka huko nyuma mkoani Mara ambapo mwanamke alipigwa na mumewe na kitwangio wa kinu mpaka kumvunja kabisa miguu yake yote miwili. Mpaka taarifa yake inatolewa kwa umma tayari alikuwa ni kilema asiye na miguu. Kisa kifananacho na hiki kilitokea pia Kilosa mkoani Morogoro ambapo mwamume alimcharanga mkewe mapanga manne sehemu ya kichwa na mgongo. Watendaji wa makosa haya wote hukimbia baada ya kutenda makosa haya na kuona kuwa hatua za dhati zinachukuliwa juu yao.

Vitendo hivi ndivyo mara nyingi vinafanya wanawake wawekwe katika kundi maalumu katika jamii. Hii inatokana na kwamba kuna uonevu mkubwa ambao unafanya usawa ukapotea katika jamii. Mila potofu, unyanyasaji na udhalilishaji wa wanawake, ukosefu wa elimu, huduma duni za jamii vyote hivi huzidi kumweka mwanamke nyuma na kuonekana kuwa na mahitaji maalumu katika jamii ili japo kuwepo na usawa wa kijinsia.

‘Tanzania itaendeleza kwa vitendo kampeni ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ya kupiga vita ukatili dhidi ya wasichana na wanawake katika Bara la Afrika inayojulikanayo ‘Afrika tuungane kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana’.  Rais Jakaya Kikwete, aliyasema hayo wakati wa hafla fupi ya kuwaaga watu 75 kutoka nchi 36 za Afrika, wanaopada Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kupaza sauti zao kupinga ukatili dhidi ya wasichana na wanawake.

Sheria zinazokemea udhalilishaji wa kijinsia na ukatili wa wanawake zipo. Hivyo serikali inashauriwa kuzisimamia sheria na kutumia vyombo vya dola kuhakikisha Tanzania ina mazingira salama na ya usawa kwa watu wote. Naiomba serikali itekeleze kwa vitendo sera na kampeni zake juu ya kuondosha unyanyasaji wa wanawake nchini.

Na Chikulupi Kasaka

Kasaka ni mwanasheria anayeishi Dar es Salaam

Leave a Comment