Jicho letu Igunga!

Tayari hekaheka zimeanza kuzizima katika jimbo la uchaguzi la Igunga. Jimbo ambalo lilikuwa chini ya uwakilishi wa Rostam Aziz kwa zaidi ya awamu tatu na kwa uamuzi wake ambao ulisukumwa na kuchoshwa kwake katika siasa za maji taka akaliachia.

Vyama vinara katika siasa nchini yaani Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF) tayari vimeshazindua kampeni zao rasmi. Huku vikiwanadi wagombea wao katika nafasi hiyo ya ubunge yaani; Mwalimu Joseph Kashindye (CHADEMA), Dkt Peter Kafumu (CCM) na Leopold Mahona (CUF).

Lakini si vyama hivyo tu ambavyo vimesimamisha wagombea, kwani vipo pia vyama vingine kama SAU ambacho kinawakilishwa na John Maguna, Said Cheni (DP), Hemed Dedu (UPDP) na Stephen Makingi (AFP).

Vyama kama UDP, TLP na NCCR-Mageuzi ambavyo vina uwakilishi bungeni katika uchaguzi mdogo huo havikusimamisha wagombea hivyo kupisha mchuano katika vyama hivyo zaidi.

“Mchuano bado ni mkali sana ikiwa ni wiki za mwanzoni za kampeni, hivyo ni mapema sana kutabiri” alisema mchambuzi mmoja maarufu wa masuala ya siasa nchini.

Kwa namna ya kipekee, mbunge aliyejiuzulu yaani Rostam Aziz ambaye alidhaniwa angesusia kwenda katika kampeni hizo alishiriki katika uzinduzi wa kampeni wa chama chake hicho. Jambo ambalo kwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakiona kama ni mchezo wa danganya toto ukiendelea kuchezwa na wanasiasa hususan toka chama hicho cha CCM.

Uchaguzi huu ukiwa na joto kali la kisiasa, ikiwa haijafika mwaka tangu nchi itoke katika kufanya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 30, 2010. Unatoa mwanya wa kuendelea kudhihirisha nguvu kali ya kisiasa iliyojionyesha kwa chama cha upinzani cha CHADEMA ambacho kilifaulu kuongeza idadi kubwa ya wabunge kwa chama hicho.

Huku ikiacha maswali mengi kwa Chama cha Wananchi (CUF) kama itamudu kuibuka kidedea na kuonyesha bado ingali na mvuto na nguvu Tanzania bara.

Kwa upande wa CCM, je litakuwa anguko jingine yaani kupoteza jimbo ambalo awali lilikuwa limeshikiliwa na chama chao? Lakini zaidi, itaweza kuonyesha namna gani chama hicho kinaweza kuogelea katika dimbwi la kugubikwa na shutuma nyingi dhidi ya baadhi ya wanachama wake ambao wengine wanashika na waliwahi kushika nyadhifa za juu serikalini hususan wanachama hao wakiwemo katika eneo la mapambano kupigania chama chao.

Leave a Comment