Mapinduzi au vita ya mafuta ya Libya?

Wananchi wanao ongoza mapambano kumng'oa Gaddafi

Siyo wote waliao sana msibani wana uchungu na marehemu bali wengine wanasema bora kaenda. Kwa mantiki hiyo, sidhani kama ni kweli mataifa kama Marekani, Uingereza na washirika wengine wote wa NATO wana uchungu na wananchi wa Libya au bara la Afrika kwa ujumla.

Baadhi ya matendo yao yamekuwa kwa manufaa yao binafsi.

Ikumbukwe hawajaanza leo matendo ya uvamizi na kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Toka vita ya pili ya dunia, ambacho ilikuwa kipindi pia shirika la kijasusi la Marekani “Central Intelligence Agency-C.I.A lilianzishwa likiwa na kazi kubwa ya kujihusisha na ufatiliaji na uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi nyingine wakitumia kivuli cha mashirika ya misaada, kazi za kujitolea, balozi zao nk

Mtindo huo umegawanyika katika sehemu kuu mbili za kioperesheni yaani; operesheni aina ya “covert” na operesheni aina ya “overt”.

Operesheni aina ya “Covert” ni uvamizi au uingiliaji wa mambo ya nchi nyingine kwa kufuata sheria na taratibu zote halali. Mfano mzuri ukiwa ni uliofanyika kwa C.I.A kuingia Pakistani kumsaka Osama Bin Laden. Serikali ya Pakistan haikuwa na taarifa yoyote juu ya operesheni hiyo maalum ya C.I.A.

Lakini mtindo wa operesheni aina ya “overt” kama endapo nchi ya Marekani kupitia vyombo vyake vya kijasusi ingeishirikisha serikali ya Pakistani katika operesheni ya kumsaka Osama.

Lengo la makala hii si kufunua namna ambavyo taasisi za kimarekani kama CIA vinavyofanya kazi lakini hasa kuangalia namna ambavyo mataifa ya kimagharibi yanavyoweza kutumia umoja kama Umoja wa Mataifa (UN) kupitia kura ya turufu kuitawala dunia.

Kutawala huku dunia kunarejesha ukoloni yaani ukoloni mamboleo katika nchi changa kama nchi za kiafrika na asia.

Kwa wafuatiliaji wa kina wa masuala haya ya vita hizi zinazosimamiwa na mataifa ya kimagharibi, hakika watakiri vita ya Iraq ilikuwa vita ya mafuta na kulipiza kisasi.

Nani asiyejua kuwa chokochoko za wamarekani dhidi ya taifa la Iran chanzo kikuu ni mafuta?

Kwa upande mwingine, nani asiyefahamu vita vya wenyewe kwa wenyewe katika lililokuwa taifa la Sudan, sasa Sudan na Sudan ya Kusini sababu kuu ni mafuta?

Je nani asiyejua kuwa vitavya nchini Kongo (DRC) sababu kuu ni uwepo wa madini?

Orodha ya nchi ni ndefu zenye migogoro na vita kama Angola kipindi cha nyuma, Afghanistan kwa sasa na nyingine nyingi zikiwa chanzo kikuu rasilimali za madini na mafuta kwa upekee.

Rais Muammar Gaddafi

Kwa mazingira kama hayo na historia, kiongozi wa nchi ya Libya, Kanali Muammar Gaddafi anapigana na ukandamizaji wa mataifa ya magharibi bila ya woga? Anaendeleza kile ambacho alikuwa akikifanya hata hadharani mbele ya mataifa hayo katika mikutano kama ya Umoja wa Mataifa (UN).

Ikumbukwe Libya ilikuwa inauza mafuta yake kwa bei wanayoitaka wenyewe bila kufuata shinikizo la mataifa ya magharibi. Ikumbukwe Libya ni nchi inayoongoza katika uchimbaji wa mafuta barani Afrika.

Ni Gaddafi huyo huyo aliyekuwa kinara wa harakati za kuziunganisha nchi za Afrika. Wazo ambalo waasisi wa mataifa kama Mwalimu Julius Nyerere na Nkwame Nkrumah walikuwa nazo. Katika ulimwengu wa “wagawe watawale” mataifa ya nchi za kimagharibi hawapendi kusikia juhudi kama hizo zikifaulu.

Katika mazingira hayo, vita vinavyoendelea nchini Libya chanzo si udikteta wa kiongozi Gaddafi ambao wananchi wanataka kumuondoa. Kwani inatia mashaka kwanini nchi za magharibi zimekimbilia haraka sana kutoa misaada ya kivita na utaalamu kwa vikundi vinavyoendesha mapambano hayo.

Chanzo ni mafuta. Chanzo ni ujasiri madhubuti kusimamia hoja na kutokukubali kuyumbishwa. Kutokukubali kuendeshwa kwa sera za kimagharibi.

Na Seleman Kitenge

Bwana Kitenge ni mwandishi mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.

2 Comments

  1. suleiman mohamed says:

    kwanza nafurahi kuona kweli wa africa tupo wachache wenye nia thabiti na mwamko wa kweli juu ya bara letu,nimakala nzuri sana iliyo sheheni ukweli mtupu …..tunahitaji vijana kama hawa wengi katika taifa letu

Leave a Comment